NA GODFREY NNKO
SERIKALI imesisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikieleza kuwa, sekta hiyo inatarajiwa kuchangia takribani asilimia 70 ya uwekezaji wote unaohitajika, huku Serikali ikigharamia asilimia 30 iliyobaki kupitia rasilimali za umma.
Waziri Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza kuhusu sekta binafsi kuchangia 70% ya uwekezaji Dira 2050 katika kongamano hilo lililofanyika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijiji Dar es Salaam. ( You Tube Screen Shot photo).Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo ametoa kauli hiyo Oktoba 11, 2026 alipomwakilisha Makamu wa Rais, Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi katika Kongamano la Kwanza la Jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji lililofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki, Dar es Salaam.
Amesema, sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kuongeza ajira, kuleta teknolojia mpya, kupanua uzalishaji na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Dkt. Akwilapo amesema, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji ushirikiano madhubuti kati ya Serikali na wawekezaji, pamoja na mazingira rafiki yatakayowezesha mitaji kuelekezwa katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuongeza thamani ya bidhaa na kukuza mapato ya taifa.
Amewataja wawekezaji kuwa na fursa katika kilimo na uongezaji thamani wa mazao, utalii, viwanda, nishati, uchumi wa buluu na uchumi wa kidijitali.
Tanzania yalenga kuvutia uwekezaji zaidi
Akizungumzia mwenendo wa uwekezaji, Dkt. Akwilapo amesema, Tanzania iliendelea kuvutia mitaji kutoka nje, huku uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi (FDI) ukifikia dola za Marekani bilioni 1.7 mwaka 2025.
Amesema, pia miradi 915 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 10.95 ilisajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA).
Kwa mujibu wa Dkt. Akwilapo uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.3 mwaka 2026, huku Serikali ikilenga kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 15.
Amesisitiza kuwa, kufikia malengo hayo kunategemea kuendelea kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza imani ya wawekezaji na kuhakikisha miradi inayotekelezwa inazalisha ajira na kuleta manufaa kwa wananchi.
Miundombinu yaimarisha ushindani
Dkt. Akwilapo amesema, Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafiri na nishati, ikiwemo reli, bandari na barabara, ili kupunguza gharama za uzalishaji na biashara, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuongeza tija.
Ameeleza kuwa, nafasi ya Tanzania katika Afrika Mashariki na Kati inatoa fursa kubwa za biashara kutokana na bandari zake zinazohudumia nchi jirani zisizo na bandari, zikiwemo Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Malawi.
Aidha, amesema uanachama wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) unawapa wawekezaji fursa ya kufikia masoko mapana zaidi ya soko la ndani.
Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kurahisisha taratibu za uwekezaji kwa kupunguza urasimu na kuboresha huduma kupitia TISEZA, ambako wawekezaji wanaweza kupata huduma mbalimbali katika kituo kimoja, zikiwemo usajili wa kampuni, vibali vya kazi na huduma zinazohusiana na ardhi.
Pia, amesema Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya kodi ili iwe rahisi kueleweka na kutekelezwa, huku ikisisitiza umuhimu wa kulinda mitaji na kuimarisha imani ya wawekezaji.
Ametaja uanachama wa Tanzania katika Wakala wa Kimataifa wa Dhamana za Uwekezaji (MIGA) na Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) kuwa sehemu ya mifumo inayohusiana na ulinzi wa uwekezaji na utatuzi wa migogoro ya kimataifa.
Teknolojia na ubia waimarisha uchumi
Akizungumzia mabadiliko ya kiteknolojia, Dkt. Akwilapo amesema, matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) na Akili Unde (AI) yanaendelea kubadilisha shughuli za kiuchumi, hivyo wafanyabiashara wanapaswa kuwekeza katika ubunifu na mifumo ya kisasa ili kuongeza ufanisi.
Amesema, matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza uzalishaji na kusaidia kampuni kufikia wateja wengi zaidi ndani na nje ya nchi.
Amesisitiza pia umuhimu wa ubia kati ya kampuni za ndani na za kigeni, akieleza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuleta uhamishaji wa teknolojia, maarifa na ujuzi kwa wataalamu wa Kitanzania, pamoja na kuongeza ajira na uwezo wa kampuni za ndani kushindana kimataifa.Ameongeza kuwa, ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za elimu ni muhimu katika kuandaa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika uchumi unaozidi kutegemea maarifa na teknolojia.
Utalii na machapisho kutangaza Tanzania
Kongamano hilo pia liliambatana na uzinduzi wa vitabu vya utalii na kitabu cha My 10 Years, kinachohusu safari na uzoefu wa Benson, mtoto wa Nyambari Nyangwine.
Dkt. Akwilapo aliipongeza Kampuni ya Nyambari Nyangwine kwa kutumia machapisho kutangaza vivutio vya Tanzania na kuimarisha uelewa wa kimataifa kuhusu utalii wa nchi.
Amesema, vitabu vinavyochapishwa kwa lugha mbalimbali vinaweza kufikisha taarifa za vivutio vya Tanzania kwa hadhira pana, kuongeza idadi ya wageni na kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii.
Amebainisha kuwa, utalii una uwezo wa kuongeza mapato ya taifa na kuunda ajira katika sekta zinazohusiana na usafiri, malazi, vyakula, sanaa na utamaduni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Group of Companies na Nyambari Nyangwine Foundation, Nyambari Nyangwine amesema, kongamano hilo ni fursa ya kuitangaza Tanzania kimataifa na kuimarisha biashara na uwekezaji.
Naye mwandishi wa fasihi, Charles Mloka amesisitiza umuhimu wa wazazi kutambua na kukuza vipaji vya watoto ili viweze kuwawezesha kufikia malengo yao.
Akielezea kitabu cha My 10 Years, mwakilishi wa familia ya Nyangwine amesema Benson, aliyezaliwa Oktoba 12, 2016 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, alianza kuonesha udadisi na kupenda kujifunza kuhusu mazingira tangu akiwa mdogo.
Kwa mujibu wa mwakilishi huyo, safari zake katika nchi mbalimbali zimempa fursa ya kujifunza historia, tamaduni na maisha ya jamii tofauti, huku uzoefu huo ukitumika kuandaa simulizi zinazolenga kuhamasisha watoto kupenda kusoma na kujifunza nje ya darasa.
Amesema, Benson ametembelea mataifa mbalimbali Afrika, Asia, Ulaya, Amerika na Australia, akipata nafasi ya kuona vivutio vya kihistoria na kujifunza kuhusu tofauti za tamaduni na mazingira.
Ameongeza kuwa, kitabu hicho kinaonesha namna safari zinavyoweza kuwa nyenzo ya elimu kwa watoto na vijana, kwa kuwajengea udadisi, kupanua maarifa na kuwahamasisha kuendeleza vipaji vyao.
Dkt. Akwilapo amewashukuru waandaaji wa kongamano hilo kwa kukutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa elimu, utalii na utamaduni, akieleza kuwa majukwaa hayo ni muhimu katika kujenga ushirikiano mpya na kubainisha fursa za maendeleo.
Pia, amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kujenga uchumi shindani, kuongeza ajira na kuhakikisha uwekezaji unaleta manufaa kwa wananchi na maendeleo endelevu ya Tanzania.