NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuondoka nchini tarehe 25 Oktoba 2026 kuelekea Jamhuri ya Korea (Korea Kusini), kushiriki majukwaa ya kimataifa yanayojikita katika utalii wa visiwa, uwekezaji, utamaduni na maendeleo endelevu.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 24, 2026 na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar, Raqey Mohamed.
Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kutembelea Maonesho ya Dunia ya Visiwa 2026 (2026 World Island Exhibition Yeosu Korea) Yeosu, pamoja na kushiriki Jukwaa la 27 la Sera za Utalii kwa Visiwa (27th Inter-Islands Tourism Policy Forum, ITOP Forum 2026) katika Kisiwa cha Jeju.
Maonesho ya Dunia ya Visiwa ya Yeosu yanawakutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali kubadilishana uzoefu, kutangaza fursa na kuonesha ubunifu katika maeneo ya utalii, rasilimali za bahari, utamaduni, teknolojia na maendeleo ya visiwa, chini ya kaulimbiu “Island, Connecting the Ocean and the Future.”
Akiwa Jeju, moja ya maeneo maarufu ya utalii nchini Korea Kusini, Rais Dkt. Mwinyi atashiriki Jukwaa la ITOP linalowakutanisha viongozi na wataalamu kutoka maeneo mbalimbali duniani kujadili utalii endelevu, uwekezaji, mabadiliko ya tabianchi na namna ya kuendeleza uchumi wa visiwa sambamba na kulinda mazingira, utamaduni na urithi.
Zanzibar imekuwa mwanachama wa ITOP tangu mwaka 2004, na kwa sasa ni mwanachama pekee kutoka Afrika katika mtandao huo wenye wanachama 12, wakiwemo Jeju, Okinawa, Hainan, Bali, Southern Province ya Sri Lanka, Hawaii, Phuket, Cebu, Penang, Galápagos na South Aegean.
Katika Kikao cha Viongozi wa ITOP (ITOP Leaders’ Roundtable), Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kuungana na viongozi kutoka visiwa na maeneo wanachama wa ITOP kujadili mustakabali wa utalii wa visiwa, kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na changamoto zinazovikabili visiwa, pamoja na kuendeleza ajenda ya utalii endelevu kwa kushirikiana na UN Tourism.
Sambamba na hayo, Zanzibar inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Jukwaa la ITOP mwaka 2027, ambapo Rais Dkt. Mwinyi atakabidhiwa bendera ya ITOP, ikiwa ni ishara rasmi ya Zanzibar kuchukua nafasi ya kuwa mwenyeji wa jukwaa hilo lijalo. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza nafasi ya Zanzibar kutangaza utalii wake na kuimarisha ushirikiano na maeneo mengine ya visiwa duniani.
Zanzibar pia itatumia majukwaa ya Yeosu na Jeju kutangaza vivutio vyake vya utalii, historia, utamaduni na urithi wa Kiswahili. Katika maonesho hayo, Zanzibar itaonesha mavazi ya Kizanzibari, ngoma na muziki wa asili, pamoja na vyakula vya asili vya Zanzibar, huku wapishi na vikundi vya sanaa vikishiriki katika programu mbalimbali zilizoandaliwa.
Katika ziara hiyo nchini Korea Kusini, Rais Dkt. Mwinyi pia anatarajiwa kukutana na viongozi wa makampuni mbalimbali yanayojishughulisha na sekta za nishati, viwanda, uzalishaji wa chakula na teknolojia, kujadili fursa za uwekezaji, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano yanayoweza kuchangia maendeleo ya Zanzibar.
Tags
Dkt. Hussein Ali Mwinyi
Habari
ITOP Forum 2026
Jeju
Kimataifa
Korea Kusini
Maonesho ya Visiwa 2026
Utalii wa Visiwa
Uwekezaji
World Island Exhibition Yeosu
Zanzibar
Zanzibar ITOP 2027
