BoT yasisitiza matumizi ya Akili Unde kuimarisha utendaji wa Sekta ya Fedha

MWANZA- Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesisitiza umuhimu wa taasisi za fedha kutumia teknolojia za kisasa, hususan Akili Unde na ubunifu wa takwimu, ili kuboresha utoaji wa maamuzi, usimamizi wa vihatarishi, ufanisi wa kiutendaji na utoaji wa huduma za fedha zilizo salama na zinazokidhi mahitaji ya wateja.
Akizungumza leo Oktoba 28, 2026, wakati wa ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania jijini Mwanza, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa matumizi ya Akili Unde yana nafasi muhimu katika kubadilisha namna benki na benki kuu zinavyotekeleza majukumu yao, hususan katika kipindi hiki ambacho teknolojia inaendelea kukua na kubadilika kwa kasi duniani.

Gavana Tutuba amesema kuwa, kwa muda mrefu, taasisi nyingi zimejikita katika mabadiliko ya kidijitali kupitia matumizi ya mifumo ya kompyuta, huduma za benki kwa njia ya simu na intaneti pamoja na teknolojia za kuhifadhi taarifa.
Hata hivyo, amesema Akili Unde inafungua hatua mpya ya maendeleo kwa kuwezesha mifumo kuchambua taarifa, kutabiri mwenendo wa mambo na kusaidia kufanya maamuzi kwa ufanisi zaidi.

Gavana Tutuba amesema, BoT imeanza kuweka misingi ya matumizi ya Akili Unde na ubunifu wa takwimu katika shughuli zake za kitaasisi, ikiwemo kuanzisha Kituo cha Ubunifu wa Akili Unde na Takwimu (AI and Data Innovation Hub) na kuidhinisha sera pamoja na mikakati ya kuongoza matumizi ya teknolojia hizo kwa kuzingatia usiri wa taarifa, uwajibikaji na usimamizi wa kibinadamu.
Aidha, amesema BoT imeingia makubaliano ya ushirikiano na taasisi tano za elimu ya juu na utafiti nchini kwa lengo la kuharakisha tafiti, majaribio na ubunifu wa matumizi ya Akili Unde katika maeneo mbalimbali, yakiwemo utafiti wa uchumi, usimamizi wa sekta ya fedha, usimamizi wa sarafu na mifumo ya malipo.

Kongamano hilo lililobeba kaulimbiu “Zaidi ya Mabadiliko ya Kidijitali: Jinsi Akili Unde Inavyobadilisha Utendaji wa Benki na Benki Kuu,” limewakutanisha wasomi, wataalamu, watendaji wa sekta ya fedha na watunga sera kwa ajili ya kujadili fursa na changamoto za matumizi ya teknolojia hiyo katika kuimarisha sekta ya fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here