NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Septemba 20,2026 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Dkt. Speciosa Wandira Kazibwe.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu,Bakari S. Machumu.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, viongozi hao wamezungumzia umuhimu wa mshikamano miongoni mwa viongozi wanawake na nafasi yao katika kuleta mabadiliko ya kijamii.
Aidha, wamejadili mchango wa viongozi wanawake katika kuhamasisha ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi na maamuzi, pamoja na kuchochea maendeleo endelevu katika jamii.
Dkt. Kazibwe alikuwa Makamu wa Rais wa Uganda kuanzia mwaka 1994 hadi 2003, na mwanamke wa kwanza barani Afrika kushika wadhifa huo.


