LUANDA- Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeng'ara katika Umoja wa Afrika kwa utashi wa uongozi kupitia uwekezaji kwenye Sekta ya Maji chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia kupitia Serikali yake imetoa kipaumbele kwa Sekta ya Maji na kutenga fedha za kutekeleza miradi pamoja na usimamizi thabiti katika kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya uhakika ya maji safi na salama.
Sambamba na kupiga hatua za haraka maeneo ambayo yalikua na changamoto kubwa kufikiwa na maji wakati kazi ya kuendelea kusambaza maeneo yote ikiendelea kwa kasi.
Hayo yameelezwa na viongozi wa Afrika katika mkutano wa Marais, Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wa Maji jijini Luanda nchini Angola kwenye Mkutano wa Maji kama Kiungo cha Amani.
Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoshiriki mkutano huu leo Oktoba 22, 2026 unaongozwa na Mheshimiwa Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.Waziri Kombo anamwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo mkutano huo, pia unamjumuisha Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso (Mb.), Waziri wa Maji na wataalam wengine.
Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Kuimarisha Utawala wa Rasilimali Maji Inayovuka Mipaka barani Afrika kama Nyenzo ya Kuzuia na Kutatua Migogoro.”
Majadiliano yamehusisha diplomasia ya maji na usimamizi wa rasilimali za maji zinazovuka mipaka; ushiriki wa jamii, wanawake na vijana; athari za mabadiliko ya tabianchi, uhamaji na migogoro; pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya maji na kujenga uwezo.
Pamoja na mambo mengine, Ujumbe wa Tanzania umetatumia jukwaa hili kueleza mafanikio yake katika sekta ya maji, mchango wake katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na usimamizi wa pamoja wa mabonde, mito na maziwa.
Tags
Balozi Mahmoud Thabit Kombo
Dr Samia Suluhu Hassan
Foreign Tanzania
Habari
Kimataifa
Mkutano wa Luanda
Rais Samia
Sekta ya Maji Tanzania
Umoja wa Afrika
Waziri Jumaa Aweso
Waziri Mahmoud Kombo











