Rais Dkt.Mwinyi azitaka nchi za NAM kuunganisha sauti kutetea maslahi ya pamoja

BELGRADE-Nchi wanachama wa Harakati za Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) zimetakiwa kuunganisha sauti na misimamo yao ili kuongeza ushawishi katika maamuzi ya kimataifa na kuhakikisha maslahi ya mataifa yanayoendelea yanasikilizwa na kupewa uzito unaostahili.
Wito huo umetolewa Septemba 1,2026 jijini Belgrade nchini Serbia na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati akihutubia Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa kuadhimisha miaka 65 tangu kufanyika kwa Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi wa NAM, uliofanyika mwaka 1961 jijini Belgrade, Jamhuri ya Serbia.

Dkt. Mwinyi amehudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwasilisha ujumbe wa Tanzania kuhusu nafasi ya NAM katika kukabiliana na changamoto zinazolikabili dunia kwa sasa.
Katika hotuba yake, Rais Mwinyi amesisitiza kuwa,misingi ya NAM iliyoasisiwa mwaka 1961 bado ina umuhimu mkubwa katika mazingira ya sasa ya kimataifa, akieleza kuwa mshikamano wa nchi wanachama ni muhimu katika kulinda maslahi ya pamoja na kuongeza nguvu ya mataifa yanayoendelea katika mijadala na maamuzi ya kimataifa.

Amesema,kutofungamana na upande wowote hakumaanishi mataifa kukosa msimamo katika masuala ya kimataifa, bali ni haki ya kila taifa kufanya maamuzi yake kwa uhuru kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wake, huku likilinda uhuru, mamlaka na heshima ya taifa.

Kwa mujibu wa Rais Mwinyi, mshikamano huo unapaswa pia kuonekana katika juhudi za kutafuta amani na kutatua migogoro inayozikabili sehemu mbalimbali za dunia.

Amehimiza matumizi ya mazungumzo, upatanishi na kujenga kuaminiana kama njia muhimu za kutafuta suluhu za migogoro, akisisitiza pia umuhimu wa kushughulikia chanzo cha migogoro, ikiwemo ukosefu wa haki, usawa na ujumuishi.
Pia, Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kufanya mageuzi katika mfumo wa taasisi za kimataifa, hususan Umoja wa Mataifa na Baraza lake la Usalama, pamoja na taasisi za fedha za kimataifa ili kuimarisha uwakilishi, uwazi na usawa katika mchakato wa kufanya maamuzi.

Amesema,Afrika inastahili kupata uwakilishi mkubwa na wa haki zaidi katika mifumo hiyo, kwa kuzingatia nafasi na mchango wa bara hilo katika masuala ya kimataifa pamoja na idadi ya mataifa yanayoliwakilisha.

Aidha, amezitaka nchi wanachama wa NAM kuimarisha Ushirikiano wa Kusini, pamoja na kutafuta maeneo ya ushirikiano kati ya NAM na BRICS, hususan katika masuala ya fedha za maendeleo na mageuzi ya mfumo wa utawala wa kimataifa.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuimarishwa bila kuathiri misingi, maadili na utambulisho wa NAM.
Akieleza msimamo wa Tanzania, Rais Dkt. Mwinyi amesema, itaendelea kuunga mkono NAM yenye umoja, mshikamano, sauti yenye nguvu na uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika dunia ya sasa.

Amesema,Tanzania itaendelea kusukuma ajenda zinazolenga kuimarisha amani, haki ya maendeleo, ushirikiano wa Kusini na kujenga mfumo wa kimataifa unaozingatia usawa, uwakilishi wa haki na maslahi ya mataifa yote.

Mkutano huo wa Belgrade unafanyika katika kumbukumbu ya miaka 65 tangu mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi za NAM uliofanyika mwaka 1961, tukio lililoweka msingi wa harakati hiyo katika mazingira ya mabadiliko makubwa ya kisiasa duniani.

Aidha,kwa Tanzania, msimamo huo unaakisi dhamira ya kuendeleza diplomasia inayosisitiza amani, ushirikiano wa kimataifa, kuheshimu mamlaka ya nchi na kuongeza nafasi ya mataifa yanayoendelea katika mifumo ya maamuzi ya dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here