Mwongozo kamili wa udahili Awamu ya Tatu wa TCU 2026/2027: Tarehe, sifa na jinsi ya kutuma maombi

NA DIRAMAKINI

UMEKOSA nafasi katika Awamu ya Kwanza na Pili? Bado una nafasi. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza rasmi kufunguliwa kwa Awamu ya Tatu na ya mwisho ya udahili wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2026/2027 kuanzia Oktoba 3, 2026.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles D. Kihampa ameyabainisha hayo Oktoba 3,2026 jijini Dodoma.

"Baada ya kukamilika kwa awamu zote mbili za udahili, tume imepokea maombi ya kuongeza muda wa kutuma maombi ya udahili kutoka kwa baadhi ya waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika awamu zilizopita na pia vyuo ambavyo bado vina nafasi vimeomba vipewe muda kuendelea kudahili.

"Hivyo, Tume imeongeza muda wa udahili kwa kufungua Awamu ya Tatu na ya mwisho ya udahili itakayoanza leo tarehe 03 hadi 09 Oktoba, 2026."

Tume inawashauri waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakuweza kupata nafasi ya kudahiliwa katika Awamu ya Pili kutokana na sababu mbalimbali, watumie fursa hii vizuri kwa kutuma maombi yao ya udahili kwenye vyuo wanavyovipenda.

Aidha, Tume inaelekeza Vyuo vya Elimu ya Juu nchini kuendelea kutangaza programu ambazo bado zina nafasi.

Waombaji udahili na vyuo wanapaswa kuzingatia utaratibu wa udahili wa Awamu ya Tatu. 

Huu ni mwongozo kamili wa kila kitu unachohitaji kujua;

1: Kwa mijibu wa TCU, waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja katika Awamu ya Pili na wale ambao hawakuweza kuthibitisha udahili katika Awamu ya Kwanza, wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimoja wapo kuanzia tarehe 03 hadi 19 Oktoba, 2026.

2:Uthibitisho huo unafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.

3:Wale ambao hawatapata kwa wakati ujumbe huo, wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalum ya siri ili kuweza kujithibitisha katika chuo husika.

4:Aidha, uthibitisho wa udahili ufanyike kupitia akaunti ambayo muombaji alitumia wakati wa kuomba udahili.

5:Kwa urahisi wa rejea, orodha ya majina ya waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja inapatikana kwenye tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz).

TAREHE MUHIMU ZA AWAMU YA TATU:

1. Tarehe 03 hadi 09 Oktoba, 2026 
Kutuma maombi ya udahili katika Awamu ya Tatu.

2. Tarehe 13 hadi 14 Oktoba, 2026 
Vyuo kuwasilisha Tume majina ya waliodahiliwa katika Awamu ya Tatu.

3. Tarehe 17 Oktoba, 2026 
Vyuo kutangaza majina ya waliodahiliwa katika Awamu ya Tatu.

4. Tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2026 
Kuthibitisha udahili kwa waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja katika Awamu ya Tatu na wale walioshindwa kuthibitisha udahili wao katika awamu za udahili zilizopita.

Vilevile, TCU imewakumbusha waombaji udahili wa Shahada ya Kwanza kuwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika.

Kwa wale ambao watapata changamoto katika kujithibitisha, vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here