Zabuni za Umma: PPAA yaelimisha wabunifu na wakadiriaji majenzi

ARUSHA- Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imewajengea uwezo Wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi kuhusu mazingira ya haki katika mchakato wa zabuni za umma.
Lengo ni ili waweze kudai haki zao pindi wanapoona hawakutendewa haki kwenye michakato ya zabuni za umma walizoshiriki.

Mkuu wa Sehemu ya Huduma za Sheria PPAA, Bi. Agnes Sayi akizungumza na waandishi wa Habari kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa PPAA, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Sita wa Wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi, ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) jijini Arusha amesema, lengo PPAA kushiriki maonesho hayo ni kutoa elimu kuhusu haki katika mchakato wa zabuni za umma.

“Sheria ya ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, iliweka sharti la lazima kuwa ununuzi wote wa umma ufanyike kieletroniki katika mfumo wa NeST, baada ya sharti hilo PPAA ilijenga Moduli ndogo ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa ambapo imekuwa na mchango mkubwa kwa taasisi nunuzi na waabuni,” amesema Bi. Sayi.

Bi. Sayi ameongeza kuwa, awali kabla ya kuanza kwa matumizi ya Moduli ya kuwasilisha Malalamiko na rufaa, wazabuni ambao hawakuridhika na uamuzi wa Maafisa Masuuli na Taasisi Nunuzi walilazimika kuwasilisha malalamiko au rufaa zao moja kwa moja katika ofisi za PPAA, Dodoma.

Jambo lililokuwa linatumia muda, gharama, kupotea kwa baadhi ya nyaraka za zabuni na kuchangia kupunguza misingi ya uwazi na uwajibikaji kwa pande zote mbili.
"Baada ya kuanza rasmi kwa matumizi ya Moduli hiyo imerahisisha uwasilishaji wa malalamiko na kutoa fursa kwa wazabuni wengi zaidi ikiwa ni pamoja na kuokoa muda, gharama, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika mchakato ya ununuzi wa umma na Utunzaji wa kumbukumbu za malalamiko na rufaa kwa usahihi na urahisi,” amesema Bi. Sayi.

Aidha, Bi. Sayi alifafanua kuwa mazingira ya haki katika mchakato wa zabuni za umma ni yale yanayohakikisha kuwa washiriki wote wanatendewa kwa usawa na bila upendeleo.

Alisisitiza kuwa, mazingira hayo yanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na masharti yaliyowekwa katika nyaraka za zabuni, huku yakipinga vitendo vya rushwa na kuhakikisha uwazi na uadilifu katika mchakato mzima wa ununuzi wa umma.

Sanjari na matumizi ya Moduli, PPAA imefanikiwa kuanzisha huduma ya Mkutano kwa njia ya Mtandao “Video Conference” ambapo hutumika kusikiliza mashauri kwa wahusika walioshindwa kufika moja kwa moja katika Ofisi za PPAA kwa ajili ya kusikiliza mashauri yalilowasilishwa mbele yake.

Bi. Sayi ameongeza kuwa huduma ya Video Conference imetoa fursa ya kuwasikiliza wahusika wa shauri walioshindwa kufika PPAA kutokana na sababu mbalimbali na kuiwezesha Mamlaka ya Rufani kutekeleza jukumu lake la msingi la utatuzi wa migogoro itokanayo na michakato ya ununuzi wa Umma.

“Kwa sasa baadhi ya mashauri yameshasikilizwa kwa kwa “video conference” na baadhi ya washiriki wakiwa katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na wengine kutoka katika mataifa ya Afrika Kusini, Nigeria, Poland, India na China,” amebainisha Bi. Sayi.

Katika hatua nyingine, Bi. Sayi ameongeza kuwa PPAA imenzisha matumizi ya Programu ya Simu ya Mkononi “Mobile App” kwa lengo la kuwawezesha wazabuni kuwasilisha malalamiko na rufaa dhidi ya maamuzi yanayotolewa katika michakato ya ununuzi wa umma.

Hatua hii inalenga kupunguza gharama za kupata haki pamoja na kuharakisha utatuzi wa migogoro.
Bi. Sayi amewasihi Wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi na wadau wengine kuzingatia sheria na kanuni za ununuzi wa umma ili kuiwezesha Serikali kuwa na mfumo wa ununuzi unaochochea ushindani, matumizi bora ya fedha za umma na utekelezaji wenye mafanikio wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mkutano Mkuu wa Sita wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) ulioanza tarehe 20 – 23 Oktoba, 2026 umeongozwa na Kaulimbiu: Kuijenga Tanzania tunayoitaka kuelekea 2050: Kuimarisha Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa kwa Mazingira Endelevu ya Ujenzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here