Wabunge Mtwara wataka wakulima wa korosho kuchangia bima ya afya

NA GODFREY NNKO

WABUNGE kutoka Mkoa wa Mtwara wamewataka wakulima wa korosho kushiriki katika kufanikisha upatikanaji wa Bima ya Afya kwa Wote, wakieleza kuwa mchango mdogo unaotokana na uzalishaji wa zao hilo unaweza kusaidia kaya nyingi kupata huduma za afya.
Wakizungumza leo Oktoba 22, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa Awamu ya Pili ya uandikishaji wa Bima ya Afya kwa Wote mkoani Mtwara, wabunge hao wameeleza kuwa, ushiriki wa wakulima, kwa kushirikiana na viongozi na wananchi, unaweza kuongeza wigo wa watu watakaonufaika na mpango huo.

Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Dkt. Yahaya Esmail Nawanda amesema, Mkoa wa Mtwara huzalisha takribani tani 200,000 za korosho, hivyo mchango wa Shilingi 50 kwa kila kilo unaweza kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 10.

Amesema, fedha hizo zinaweza kusaidia kugharamia bima za afya kwa kaya nyingi, akibainisha kuwa, mkoa huo una takribani kaya 200,200 zinazozalisha korosho.

“Ukiangalia uzalishaji wa korosho katika Mkoa wa Mtwara, mchango wa Shilingi 50 kwa kila kilo unaweza kuleta fedha nyingi zitakazosaidia wananchi kupata bima ya afya. Hilo ndilo tunalotaka kulifanikisha ili wakulima na familia zao wanufaike na huduma za afya,” amesema Dkt. Nawanda.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mtwara, Mheshimiwa Asha Salum Motto amesema, wanawake wa mkoa huo, kupitia Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) wamekuwa wakihamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya katika kata na wilaya mbalimbali.

Amesema, mkoa una jumla ya kata 191 na kwamba juhudi za uhamasishaji zimeelekezwa katika kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kuongeza uelewa na ushiriki wao katika mpango huo.

Motto amesisitiza kuwa, wanawake wako tayari kuendeleza kampeni hiyo, akieleza kuwa afya ya familia ni muhimu katika kulinda ustawi wa jamii na nguvu kazi ya taifa.

“Tunawaomba wananchi tuchukue hatua sasa kwa kujiunga na bima ya afya bila kusubiri kuugua. Tunaamini kuwa kwa kutumia fursa zilizopo, ikiwemo mapato yatokanayo na kilimo cha korosho, tunaweza kuwezesha familia nyingi kupata huduma za afya,” amesema.
Pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji katika sekta ya afya, huku akimshukuru Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya mkoani humo.

Aidha, amebainisha kuwa, eneo lao limepokea magari mawili ya wagonjwa akieleza kuwa, hatua hiyo itasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Naye Mbunge wa Tandahimba, Mheshimiwa Katani Ahmad Katani amesema, ana imani kuwa utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote utaleta matokeo chanya kwa wananchi, akitumia uzoefu wake wa kufanya kazi na Waziri wa Afya bungeni kueleza matarajio yake kuhusu utekelezaji wa mpango huo.

Kwa upande mwingine, wabunge hao wameahidi kushirikiana na viongozi wa mkoa kuhamasisha wakulima wa korosho na wananchi kwa ujumla kuchangia na kujiunga na bima hiyo, kwa lengo la kuhakikisha kaya nyingi zaidi zinapata fursa ya kupata huduma za afya.
Wamesema, ushirikiano kati ya serikali, wakulima na wananchi ni muhimu katika kufanikisha mpango huo na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Nanauka amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa kushiriki kikamilifu katika uandikishaji wa wanachama wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akisema mkoa huo umeongoza katika zoezi hilo.

Pia, amewapongeza wakazi wa Jimbo la Mtwara Mjini kwa kile alichokieleza kuwa wamefanya vizuri katika uandikishaji, huku akieleza matumaini yake kuwa awamu ya pili itaimarisha zaidi mwitikio wa wananchi.

Ili kuunga mkono mpango huo, Dkt. Nanauka amesema, ameandaa mchango wa bima 100 jimboni ili kunufaisha wajane na makundi mengine yenye changamoto za upatikanaji wa huduma za afya.
Amesema, ushiriki wa makundi hayo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata kinga ya kifedha dhidi ya gharama za matibabu.

Dkt. Nanauka amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha miundombinu, vifaa tiba na rasilimali watu katika sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.

Amesema, kaulimbiu ya “Mtwara kuchele” inaakisi ari ya wananchi wa mkoa huo katika kushiriki shughuli za maendeleo, ikiwemo uandikishaji wa bima ya afya na matumizi ya huduma zinazotolewa na Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here