Rufiji kuandika historia mpya, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa na Chuo cha Afya mbioni

NA GODFREY NNKO

MAMIA ya wananchi wamejitokeza katika Viwanja vya Kijiji cha Nyamwage, Kata ya Mbwara iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani kushuhudia tukio la kihistoria la uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa pamoja na Chuo cha Afya Samia Suluhu Hassan.
Hafla hiyo inafanyika leo Oktoba 4, 2026 ambapo mgeni rasmi ni Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji.

Uwekezaji huo unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa zaidi kuwahi kutekelezwa katika Sekta ya Afya wilayani Rufiji, hatua ambayo imeibua matumaini mapya miongoni mwa wananchi kuhusu upatikanaji wa huduma bora, za kisasa na zinazopatikana kwa urahisi zaidi katika eneo hilo.

Wananchi waliojitokeza kushuhudia hafla hiyo wameeleza furaha yao, wakisema ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa pamoja na Chuo cha Afya ni hatua muhimu itakayobadili kwa kiasi kikubwa sura ya huduma za afya na mafunzo ya wataalamu wa afya katika wilaya hiyo na maeneo ya jirani.

Pia, wananchi hao, wameieleza DIRAMAKINI kubwa, uwekezaji huu una umuhimu mkubwa kwa kuwa utasaidia kusogeza huduma za kibingwa na za rufaa karibu na wananchi, huku uwepo wa chuo cha afya ukitarajiwa kuongeza fursa za mafunzo na uzalishaji wa wataalamu watakaohitajika katika kukidhi mahitaji ya sekta hiyo.

Vilevile,wananchi wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka msukumo katika kuboresha Sekta ya Afya na kuwekeza katika miundombinu inayolenga kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Wamesema, uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo ni ishara ya utekelezaji wa jitihada za Serikali katika kuhakikisha wanapata huduma za afya zilizo bora na zenye kuendana na mahitaji ya wakati.

Aidha, wananchi wameeleza kuwa ujenzi wa hospitali hiyo pamoja na chuo cha afya hautakuwa na manufaa kwa wakazi wa Rufiji pekee, bali unaweza kuwa na mchango mpana kwa wananchi kutoka maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani na mikoa jirani watakaohitaji huduma za rufaa na za kibingwa.

Tukio hilo limekusanya viongozi mbalimbali wa Serikali, watendaji wa sekta ya afya pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Rufiji, huku likibeba matumaini mapya ya kuimarika kwa huduma za afya na mafunzo ya wataalamu katika wilaya hiyo.

Aidha,uwekaji wa jiwe la msingi unafungua rasmi hatua muhimu ya utekelezaji wa mradi huo, ambao unatarajiwa kuwa miongoni mwa uwekezaji wenye umuhimu mkubwa katika maendeleo ya huduma za afya katika Mkoa wa Pwani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here