NA DIRAMAKINI
SIMBA Sports Club ya jijini Dar es Salaam imeanza kwa kishindo safari yao katika Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya kuitandika Mighty Wanderers ya Malawi mabao 6-1 katika mchezo wa marudiano uliochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo umeiwezesha Simba kusonga mbele kwa jumla ya mabao 7-1, baada ya pia kushinda mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 uliochezwa katika Uwanja wa Taifa wa Bingu nchini Malawi.
Katika mtanange huo wa Septemba 13,2026 Simba SC imeanza mchezo hup wa marudiano kwa kasi, ikionesha dhamira ya kutafuta ushindi mkubwa, huku mshambuliaji Clatous Chama akiifungia timu hiyo bao la kwanza dakika ya saba.
Chama alifungua ukurasa wa mabao kwa shuti kali la mguu wa kushoto akiwa ndani ya eneo la hatari, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Anicet Oura na kuiweka Simba mbele.
Dakika ya 28, Libasse Gueye aliongeza bao la pili kwa kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Elie Mpanzu kutoka upande wa kushoto na kuifanya Simba kutawala mchezo kwa kujiamini zaidi.
Aidha,Chama alirejea tena kwenye orodha ya wafungaji dakika ya 33, akifunga bao lake la pili na la tatu kwa Simba katika mchezo huo baada ya kufuatilia mpira uliookolewa na kipa wa Mighty Wanderers, Dalitso Phiri kufuatia shuti kali la Oura.
Hata hivyo, Mighty Wanderers ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 43 kupitia Isack Kaliati, aliyefunga kwa mkwaju wa penalti baada ya nahodha msaidizi wa Simba, Rushine De Reuck kumchezea madhambi mshambuliaji Clement Nyondo ndani ya eneo la hatari.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Simba ikiwa mbele kwa mabao 3-1, huku wenyeji wakiendelea kuutawala mchezo katika maeneo mengi ya uwanja.
Vilevile,kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuendelea kutafuta mabao zaidi, na juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 69, pale Gueye alipofunga bao lake la pili katika mchezo huo na la nne kwa Simba.
Gueye alitumia vyema mguu wake wa kushoto kuupiga mpira uliomshinda kipa Phiri, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Oura, ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji waliohusika kwa kiasi kikubwa katika mashambulizi ya Simba.
Dakika za mwisho za mchezo ziliendelea kuwa za Simba, ambapo Kaletso Makgalwa alifunga bao la tano dakika ya 88 baada ya Ismail Mgunda kufanya kazi kubwa katikati ya uwanja na kutoa pasi safi iliyomuwezesha Makgalwa kumalizia shambulizi hilo.
Simba haikuishia hapo, kwani ilipata bao la sita katika dakika za mwisho za mchezo kupitia Morice Abraham, aliyemalizia krosi iliyopigwa na Makgalwa.
Ushindi huo wa mabao 6-1 umeipa Simba tiketi ya kuendelea na kinyang'anyiro cha kuwania taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa imevuka hatua hiyo kwa jumla ya mabao 7-1.
SIMBA KUKUTANA NA 15 DE AGOSTO
Aidha,baada ya kuiondoa Mighty Wanderers, Simba sasa itakutana na 15 de Agosto ya Equatorial Guinea katika hatua inayofuata ya mashindano hayo.
15 de Agosto imefuzu hatua hiyo baada ya kuitoa Fomboni FC ya Comoro katika hatua ya awali ya mashindano.
Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo, mchezo wa kwanza wa hatua hiyo utachezwa kati ya Oktoba 16 na 18, 2026 huku mchezo wa marudiano ukipangwa kuchezwa kati ya Oktoba 23 na 25, 2026.
Simba sasa inaingia katika hatua hiyo ikiwa na matumaini ya kuendelea na mwenendo wake mzuri na kusonga mbele zaidi katika mashindano makubwa ya klabu barani Afrika.
YANGA SC YASONGA MBELE
Mbali na hayo, Yanga SC imefanikiwa kusonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa Gaborone United ya Botswana kwa mabao 2-1.
Ni kupitia mtanange uliopigwa Septemba 12,2026 katika dimba la Azam Complex lilopo Chamanzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Aidha,baada ya kuiondoa Gaborone United, Yanga sasa imepangiwa kukutana na CFFA ya Madagascar katika hatua ya pili ya awali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Tags
Gaborone United
Habari
Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika
Michezo
Michuano ya Mabingwa Afrika
Mighty Wanderers
Simba SC
Young Africans SC





