iTrust yazindua rasmi iAfrica ETFs, Watanzania kuwekeza barani Afrika

NA GODFREY NNKO

KAMPUNI ya iTrust Finance Limited imezindua rasmi mifuko mitatu ya uwekezaji wa hisa inayolenga sekta muhimu za uchumi wa Afrika, ikiwa na lengo la kupanua fursa kwa wawekezaji wa Tanzania kushiriki katika masoko ya mitaji ya bara hilo.
Mifuko hiyo inayojulikana kwa pamoja kama iAfrica Exchange Traded Funds (ETFs), inalenga kuwawezesha wawekezaji binafsi na taasisi kupata fursa za kuwekeza katika kampuni zilizoorodheshwa katika masoko ya hisa ya Afrika kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo Oktoba 27, 2026 kufuatia idhini ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ya Hati za Ofa na Hati za Udhamini za mifuko hiyo, iliyotolewa Oktoba 5, 2026 kwa mujibu wa Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania.

Mifuko hiyo ni iAfrica Financials ETF, unaolenga sekta ya huduma za kifedha; iAfrica Mining & Energy ETF, unaojikita katika sekta za madini na nishati; pamoja na iAfrica Telco & Tech ETF, unaolenga mawasiliano na teknolojia.

iTrust Finance Limited itakuwa msimamizi wa mifuko hiyo, huku Benki ya NBC ikiwa mdhamini na mtunzaji wa mali zake. Mifuko hiyo imesajiliwa na CMSA kwa namba I0074/F08, I0074/F09 na I0074/F10.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Afisa wa Biashara na Maendeleo ya Soko, Bw. Emmanuel Nyalali amesema, mifuko hiyo inaongeza chaguo la bidhaa za uwekezaji na kupanua fursa kwa wawekezaji wenye malengo na uwezo tofauti wa kifedha.

Nyalali amesema kuwa, mifuko hiyo itasimamiwa kikamilifu na meneja wa uwekezaji atakayechagua na kurekebisha uwekezaji kulingana na malengo ya kila mfuko, kwa lengo la kukuza thamani ya uwekezaji kwa muda mrefu.

Pia, amesisitiza kuwa, uwekezaji wa pamoja unatoa fursa ya kusambaza fedha katika kampuni mbalimbali, lakini wawekezaji wanapaswa kuelewa kuwa thamani ya uwekezaji inaweza kupanda au kushuka kutokana na mabadiliko ya soko na hali za biashara.

Naye Mkurugenzi wa Usimamizi na Uchunguzi wa Soko kutoka CMSA, Exaut Julius akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama amesema, mamlaka hiyo imeidhinisha nyaraka za ofa na hati za udhamini za mifuko hiyo baada ya iTrust Finance Limited kutimiza matakwa ya kisheria.

Amesema, idhini hiyo imetolewa kwa kuzingatia Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania, pamoja na kanuni zinazosimamia uanzishwaji na uendeshaji wa mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

Vilevile amesema, hatua hiyo inaonesha umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria katika kuanzisha na kuendesha bidhaa za uwekezaji.

Ameeleza kuwa, mifuko hiyo itasaidia kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa fursa kwa watu wenye uwezo tofauti wa kifedha kuwekeza kwa pamoja katika masoko ya mitaji.
CMSA imeipongeza iTrust Finance Limited pamoja na wadau walioshiriki katika kuanzisha mifuko hiyo, akieleza matumaini yake kuwa itaendeshwa kwa weledi na kutoa manufaa kwa wawekezaji.

Kupanua wigo wa uwekezaji barani Afrika

Akizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa iTrust Finance Limited, Bw. Faiz Arab amesema, kuanzishwa kwa bidhaa hizo ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo kupanua huduma za uwekezaji na kukidhi mahitaji ya wawekezaji wanaotaka kutumia fursa zinazopatikana nje ya mipaka ya kikanda.

Amesema, wawekezaji wa ndani wamekuwa wakionesha nia ya kupanua uwekezaji wao zaidi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Kwa miaka mingi, ujumbe mmoja umekuwa ukijirudia kutoka kwa wawekezaji wetu: wako tayari kuwekeza nje ya mipaka ya kikanda. Mifuko ya iAfrika inajibu hitaji hilo kwa kuwaletea Watanzania fursa za uwekezaji zinazopatikana katika bara la Afrika,” amesema Arab.

Ameongeza kuwa, mifuko hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi wa Afrika, huku ikiwasaidia wawekezaji kugawa mitaji yao katika kampuni na nchi tofauti kupitia mfumo mmoja wa uwekezaji.

Dirisha la kupokea maombi ya ofa ya uwekezaji limefunguliwa Oktoba 26, 2026 na linatarajiwa kufungwa Novemba 27, mwaka huu kwa ofa ya awali.

Sekta tatu zinazolengwa

Akifafanua kuhusu mifuko hiyo, Mchambuzi wa Uwekezaji wa Mifuko wa iTrust, Bw. Azaan Sachedina amesema, kila mfuko umeundwa kulenga sekta maalumu yenye nafasi katika maendeleo ya uchumi wa Afrika.

Amesema, iAfrica Financials ETF inalenga kampuni za huduma za kifedha zikiwemo benki, bima, usimamizi wa mali na biashara zinazotumia teknolojia katika utoaji wa huduma za kifedha.

Upande wa iAfrica Telco & Tech ETF unalenga kampuni za mawasiliano na teknolojia ikiwemo zinazohusika na huduma za kidijitali, vituo vya kuhifadhi na kuchakata taarifa, mifumo ya malipo kwa njia ya simu na biashara zinazotumia teknolojia katika shughuli zake.

Mfuko wa iAfrica Mining & Energy ETF umejikita katika kampuni za madini na nishati ikiwemo uzalishaji wa madini muhimu, nishati jadidifu, miundombinu ya nishati na uchakataji wa rasilimali za asili.
Kwa kuunganisha sekta hizo katika bidhaa tofauti za uwekezaji, mifuko hiyo inalenga kuwapa wawekezaji nafasi ya kuchagua maeneo yanayoendana na malengo yao ya kifedha na kupunguza utegemezi wa sekta moja pekee.

Kiwango cha chini cha uwekezaji Shilingi 100,000

Vilevile, amesema bei ya kila kipande katika mifuko yote mitatu ni Shilingi 1,000 huku kiwango cha chini cha ununuzi kikiwa vipande 100 kwa kila mfuko sawa na Shilingi 100,000.

Mifuko hiyo itasimamiwa kikamilifu, huku gawio litakalopatikana likielekezwa tena katika mali zinazounda mfuko husika.

Mfumo huo unalenga kukuza thamani ya uwekezaji kwa muda mrefu, ingawa matokeo yatategemea mwenendo wa soko na thamani ya mali zilizowekezwa.

Katika kudhibiti hatari, Mchambuzi huyo amesema, kampuni imeweka kiwango cha juu cha asilimia 40 cha uwekezaji katika nchi moja kwa kila mfuko.

Aidha, mifuko hiyo inalenga kampuni zenye thamani ya soko inayozidi dola za Marekani milioni 100 na zinazokidhi vigezo vya ukwasi.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, usajili wa taarifa za wawekezaji unatarajiwa kukamilika Desemba 11, 2026 na matokeo ya mgao wa vipande kutangazwa Desemba 28, mwaka huu.

Vipande vilivyotengewa wawekezaji vinatarajiwa kuwekwa katika akaunti zao za mfumo wa uwekaji na utunzaji wa dhamana (CDS) Januari 11, 2027, huku biashara katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ikipangwa kuanza Januari 14, 2027.

NBC yaeleza umuhimu wa uwekezaji wa Waafrika

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw. Theobald Sabi amesema, mazingira ya uwekezaji barani Afrika yanabadilika, hali inayohitaji kuwepo kwa mifumo inayowawezesha Waafrika wenyewe kushiriki katika kufadhili maendeleo ya uchumi wa bara hilo na kunufaika nayo.

“Kwa miaka mingi, mijadala kuhusu uwekezaji barani Afrika imejikita zaidi katika kuvutia mitaji kutoka nje ya bara. Sasa tunashuhudia ajenda nyingine muhimu, ambayo ni kuwawezesha Waafrika wenyewe kuwekeza katika ukuaji wa Afrika na kushiriki katika ustawi wao wa kiuchumi,” amesema Bw. Sabi.

Ameeleza kuwa, mfuko huo unatoa njia kwa wawekezaji binafsi na taasisi nchini kupata fursa za uwekezaji katika kampuni zilizoorodheshwa katika masoko mbalimbali ya hisa barani Afrika.

Ameongeza kuwa, mpango huo unaendana na juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa bara, ikiwemo utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), kwa kupanua uhusiano kati ya masoko ya mitaji ya nchi mbalimbali.

Bw. Sabi amesema, NBC inachangia katika mpango huo kwa kutumia uzoefu wake wa soko la ndani, utaalamu wa kikanda na mahusiano ya kimataifa kusaidia utunzaji wa mali na kurahisisha miamala ya uwekezaji.

Ushirikiano uliozaa matokeo

Uzinduzi wa mifuko hiyo unaendeleza ushirikiano kati ya NBC na iTrust Finance katika kuanzisha bidhaa mbalimbali za uwekezaji.

Taasisi hizo tayari zimeshirikiana katika kuanzisha mifuko mitano ya uwekezaji wa pamoja pamoja na iTrust EAC Large-Cap ETF, unaolenga kampuni kubwa za Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, ofa ya awali ya mfuko wa EAC Large-Cap ETF ilikusanya Sh bilioni 54.03 dhidi ya lengo la Sh bilioni 10, sawa na zaidi ya mara tano ya kiwango kilicholengwa.

Matokeo hayo yanaonesha mwitikio uliopatikana katika ofa hiyo na juhudi zinazoendelea za kupanua bidhaa za uwekezaji zinazopatikana katika soko la mitaji la Tanzania.

Wawekezaji watatumia njia za kidijitali na matawi ya NBC

Wawekezaji wanaotaka kushiriki katika ofa hiyo wanaweza kuwasilisha maombi kupitia programu ya simu ya iTrust inayopatikana katika mifumo ya iOS na Android, au kutembelea matawi ya NBC nchini kote.
Pia, Bw. Sabi amesema, maombi yanaweza kufanyika kupitia kampuni za udalali zilizoidhinishwa kufanya biashara katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.

NBC imesema imewaandaa wafanyakazi wake katika matawi mbalimbali kutoa maelezo na mwongozo kwa wawekezaji wanaohitaji kufahamu masharti ya ofa hiyo na namna ya kushiriki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here