LINDI-Septemba Mosi, 2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Kilwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe.Carolyne Mtui (SRM) na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw.Naftal Mnzava limefunguliwa shauri la uhujumu uchumi Na.ECO.19495/2026.
Ni kati ya Jamhuri dhidi ya Bw. Salumu Mohamedi Kitengwike (35) ambaye alikuwa Meneja katika Chama cha Msingi cha Ushirika Matandu cha Kata ya Njinjo wilayani Kilwa.
Mshtakiwa anakabiliwa na kosa la ubadhirifu na ufujaji kinyume na kifungu cha 28(1),matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu 31 (2) PCCA Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2023.
Sambamba na kuisababishia hasara Matandu AMCOS kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi Aya 10, jedwali la kwanza, Sura ya 200 marejeo 2023, baada ya mshtakiwa kufanya ubadhirifu na ufujaji kiasi cha Shilingi 14,945,000.
Mshtakiwa kwa kipindi cha msimu wa ufuta 2024/2025 chama kiliingiziwa fedha za ushuru toka Chama Kikuu cha Lindi-Mwambao kiasi cha Shilingi 66,000,000 kupitia kikao cha bodi ya chama hicho kiliidhinisha kiasi cha Shiingi 44,945,000 kwa matumizi mbalimbali ya chama.
Mtuhumiwa baada ya kutoa fedha benki kiasi cha Shilingi 14,945,000 alitumia kwa matumizi yake binafsi.Baada ya kusomewa mashtaka yake, Mshtakiwa alikana shtaka na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya mahakama. Shauri limepangwa tena tarehe Septemba 16,2026 kwa ajili ya uwasilishaji wa hoja za awali (PH).
Tags
Habari
Mahakamani Leo
Matandu AMCOS
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania
