LUSAKA-Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 01, Septemba, 2026, amehudhuria sherehe za kuapishwa kwa Mheshimiwa Hakainde Hichilema, Rais Mteule wa Jamhuri ya Zambia, jijini Lusaka, nchini Zambia.
Rais Hichilema amechaguliwa kuiongoza Zambia kwa muhula wa pili, baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 13 Agosti, 2026 nchini humo.
Tanzania na Zambia zimeendeleza ushirikiano wa kindugu na kihistoria, ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Dkt. Kenneth Kaunda wa Zambia.
Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili umeendelea kuimarika kupitia uchumi, nishati, miundombinu, biashara na uwekezaji, ukichagizwa na miradi ya pamoja inayounganisha maslahi ya pande zote mbili na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa.
Miradi hiyo inahusisha ufufuaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ujenzi wa bomba jipya la mafuta la TAZAMA, pamoja na maunganisho ya gridi za umeme kati ya Zambia, Tanzania na Kenya.Katika muhula wa kwanza wa Rais Hichilema, thamani ya biashara kati ya Tanzania na Zambia iliongezeka kutoka shilingi bilioni 320.978 mwaka 2021 hadi shilingi bilioni 820.359 mwaka 2024.
Zambia, ambayo ni mtumiaji wa pili mkubwa wa Bandari ya Dar es Salaam, imewekeza katika miradi 29 nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani milioni 86.34, na kuzalisha ajira 1,204; huku Watazania wakimiliki hisa katika kampuni kubwa na za kati takribani 965 nchini Zambia.

