BoT yaiheshimisha Tanzania huduma jumuishi za kifedha, yazoa tuzo tano Kimataifa

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imepata tuzo tano za utambuzi katika mkutano wa kimataifa wa Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (Alliance for Financial Inclusion-AFI) duniani, kutokana na hatua na mikakati mbalimbali iliyotekelezwa nchini katika kukuza huduma jumuishi za kifedha, kuimarisha usawa wa kijinsia katika huduma za kifedha na kuongeza ulinzi wa watumiaji.
Tuzo hizo zimetolewa katika mkutano wa AFI uliofanyika Papua New Guinea kuanzia Septemba 1 hadi 4, 2026 ambapo Tanzania iliwakilishwa na ujumbe wa Benki Kuu chini ya Gavana Emmanuel Tutuba.

Hayo yamesemwa leo Septemba 16,2026 na Meneja wa Huduma Jumuishi za Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania,Bi.Nangi Massawe wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za BoT jijini Dar es Salaam.

Bi.Massawe amesema,utambuzi huo unatokana na utekelezaji wa hatua mbalimbali ambazo Tanzania imekuwa ikichukua kupitia sera, mikakati na programu za kuimarisha ujumuishi wa kifedha kote nchini.

Amesema, AFI ni jumuiya ya kimataifa inayojumuisha zaidi mabenki makuu na wadhibiti wa sekta ya fedha kutoka nchi zinazoendelea ikiwa na wanachama kutoka nchi 84 na taasisi 90.

Meneja huyo amesema, jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kusaidia nchi wanachama kuweka na kutekeleza mikakati inayowawezesha wananchi kupata na kutumia huduma rasmi, salama na zenye manufaa za kifedha.

Amesema tangu kuanzishwa kwake, AFI imekuwa chombo muhimu cha kubadilishana uzoefu, kuweka sera na kufuatilia hatua zinazochukuliwa na nchi wanachama katika kuongeza ushiriki wa wananchi katika mfumo rasmi wa fedha.

Bi.Massawe amesema,Tanzania imepata tuzo ya kwanza katika kipengele cha Maya Declaration Award, ambacho hutambua nchi au taasisi zilizofikia malengo na ahadi walizojiwekea katika kuendeleza huduma jumuishi za kifedha.

Amesema,waliweka jumla ya ahadi 13 chini ya mpango huo na Tanzania kufanikiwa kutekeleza sita, huku hatua nyingine zikiendelea kufanyiwa kazi.

Miongoni mwa mafanikio yaliyotajwa ni Tanzania kufanikiwa kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha, ambapo kwa sasa nchi iko katika utekelezaji wa mkakati wa tatu.

Mkakati wa kwanza uliwekwa mwaka 2013, wa pili mwaka 2017, wakati mkakati wa tatu uliwekwa mwaka 2023 na unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano hadi mwaka 2028.

Amesema, hatua hiyo imeiweka Tanzania miongoni mwa nchi chache wanachama wa AFI ambazo zimefikia hatua ya kuwa na mkakati wa tatu wa huduma jumuishi za fedha.

Pia amesema kiwango cha ujumuishi wa kifedha nchini kimeendelea kuongezeka, kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi asilimia 76 mwaka 2023, huku vipimo vya ndani vinavyoendelea kufanyika vikionesha kuwa kiwango hicho kimefikia karibu asilimia 80.

Aidha, amesema idadi ya watu wazima ambao hawakuwa na huduma rasmi za kifedha imepungua kutoka takribani milioni 7.8 mwaka 2017 hadi milioni 6.4 mwaka 2022.

Hatua nyingine, amesema ni kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za kifedha ndani ya eneo la kilomita tano kutoka asilimia 86 hadi asilimia 89, huku matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya simu yakiongezeka kutoka asilimia 60 hadi asilimia 72.

Katika eneo la usawa wa kijinsia, Bi.Massawe amesema,pengo kati ya wanawake na wanaume katika upatikanaji wa huduma za kifedha limepungua kutoka takribani asilimia 10 mwaka 2017 hadi asilimia 3.2 mwaka 2022, huku vipimo vinavyoendelea kufanyika vikionesha mwelekeo wa kupungua zaidi.

Wakati huo huo, B.Massawe amesema, Tanzania pia ilipata tuzo ya Financial Inclusion Policy Achievement Award, tuzo inayotambua mafanikio katika kuweka na kutekeleza sera za huduma jumuishi za kifedha, hususan zinazolenga kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma kati ya makundi mbalimbali ya wananchi.
Bi.Massawe amesema katika eneo hilo, Tanzania imeweka mkazo maalumu kwa wanawake ambao kwa muda mrefu wamekuwa miongoni mwa makundi yanayokabiliwa na changamoto katika kupata na kutumia huduma rasmi za fedha.

Amesema,kupitia Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023–2028, Tanzania imeweka kipengele maalumu kinachohusu jinsia, kwa lengo la kuhakikisha wanawake wanafikiwa na huduma za fedha zinazozingatia mahitaji yao.

Aidha, juhudi zimefanyika katika kubuni bidhaa na huduma za kifedha zinazolenga mahitaji maalumu ya wanawake, kurahisisha upatikanaji wa huduma kupitia mawakala na huduma za fedha kwa njia ya simu, pamoja na kupunguza vikwazo vinavyotokana na mahitaji ya nyaraka.

Benki Kuu pia imeweka mwongozo kuhusu wakopeshaji wa kidijitali, uwazi wa gharama za mikopo na udhibiti wa gharama, huku hatua nyingine zikilenga kupunguza changamoto ya dhamana inayowazuia wananchi, hususan wajasiriamali wadogo, kupata mikopo.

Tuzo ya tatu iliyotajwa ni ya AFI Gender Inclusive Finance Champion Institution, ambayo Tanzania ilipata kutokana na utekelezaji wa hatua zinazolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika mfumo rasmi wa fedha.

Hatua hizo zimehusishwa na utekelezaji wa Denarau Action Plan, mpango wa AFI unaolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika mfumo rasmi wa fedha na kupunguza pengo la kijinsia katika upatikanaji na matumizi ya huduma hizo.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa, Bi.Massawe amesema, ni kuweka malengo mahsusi ya kuwafikia wanawake, kutumia takwimu zilizogawanywa kwa jinsia katika kupanga sera, kubuni bidhaa zinazokidhi mahitaji ya wanawake na kupanua huduma za kifedha kupitia mifumo ya kidijitali.

Benki Kuu pia imekuwa ikisisitiza matumizi ya takwimu zilizogawanywa kwa jinsia kutoka taasisi za fedha ili kurahisisha upimaji wa maendeleo ya wanawake katika mfumo rasmi wa fedha.

Aidha, hatua zimechukuliwa kupunguza vikwazo vya kisheria na kiudhibiti vinavyoweza kuathiri uwezo wa wanawake kumiliki mali, kufungua akaunti, kupata vitambulisho, kusajili biashara na hatimaye kupata mikopo na huduma nyingine rasmi za kifedha.

TUZO MBILI KWA WATENDAJI

Mbali na tuzo tatu za taasisi, watendaji wawili wa Benki Kuu walipata tuzo za Technical Leadership Awards kutokana na mchango wao katika maeneo mbalimbali ya huduma jumuishi za fedha.

Mmoja wao ni Dkt. Khadija Kishimba, Meneja wa Idara ya Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Kifedha aliyetambuliwa katika eneo la market conduct and consumer empowerment, linalohusu mwenendo wa masoko na uwezeshaji wa watumiaji wa huduma za kifedha.

Mwingine ni Nangi Massawe, Meneja wa Huduma Jumuishi za Fedha aliyetambuliwa katika eneo la uongozi wa sera za huduma jumuishi za kifedha.

Mafanikio hayo yameifanya Tanzania kupata tuzo tatu za taasisi na tuzo mbili za watu binafsi kupitia Benki Kuu.

Akizungumzia juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za fedha, Bi.Massawe amesema Benki Kuu imeanzisha programu za elimu ya fedha zinazolenga watu walio ndani na nje ya mfumo rasmi wa elimu.

Amesema,Benki Kuu imeingia makubaliano na baadhi ya vyuo vikuu nchini ili kuendesha programu za mafunzo ya elimu ya fedha, ambapo washiriki wanaopata mafunzo hayo huwezeshwa kwenda kutoa elimu kwa makundi mengine ya wananchi.

Mpango huo unalenga kutumia mfumo wa mfundishe mkufunzi, ambapo wahitimu wa mafunzo hayo wanaweza kwenda katika maeneo mbalimbali kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wakiwemo walioko vijijini na walio nje ya mfumo wa shule.

Aidha,mpango huo unalenga kuongeza wigo wa wananchi wanaofikiwa na elimu ya fedha bila kutegemea upatikanaji wa televisheni, redio au majukwaa mengine ya mawasiliano pekee.

Katika eneo la gharama za huduma za kifedha, Benki Kuu imeeleza kuwa, imeweka mwongozo wa gharama kwa watoa huduma za fedha kwa lengo la kuongeza uwazi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa gharama zinazofikika.

Amesema,mwongozo huo umeanza kutumika baada ya majadiliano kati ya Benki Kuu na watoa huduma za fedha. Benki Kuu pia imeweka msisitizo wa kuwafanya watoa huduma kuweka wazi gharama zinazotozwa katika maeneo ambayo huduma zinatolewa, ikiwemo kwenye kaunta, ili watumiaji waweze kufahamu gharama kabla ya kutumia huduma husika.
Hatua hiyo inalenga kuongeza uwazi katika soko la huduma za fedha na kusaidia wananchi kufanya maamuzi wakiwa na taarifa sahihi kuhusu gharama wanazotakiwa kulipa.

Kwa upande mwingine, Tanzania imeendelea kuangalia makundi yenye mahitaji maalumu, ikiwemo watu wenye ulemavu na watu waliolazimika kuhama maeneo yao kutokana na majanga na athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa kuweka mikakati ya kuwaunganisha na mifumo rasmi ya kifedha.

Hata hivyo, mafanikio hayo yanaendelea kuwa sehemu ya jitihada za Tanzania katika kupanua wigo wa huduma rasmi za kifedha na kuhakikisha makundi mbalimbali ya wananchi yanaweza kuzifikia na kuzitumia huduma hizo kwa usalama na manufaa katika maisha na shughuli zao za kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here