Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe atoa wito kuhusu Bima ya Afya

NA GODFREY NNKO

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe amewahimiza wananchi wa makundi yote kujiunga na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akisisitiza kuwa awamu ya pili ya uandikishaji imefungua fursa kwa kila mwananchi, bila kujali hali yake ya kiuchumi au sekta anayofanyia kazi.
Dkt. Magembe ametoa wito huo leo Oktoba 22, 2026 wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya uandikishaji wa mpango huo uliofanyika katika Uwanja wa Sabasaba mkoani Mtwara, akieleza kuwa awali uandikishaji ulilenga zaidi wananchi wasio na uwezo wa kiuchumi.

Amesema, hatua hiyo mpya inalenga kupanua wigo wa wananchi wanaonufaika na bima ya afya kwa kuwajumuisha watu wenye uwezo wa kiuchumi, wafanyakazi wa sekta binafsi na makundi mengine katika jamii.

“Awali tulianza kwa kuandikisha kundi la wananchi ambao hawakuwa na uwezo wa kiuchumi. Leo tunafungua milango kwa kila mtu, wakiwemo wenye uwezo wa kifedha na wale wanaofanya kazi katika sekta binafsi na sekta nyingine,” amesema Dkt. Magembe.
Ameeleza kuwa, mpango huo haupaswi kutazamwa kama huduma inayojitegemea, bali ni nyenzo ya kuimarisha na kuboresha huduma za afya ambazo tayari zinatolewa nchini.

Aidha, amezitaka mamlaka na wataalamu wa afya kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mpango huo, ikiwemo matumizi ya mapato yatakayokusanywa kupitia bima hiyo ili yaelekezwe katika kuboresha huduma na kuongeza manufaa kwa wananchi.

Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa kuboresha huduma kwa wateja katika vituo vya afya, akibainisha kuwa namna wananchi wanavyopokelewa, wanavyohudumiwa na wanavyopata taarifa kuhusu bima hiyo inaweza kuchangia kujenga imani yao na kuongeza mwitikio wa kujiandikisha.
Pia, amehimiza wataalamu wa afya kubadili mtazamo na kuboresha mawasiliano na wananchi ili kuwahamasisha kutumia huduma za bima ya afya na kuendelea kuwa na imani na mfumo huo.

Katika hatua nyingine, amewataka wananchi wa Mtwara kutumia fursa ya msimu wa korosho kupanga matumizi ya mapato yao kwa kujiunga na bima ya afya, akieleza kuwa kufanya hivyo kutawasaidia kuwa na utaratibu wa kugharamia huduma za matibabu wanapozihitaji.
Hata hivyo, uzinduzi huo unafungua hatua mpya ya uandikishaji katika Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ukiwa na lengo la kupanua ushiriki wa wananchi na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kupitia mfumo wa bima kote nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here