DOHA-Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB) imehitimisha mkutano wake wa 11 wa mwaka nchini Qatar, huku ikitangaza rasmi kuwa Jamhuri ya Azerbaijan ndiyo itakuwa mwenyeji wa mkutano wa 12 mwaka 2027.
Katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika mwishoni mwa mkutano huo na kushuhudiwa na Waziri wa Fedha wa Tanzania ambaye pia ni mmoja wa Magavana wa Benki hiyo, Mhe.Balozi Khamis Mussa Omar,Waziri wa Uchumi wa Qatar, Bw. Al-Kuwari, alimkabidhi nyundo ya uenyekiti Gavana wa Azerbaijan, Bw. Mikayil Jabbarov, tukio lililoashiria kukamilika kwa uenyeji wa Qatar na kuanza kwa maandalizi ya mkutano ujao nchini Azerbaijan.
Gavana Jabbarov alieleza kuwa, Azerbaijan imejipanga vyema kuandaa mkutano huo, akibainisha kuwa nchi hiyo ina uzoefu mkubwa katika kuandaa mikutano ya kimataifa.
Alitolea mfano wa mkutano wa COP29 uliofanyika mwaka 2024 na mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu uliofanyika mwaka 2026 jijini Baku.
Kwa mujibu wa Gavana Jabbarov, mkutano wa mwaka 2027 utalenga kuimarisha ushirikiano katika nyanja za miundombinu, nishati safi, na miundombinu ya kidijitali huku akisisitiza kuwa Azerbaijan, ikiwa ni mwanachama mwanzilishi wa AIIB, inaona mkutano huo kama fursa ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi za Asia Afrika na Ulaya.
Rais wa AIIB, Bi. Zou Jiayi, alitoa shukrani kwa serikali ya Qatar kwa uenyeji wake na kuelezea matumaini yake kwa ushirikiano na Azerbaijan katika maandalizi ya mkutano ujao. Mkutano wa 2027 unatarajiwa kuwa na umuhimu mkubwa katika kuweka mwelekeo mpya wa maendeleo ya benki hiyo.
Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (Asian Infrastructure Investment Bank – AIIB) ni benki ya maendeleo ya nchi nyingi inayojitolea kufadhili Miundombinu ya Kesho, huku uendelevu ukiwa msingi wake.
AIIB ilianza shughuli zake mwaka 2016 na sasa ina wanachama 111 walioidhinishwa duniani kote, Ikiwa na mtaji wa Dola za Marekani bilioni 100 na kupewa daraja la AAA na mashirika makuu ya kimataifa ya kukadiria uwezo wa kuyafikia masoko ya mitaji ya kimataifa (credit rating Agencies), ambapo inashirikiana na washirika kuhamasisha mitaji na kuwekeza katika miundombinu na sekta nyingine zenye tija zinazochangia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kuuunganisha mtandao wa miundmbinu wa kikanda.







