MWANZA-Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMATA) yanatarajiwa kuimarisha mshikamano, umoja na urafiki miongoni mwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini, huku wananchi wakipata fursa ya kujifunza na kushuhudia michezo mbalimbali.
Mashindano hayo yatafanyika jijini Mwanza kuanzia Septemba 21 hadi Oktoba 5, 2026, katika Uwanja wa CCM Kirumba, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo: “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kudumisha amani.”
Akizungumza wakati wa maandalizi ya ufunguzi wa mashindano hayo, Mwenyekiti wa BAMATA, Meja Jenerali, Said Hamis Said, amesema michezo hiyo ni sehemu muhimu ya kuwaweka wanajeshi na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama katika hali nzuri kiafya, pamoja na kuimarisha ushirikiano.
Michezo hiyo inashirikisha timu kutoka Kanda saba ambazo ni Kanda ya JKT, JWTZ, Ngome, Uhamiaji, SMZ, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Jeshi la Polisi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamduni, amesema ushiriki wa vyombo hivyo katika mashindano hayo unaonyesha mshikamano na umoja uliopo kati ya vyombo vya ulinzi na usalama nchini.





