Rais Dkt.Samia mgeni rasmi Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na CEOs wa taasisi za umma nchini

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (C-CEOs Forum) 2026 ambao unaotarajiwa kufanyika Septemba 28 hadi 30, 2026 jijini Arusha.
Kaimu Msajili wa Hazina,Bi.Lightness Mauki, amesema hayo leo Septemba 9,2026 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Msajili wa Hazina,Bw. Nehemiah Mchechu wakati wa kikao cha Ofisi ya Msajili wa Hazina na wahariri wa vyombo vya habari nchini.

Bi.Mauki amesema, mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 1,000, wakiwemo wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma nchini pamoja na wadau mbalimbali.

Mkutano huo utafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), ambapo kupitia mijadala ya kitaasisi, Serikali inalenga kuimarisha ufanisi, uwajibikaji, uwazi na ubunifu katika taasisi za umma ili ziweze kuwa wabia madhubuti wa maendeleo ya Taifa.

Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo: “Mashirika ya Umma yenye Ufanisi wa Juu kwa Uchumi Shindani, Shirikishi na Imara katika Kutekeleza Dira 2050.”

Bi. Mauki amesema, kaulimbiu hiyo inalenga kusisitiza umuhimu wa taasisi za umma kushiriki kikamilifu katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa maslahi mapana ya Taifa.

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeeleza kuwa, imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hususan katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kupitia taasisi na mashirika inayoyasimamia.
Bi.Mauki amesema, mapato yasiyo ya kodi yameongezeka kwa asilimia 108 kutoka Shilingi bilioni 637 katika mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia Shilingi trilioni 1.327 katika mwaka wa fedha 2025/26.

Aidha, amesema thamani ya uwekezaji katika taasisi za umma imeongezeka kwa asilimia 41, kutoka Shilingi trilioni 65.19 mwaka 2019/20 hadi kufikia Shilingi trilioni 92.

Ofisi hiyo pia imefanikiwa kutoa mafunzo ya utangulizi kwa watendaji wakuu 193 kutoka taasisi 193, huku ikifanya tathmini huru ya utendaji kwa taasisi 184 hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26.

Mafanikio hayo yamekuja wakati Serikali ikiendelea kuimarisha usimamizi wa mali na uwekezaji wa umma, kwa lengo la kuhakikisha taasisi za umma zinaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here