Mahakama ya Tanzania yakutana na wadau kutathmini utekelezaji wa mikakati ya mashauri ya kiuchumi

NA MARY GWERA,
Mahakama

MAHAKAMA ya Tanzania pamoja na Wadau wa Sekta ya Sheria na Uchumi wamekutana kufanya Tathmini ya Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara lengo likiwa ni kuboresha ufanisi katika mnyororo wa haki za kiuchumi sambamba na kuoanisha utendaji kazi na Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiongoza Mkutano kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.

Akifungua Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano- Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewasisitiza wajumbe wa Mkutano huo kuwa huru kutoa maoni na changamoto zilizopo zikiwemo zinazoigusa Mahakama ili kuboresha uwazi na uwajibikaji katika utoaji haki nchini.

“Mkutano huu una mambo mazuri tu yanayotusaidia kuboresha ufanisi katika maeneo yetu ya kazi kwa jinsi yanavyohusiana na kuuwiana na mnyororo wa haki jinai, haki inaweza kuwa ni haki jinai au katika muktadha wa kikao hiki cha mashauri ya kiuchumi. Kwahiyo nawashauri kwamba muwe huru kabisa mnavyoshiriki mkutano huu. Wengi wenu nawafahamu ninyi tu si kwamba ni viongozi, lakini ni wataalamu mahiri katika maeneo yenu, hivyo tunategemea kupata ushirikiano wenye tija kwa sababu ya uwepo wenu,” amesema Mhe. Masaju.

Aidha, Jaji Mkuu amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, umuhimu wa kiongozi haupatikani kwa Kiongozi kuwa ofisini pekee bali umuhimu wake unapatikana kwa huduma yake anayotoa katika jamii.

Mhe. Masaju amesema, nafasi na mchango wa Mahakama na Wadau katika utekelezaji wa majukumu ya kikatiba na kisheria katika muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni muhimu.

“Msingi Mkuu wa Dira hii ni Taifa Jumuishi lenye Ustawi, Haki na Linalojitegemea.Kwahiyo tunavyokaa hapa sasa pamoja na Mikakati hii tuliyokwishajiwekea tuweke au tupendekeze mikakati ya kutekeleza majukumu yetu ya kikatiba na kisheria katika muktadha wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo inamhususu kila mmoja wetu hapa. Kwa hiyo hiki kikiwa ni kikao cha tatu tunakutana ili kutathmini utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kushughulikia mashauri ya kodi, biashara, ardhi, mabenki na ushindani wa kibiashara,” ameeleza Jaji Mkuu.

Ameongeza kuwa, pamoja na kutathmini utekelezaji wa mikakati waliyojiwekea, Mkutano huo pia ni fursa ya kujadili masuala mengine yanayoweza kujitokeza baada ya kikao kilichopita na yale yanayoweza kujitokeza siku za mbeleni ambayo yanaweza kuathiri utekelezaji wa mikakati iliyowekwa katika utekelezaji wa majukumu ya Mahakama na Wadau.

“Mnapokuwa mmerejea katika Ofisi zenu muende mkayatekeleze haya lakini pia muwashauri viongozi wenu umuhimu wa kuyatekeleza hayo,” amesisitiza Mhe. Masaju huku akigusia juu ya umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi akirejea Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Mahakama inahimizwa kukuza usuluhishi na kuzikumbusha Taasisi nyingine kuwa, zinapaswa kwanza kutatua migogoro kabla ya kufikisha mashauri mahakamani.

“Naomba niwarejeshe katika mkakati wa sita na wa kumi katika mikakati yetu inayohusu utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi. Lakini pia kwa njia za kiutawala katika maeneo yetu ya kazi. Na hili sharti ni sharti la kikatiba linatokana na ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo Mahakama inapotekeleza jukumu lake la kutoa maamuzi katika mashauri ya madai na jinai inatakiwa pia kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya watu wanaohusika katika migogoro,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Picha za Wadau mbalimbali za Wadau wa Mkutano kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma akitoa neno la utangulizi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Kadhalika, Jaji Mkuu amekitaka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kupitia Mawakili wake kuwasimamia wateja wao kwa maadili na kuwashauri kutumia mifumo ya usuluhishi na mamlaka za udhibiti badala ya kukimbilia mahakamani. Hatua hiyo inalenga kuepuka gharama zisizo za lazima na mapingamizi ya kisheria (preliminary objections) lakini vilevile ni utekelezaji wa Kanuni ya 59 ya Kanuni za Maadili ya Mawakili, 2018 Tangazo la Serikali Na. 118 la 2018 inayoelekeza Mawakili kuwataarifu Wateja wao kuhusu uwezekano na faida za kumaliza mashauri kwa mfumo wa usuluhishi

Akizungumzia kuhusu Uhuru wa Mahakama na Usimamizi wa Sheria; Mhe. Masaju amesema, kwa mujibu wa Ibara ya 107B ya Katiba, Mahakama itaendelea kuwa huru na kusimamia sheria huku akibainisha kuwa, mashauri ambayo hayakufuata taratibu za awali za kupatiwa ufumbuzi kwanza katika mamlaka husika kabla ya kuzihusisha Mahakama yatarejeshwa kwenye mamlaka husika.

“Na sisi huku mahakamani tutaendelea kusimamia sheria kwa ufanisi ipasavyo. Kwa sababu hata hivyo ni sharti letu la jukumu letu la kikatiba katika ibara ya 107B kwamba katika kutekeleza majukumu yetu Mahakama itakuwa huru isipokuwa itazingatia tu masharti ya Katiba na Sheria za Nchi,” ameeleza Jaji Mkuu.

Kupitia mkutano huo, Mahakama na Wadau hao wataendelea kubainisha changamoto zilizosababisha ucheleweshaji au zinazosababisha ucheleweshaji wa usikilizaji wa mashauri ya kiuchumi na kuendelea kutekeleza ipasavyo mikakati iliyowekwa na mingine itakayokubalika katika Mkutano huo.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akitoa taarifa ya utekelezaji wa mikakati kwa upande wa Mahakama ya Tanzania wakati wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu akichangia jambo wakati wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe akichangia jambo wakati wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mkutano huo umehudhuriwa na Amidi wa Mahakama Kuu na Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Amir Mruma, Majaji Wafawidhi kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, Jaji Mfawidhi Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Wasajili wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu pamoja na baadhi ya Naibu Wasajili kutoka Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.

Wadau wengine waliohudhuria Mkutano huo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe na wengine kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wizara ya Fedha, Tume ya Taifa ya Mipango, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Msajili wa Baraza la Ushindani.

Wengine ni kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Umoja wa Mabenki (TBA), Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama, Baraza la Ushindani, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here