Prof. Kabudi: Mji wa Serikali Mtumba kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi

DODOMA- WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla, huku akiwataka wawekezaji na wafanyabiashara nchini kuzitumia fursa hizo kwa kuwekeza katika shughuli zenye tija.
Prof. Kabudi ameyasema hayo leo tarehe 27 Oktoba, 2026 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa majengo ya ofisi za wizara, taasisi za serikali na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba.

Amesema uwekezaji unaofanyika katika mji huo unatoa nafasi kwa sekta binafsi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya wananchi.
Ameongeza kuwa, kadiri shughuli za serikali zinavyozidi kuimarika katika mji huo, ndivyo mahitaji ya huduma mbalimbali yatakavyoongezeka, hali itakayofungua fursa za uwekezaji katika sekta za usafirishaji, malazi, biashara na huduma za kitaalamu.

Vilevile, amebainisha kuwa, Mji wa Serikali Mtumba ni alama muhimu ya utekelezaji wa dhana ya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali, huku ukiendelea kuchochea maendeleo na kufungua fursa mpya kwa wananchi.

“Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na wafanyabiashara ili kutumia kwa ufanisi fursa zinazotokana na maendeleo ya Mji wa Serikali na Makao Makuu,” amesema Prof. Kabudi.
Aidha, ameitaka sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika Mji wa Serikali Mtumba na Dodoma kwa ujumla ili kunufaika na fursa zinazotokana na kuongezeka kwa shughuli za Serikali na ukuaji wa mji huo.

Kwa upande mwingine, Prof. Kabudi amewataka watumishi wa umma wanaofanya kazi katika Mji wa Serikali Mtumba kutumia vizuri miundombinu iliyowekwa ili kuimarisha uwajibikaji, uadilifu, ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Sambamba na hayo, amesisitiza kuwa, uwepo wa majengo mazuri ya serikali pekee hautoshi kuleta matokeo yanayotarajiwa bila kuambatana na utendaji bora, nidhamu ya kazi na uzalendo kwa watumishi wa umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here