YEOSU- Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar inalenga kuimarisha zaidi ushirikiano na Korea Kusini, hususan katika utalii, uchumi wa buluu, nishati mbadala, maendeleo ya viwanda, teknolojia na elimu, kwa kujifunza kutokana na uzoefu na mafanikio ya nchi hiyo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 27 Oktoba 2026 jijini Yeosu, Korea Kusini, akiwa ameanza ziara yake ya kikazi nchini humo yenye mikutano na ziara mbalimbali zinazohusu uwekezaji, teknolojia, uchumi wa buluu na maendeleo ya viwanda.
Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amezungumza na Meya wa Jiji la Yeosu, Mhe. Seo Young-hak, kuhusu maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Yeosu.
Amesema, maeneo hayo ni pamoja na utalii na utamaduni, uchumi wa buluu, ufugaji wa samaki na uzalishaji wa mazao ya baharini, nishati mbadala na miundombinu ya visiwa, viwanda na uwekezaji, pamoja na elimu na mafunzo.
Katika uchumi wa buluu, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza umuhimu wa Zanzibar kunufaika na uzoefu wa Korea katika uvuvi wa kisasa, ufugaji wa samaki, mifumo ya uhifadhi wa mazao kwa baridi na usarifu wa mwani, ili kuongeza thamani, kupanua masoko na kuongeza kipato cha wakulima na wavuvi.Aidha, ameeleza nia ya kushirikiana zaidi katika nishati mbadala, ikiwemo nishati ya jua na upepo, pamoja na teknolojia na miundombinu inayoweza kuhimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Katika eneo la viwanda na uwekezaji, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inaweza kujifunza kutokana na uzoefu wa Yeosu katika uendelezaji wa viwanda, ujuzi wa kiufundi na matumizi ya teknolojia, huku akiwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kuangalia fursa zilizopo Zanzibar.
Ameeleza kuwa, Zanzibar tayari inanufaika na ushirikiano wa Korea Kusini kupitia programu mbalimbali, zikiwemo ufadhili wa masomo na miradi ya elimu, huku akisisitiza umuhimu wa kupanua ushirikiano huo katika maeneo mengine ya maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi pia ameeleza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya Hospitali ya Rufaa ya Binguni pamoja na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonesho Zanzibar, ambayo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati yenye nafasi ya kunufaika na ushirikiano wa Korea Kusini.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi ametembelea kampuni ya POSCO, Gwangyang, inayojishughulisha na uzalishaji wa chuma, na kujionea matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa viwandani pamoja na juhudi za kuendeleza viwanda vinavyozingatia utunzaji wa mazingira.
Pia ametembelea K-Food, Goheung-gun, kampuni inayozalisha na kuchakata bidhaa za mwani, na kujionea matumizi ya teknolojia katika uchakataji wa mwani, uongezaji thamani na upanuzi wa masoko, maeneo yenye umuhimu katika kuongeza manufaa ya zao hilo kwa wakulima wa Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi ametembelea Maonesho ya Dunia ya Visiwa 2026 (2026 World Island Exhibition Yeosu Korea), ambako amejionea ubunifu, bidhaa na uzoefu mbalimbali unaowasilishwa na washiriki kutoka mataifa mbalimbali.






