Mfanyabiashara Ayii Duang asema atatoa fedha taslimu kugharamia uchaguzi Sudan Kusini, lakini uchaguzi usipofanyika mwaka huu atazidai zote

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Sudan Kusini, Ayii Duang Ayii amesema, yuko tayari kulipa fedha taslimu ikiwa ni mchango wake wa uchaguzi Septemba 16, 2026, lakini ameonya kuwa atadai kurejeshewa fedha hizo iwapo uchaguzi uliopangwa hautafanyika.
Mfanyabiashara wa Sudan Kusini, Ayii Duang Ayii. (Picha na Mtandao).

Ayii ametoa kauli hiyo huku akisisitiza umuhimu wa Sudan Kusini kwenda kwenye uchaguzi ili kuwapa wananchi nafasi ya kuwachagua viongozi wanaowataka na kusaidia kukomesha wimbi la mauaji na machafuko yanayoendelea nchini humo.

Akizungumza kuhusu mchango huo, Ayii amesema, yuko tayari kutekeleza wajibu wake wa kifedha kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi, lakini anataka kuwe na uhakika kwamba uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa.

“Ikiwa uchaguzi hautafanyika kama ulivyopangwa,nitaomba nirejeshewe fedha zangu,” amesema Ayii.

Aidha, Ayii amemtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Sudan People's Liberation Movement (SPLM), Akol Paul Kordit kuunga mkono kufanyika kwa uchaguzi huo akisisitiza kuwa, wananchi wa Sudan Kusini wanapaswa kupata fursa ya kutumia kura zao kuamua mustakabali wa uongozi wa nchi.

Kwa mujibu wa Ayii, uchaguzi ni sehemu muhimu ya kutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika mchakato wa kisiasa na kuchagua viongozi wanaowaamini, hatua ambayo anaamini inaweza kusaidia kuweka msingi wa kumaliza mzunguko wa mauaji na migogoro unaoendelea kuikabili nchi hiyo.

Kauli hiyo inakuja wakati Sudan Kusini ikiendelea kukabiliwa na changamoto za kisiasa na kiusalama, huku mjadala kuhusu uchaguzi na mustakabali wa mchakato wa kisiasa ukiendelea kuwa suala nyeti nchini humo.

Wakati huo huo, Serikali ya Rais Salva Kiir bado inakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki ya Haki (EACJ) iliyopo Arusha, Tanzania, inayohusisha mzozo wa madai ya thamani ya dola za Marekani bilioni 1.05.

Kesi hiyo inahusisha Serikali ya Sudan Kusini na kampuni ya South Sudan Supreme Airlines Ltd., inayomilikiwa na mfanyabiashara Ayii Duang Ayii.

Mzozo huo wa kisheria unaongeza uzito katika mazingira ambayo Ayii, ambaye pia ni mfanyabiashara mashuhuri nchini Sudan Kusini, ameendelea kutoa msimamo wake kuhusu masuala ya utawala, uchaguzi na mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo.

Aidha,kwa sasa, mjadala kuhusu kufanyika kwa uchaguzi unaendelea kuwa miongoni mwa masuala muhimu yanayoangaliwa kwa karibu na wananchi na wadau wa kisiasa nchini Sudan Kusini, hasa kutokana na matarajio kwamba sanduku la kura linaweza kutoa njia ya kisiasa ya kushughulikia baadhi ya changamoto zinazoikabili nchi hiyo.

Sudan Kusini inatarajiwa kufanya uchaguzi mwezi Desemba,mwaka huu baada ya miaka kadhaa ya kucheleweshwa mara kwa mara.

Mkataba wa amani wa 2018 ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano nchini Sudan Kusini.

Ingawa, mvutano umeongezeka katika miezi ya hivi karibuni baada ya kukamatwa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar mnamo 2025.

Chini ya mchakato wa amani, uchaguzi ulipaswa kufanywa mnamo mwaka 2022,lakini ukacheleweshwa hadi 2024 na tena hadi mwaka huu 2026. (NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here