Rufiji: Undani wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Chuo cha Afya Samia Suluhu Hassan

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amesema, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Chuo cha Afya Samia Suluhu Hassan katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani utakuwa miongoni mwa hatua kubwa za Serikali katika kusogeza huduma za afya za kibingwa na bobezi karibu na wananchi hususan wakazi wa Rufiji, Kibiti, Mafia, Mkuranga na Kilwa mkoani Lindi.
Ameyasema hayo leo Oktoba 4,2026 wakati akiweka mawe ya msingi ya ujenzi wa miradi hiyo katika Kijiji cha Nyamwage, Kata ya Mbwara iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, akisema uwekezaji huo utasaidia kuondoa changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za rufaa.

Amesema, uamuzi wa kujenga hospitali hiyo unatokana na uhalisia wa kijiografia wa Mkoa wa Pwani, ambao una maeneo yaliyotawanyika na changamoto za usafiri, hivyo kufanya umbali wa kufuata huduma za afya kuwa suala linaloweza kuathiri maisha ya wagonjwa.

Waziri Mchengerwa amesema, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa inayohudumia wananchi wa Pwani kwa sasa iko Tumbi wilayani Kibaha, upande wa kaskazini mwa mkoa, hali inayowalazimu wananchi kutoka maeneo ya Kusini mwa Pwani kusafiri umbali mrefu wanapohitaji huduma za kibingwa.

Amesema, baadhi ya wananchi kutoka Rufiji, Kibiti, Mafia na maeneo ya jirani na Kilwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa wanapohitaji huduma za rufaa, hasa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka wakiwemo wajawazito, watoto na majeruhi wa ajali.

“Kwao umbali si takwimu, ni tofauti kati ya uhai na kifo. Ndiyo maana Serikali imeamua kuileta hospitali hii kwa wananchi, si mwananchi kuifuata hospitali,” amesema.

Amesema, kwa baadhi ya wananchi wanaotoka maeneo hayo kuelekea hospitali za rufaa zilizopo mbali, safari inaweza kufikia zaidi ya kilomita 500 hali ambayo imekuwa ikiongeza gharama, muda na hatari kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka.

Amesema, uwepo wa Hospitali ya Rufaa Rufiji utasaidia kupunguza changamoto hiyo na kutoa fursa kwa wananchi kupata huduma za kibingwa karibu zaidi na maeneo yao.

Waziri Mchengerwa amesema, hospitali hiyo haitakuwa kwa ajili ya wakazi wa Rufiji pekee, bali itahudumia pia wananchi wa Kibiti, Mafia, Mkuranga na maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani pamoja na wananchi wa Kilwa mkoani Lindi na maeneo ya jirani.

Amesema, ujenzi wa hospitali hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati iliyopo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, akisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutafsiri kwa vitendo ahadi ya kuwafikishia wananchi huduma muhimu mahali wanapoishi.

“Tunaposema kusogeza huduma karibu na wananchi, hii ndiyo tafsiri halisi ambayo Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amekwenda kuwatendea Watanzania wa maeneo haya,”amesema.

Waziri Mchengerwa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya, akisema maono yake yamekuwa chachu ya mabadiliko katika sekta hiyo na kuwezesha huduma za kibingwa kusogezwa kutoka katika miji michache kwenda mikoani.

Amesema, uwekezaji huo unaendana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Vilevile, Waziri Mchengerwa amesema, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa itakapokamilika itakuwa na wataalamu wa kutosha, vifaa vya kisasa, maabara, bohari ndogo ya dawa, huduma za damu salama pamoja na huduma mbalimbali za kibingwa.

Amesema, huduma za afya ya mama na mtoto zitakuwa miongoni mwa maeneo muhimu yatakayoboreshwa kupitia hospitali hiyo, hatua ambayo inalenga kuchangia kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.
Aidha, amesema ujenzi wa hospitali hiyo umeambatanishwa na ujenzi wa Chuo cha Afya Samia Suluhu Hassan ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa wataalamu wa afya katika eneo hilo na maeneo mengine nchini.

“Jengo bila mtaalamu ni ukuta tu. Ndiyo maana tunajenga hospitali na chuo kwa pamoja,” amesema Waziri Mchengerwa.

Amesema, chuo hicho kitatoa mafunzo kwa vijana watakaosaidia kujaza nafasi za kada mbalimbali za afya zenye uhitaji mkubwa, hivyo kuwa sehemu ya suluhisho la upungufu wa watumishi wa afya wilayani Rufiji, Kibiti, Mkuranga, Mafia mkoani Pwani na taifa kwa ujumla.

Miradi itasimamiwa kwa kasi

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo amesema, Serikali ya Mkoa itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan ya afya ili ikamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

RC Nyongo amewahakikishia wananchi kuwa, miradi ya kimkakati ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Chuo cha Afya Samia Suluhu Hassan itaendelea kutekelezwa kwa kasi inayotakiwa.

Amesema, lengo ni kuhakikisha huduma za afya zinakuwa bora za kuaminika na zinapatikana kwa wakati bila wananchi kukumbana na vikwazo vinavyotokana na usafiri au umbali mrefu.

Mkuu huyo wa mkoa pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali ya mkoa, viongozi wa wilaya na wananchi katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.

Amesema, ushirikiano huo ni nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo endelevu na kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi zinazowakabili wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake na juhudi za kuhakikisha huduma muhimu ikiwemo afya zinawafikia wananchi kwa urahisi.

Amesema, Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya afya na zahanati nchini, huku Wilaya ya Rufiji ikiendelea kunufaika na uwekezaji huo.

Dkt.Samizi amesema, uwekezaji huo umeimarisha huduma za afya hususan za mama na mtoto na kuchangia katika juhudi za kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Amesema, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa utaongeza zaidi uwezo wa wananchi wa Rufiji na maeneo ya jirani kupata huduma za juu za afya bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Ilani inatekelezwa bila ubaguzi

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao amesema, utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho unalenga kuhakikisha wananchi wananufaika na maendeleo bila ubaguzi wa maeneo.
Mlao amewataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati na kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Amesema, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa na Chuo cha Afya ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Serikali katika kuboresha huduma za kijamii na kuinua maisha ya wananchi.

Hospitali na chuo ni miradi inayotegemeana

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari amesema, uwekaji wa jiwe la msingi la miradi hiyo ni sehemu ya safari ya mageuzi makubwa yanayoendelea katika sekta ya afya nchini.

Amesema, Serikali imekuwa ikisogeza huduma za kibingwa ambazo hapo awali zilipatikana katika miji michache, kupitia ujenzi na uboreshaji wa hospitali za rufaa katika mikoa mbalimbali.

Tayari amesema, Wizara ya Afya ilifanya tathmini ya kitaalamu kabla ya kuamua kuifanya Hospitali ya Rufaa Rufiji kuwa mradi wa kimkakati, kutokana na umuhimu wake kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka Rufiji.

Amesema, uwekezaji huo unaendana pia na mipango ya Serikali ya kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unaenda sambamba na upatikanaji wa huduma bora.

“Bima ya afya kwa wote haitakuwa na tija kama wananchi hawatapata huduma bora. Kwa hiyo, uwekezaji huu unaendana na mipango na mikakati ya Wizara ya Afya katika kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi,” amesema.

Amesema, hospitali hiyo itakuwa na huduma za kibingwa ikiwemo huduma bora za mama na mtoto, maabara ya kisasa, bohari ndogo ya dawa na huduma za damu salama.

Kwa upande mwingine amesema,Chuo cha Afya kitawaandaa vijana kuwa wataalamu wa afya watakaohitajika sasa na baadaye, hivyo kuifanya miradi hiyo miwili kutegemeana katika kuhakikisha huduma za afya zinakuwa bora na endelevu.

Tayari ameahidi kuwa, Wizara ya Afya itasimamia kwa karibu ujenzi wa hospitali hiyo ili ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Amesema, Serikali kupitia Bohari ya Dawa itahakikisha hospitali hiyo inapofunguliwa inakuwa na dawa na vifaa tiba vinavyohitajika, pamoja na vifaa vya kisasa kulingana na huduma zitakazotolewa.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili waweze kunufaika kikamilifu na huduma zitakazotolewa katika hospitali hiyo.

Amesema, hatua hiyo itasaidia kuhakikisha wananchi hawataishia kuona miundombinu ya afya ikijengwa, bali watakuwa na uwezo wa kuitumia wanapohitaji huduma.

Rufiji ni kitovu cha maendeleo

Akizungumza kuhusu maendeleo mapana ya Rufiji, Mheshimiwa Mchengerwa amesema, eneo hilo limeanza kubadilika kwa kasi kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika katika sekta mbalimbali.
Ametaja miongoni mwa miradi hiyo kuwa ni uzalishaji wa umeme wa megawati 2,115 kupitia Mradi wa Julius Nyerere Hydro Power Project, uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na fursa zinazotokana na Bonde la Mto Rufiji.

Amesema, uwekezaji huo unapaswa kwenda sambamba na upatikanaji wa huduma bora za kijamii, ikiwemo afya na elimu ili wananchi waweze kunufaika na fursa za kiuchumi zinazozalishwa katika eneo lao.

Waziri Mchengerwa pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa juhudi za kuhamasisha uwekezaji na maendeleo ya viwanda katika maeneo ya Rufiji, Kibiti na Mkuranga.

Amesema, upatikanaji wa huduma za afya bora katika eneo hilo utakuwa kichocheo muhimu kwa uwekezaji, kwa kuwa wawekezaji wanahitaji mazingira yenye huduma muhimu za kijamii kwa wafanyakazi na jamii kwa ujumla.

Pongezi kwa Serikali

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha wanawake wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Kijakazi Yunus Mohamed amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuimarisha sekta ya afya nchini, akisema wananchi wa Lindi, hususan wanawake, tayari wameanza kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.

Kwa mujibu wa Kijakazi, tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani, Serikali imeongeza kwa kiasi kikubwa miundombinu ya afya katika Mkoa wa Lindi, hatua ambayo amesema imeongeza matumaini kwa wananchi kuhusu upatikanaji wa huduma bora na salama.

Amesema, katika kipindi hicho, Serikali imejenga hospitali za wilaya nne, zahanati zaidi ya 40 pamoja na vituo vya afya zaidi ya 267, akisisitiza kuwa hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na maeneo wanayoishi.

Kijakazi amesema ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa katika eneo la Rufiji utakuwa na umuhimu wa kipekee kwa wananchi wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi kutokana na ukaribu wa kijiografia wa eneo hilo ikilinganishwa na safari wanazolazimika kufanya kwa sasa wanapohitaji huduma za rufaa.

Amesema, kwa sasa wagonjwa kutoka Kilwa wanaohitaji huduma za rufaa hulazimika kusafiri hadi Lindi Mjini, umbali ambao ni mrefu na unaoweza kuongeza changamoto kwa wagonjwa, hasa wale wanaohitaji matibabu ya haraka.

“Hospitali hii ya rufaa itakapokamilika itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi, hususan Wilaya ya Kilwa,” amesema Kijakazi.

Ameongeza kuwa, uwepo wa hospitali hiyo Rufiji utapunguza umbali wa safari za wagonjwa kutoka Kilwa na maeneo mengine ya jirani, hivyo kupunguza gharama na muda wa kusafiri pamoja na kuongeza uwezekano wa wagonjwa kupata huduma kwa wakati.

Mheshimiwa Kijakazi amesema, wagonjwa kutoka Kilwa wanaopewa rufaa kwenda Lindi Mjini wakati mwingine hulazimika kusafiri zaidi ya kilomita 400 wanapohitaji kuendelea kupata huduma za juu zaidi katika mikoa mingine.

Amesema, hospitali hiyo itakapokamilika, baadhi ya wagonjwa watakaokuwa wanapata rufaa kupitia Rufiji wataweza kuelekezwa katika vituo vya juu vya tiba kwa njia fupi zaidi ikiwemo kuelekea Dar es Salaam.

“Uwepo wa hospitali hii utapunguza safari, utaokoa maisha na kupunguza changamoto wanazokutana nazo wananchi wanapolazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya,” amesema.

CCM Wilaya

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Juma Kassim Ndaruke amesema, uwekaji wa jiwe la msingi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Chuo cha Afya ni ushahidi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ndaruke amesema, wananchi wa Mkoa wa Pwani wanatambua na kuthamini uwekezaji unaofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii, akitaja ujenzi wa miradi hiyo miwili kuwa miongoni mwa hatua zitakazobadili huduma za afya na mafunzo ya wataalamu katika eneo hilo.

Amesema, ujenzi wa hospitali hiyo utakuwa na manufaa makubwa si kwa wakazi wa Rufiji pekee, bali pia wananchi wa Kibiti, maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani pamoja na wananchi wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi na maeneo ya jirani.

“Uzinduzi wa miradi hii miwili leo ni uthibitisho tosha wa kazi njema inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Pwani,” amesema Ndaruke.
Aidha, Ndaruke amempongeza Waziri wa Afya kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, akisema ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa sambamba na Chuo cha Afya utasaidia kuongeza uwezo wa wananchi kupata huduma za afya karibu na maeneo yao, huku chuo hicho kikitarajiwa kuchangia katika upatikanaji wa wataalamu wa afya.

Amesema, viongozi wa CCM na wananchi wa Pwani wako tayari kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Kijakazi amesema, uwekezaji huo unapaswa kutazamwa zaidi kama sehemu ya juhudi za kuokoa maisha ya wananchi, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kuhakikisha huduma za afya za kibingwa zinapatikana kwa urahisi zaidi kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here