NA GODFREY NNKO
MFUMO wa Kielektroniki wa Manunuzi ya Umma (NEST) umewezesha kutolewa kwa zabuni 403,643 zenye thamani ya Shilingi trilioni 42.6, huku ukiokoa takribani Shilingi bilioni 28 kutokana na kupunguza matumizi ya karatasi za nyaraka za zabuni.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba ameyasema hayo leo Oktoba 29, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya mamlaka hiyo, wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR).
Amesema, mfumo huo umeimarisha uzingatiaji wa sheria za ununuzi wa umma, ambapo kiwango cha uzingatiaji kimeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2023/24 hadi asilimia 79 mwaka 2025/26.
Bw. Simba ameeleza kuwa, NEST imepunguza gharama na muda wa kushiriki zabuni kwa kuwawezesha wazabuni kuwasilisha maombi kwa njia ya kielektroniki bila kulazimika kusafiri kwenda kwenye taasisi nunuzi.
Aidha, amesema makundi maalumu yamepata zabuni zenye thamani ya Shilingi bilioni 82.34, zikiwemo za vijana Shilingi bilioni 44.74, wanawake Shilingi bilioni 33.51, wazee Shilingi bilioni 3.78 na watu wenye ulemavu Shilingi milioni 680.
Amesema, hadi sasa makundi 33,659 yamesajiliwa katika mfumo huo, huku PPRA ikiendelea kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi na kujisajili ili kunufaika na fursa za ununuzi wa umma.
Katika hatua nyingine, Bw. Simba amesema zaidi ya benki 36 zimeunganishwa na mfumo wa Bank Security Portal, unaorahisisha utoaji na uhakiki wa dhamana za zabuni.
Ameongeza kuwa, NEST imeboreshwa pia kuwezesha uwasilishaji wa malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki.
Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa, programu ya simu ya NEST Tender, inayopatikana kupitia Play Store na App Store inawawezesha watumiaji kupata taarifa za zabuni, kuwasilisha maombi na kufuatilia malipo.
Bw. Simba amesema, PPRA itaendelea kutoa elimu kwa wadau kuhusu sheria na taratibu za ununuzi wa umma, kwa lengo la kuimarisha uwazi, ushindani wa haki, uwajibikaji na ushiriki wa wazawa katika kukuza uchumi wa taifa.
Tags
Dar es Salaam
Dennis Simba
Dira 2050
Habari
Makundi Maalum
Mfumo wa Kielektroniki
NEST
OTR
PPRA
Ununuzi wa Umma
Wazabuni
Zabuni za Serikali
