NA GODFREY NNKO
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limepata mafanikio makubwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita kuanzia mwaka 2021 hadi 2026 likiimarisha miundombinu ya upimaji, udhibiti wa ubora na usalama wa bidhaa.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 27, 2026.Sambamba na kuweka mazingira bora ya biashara kwa wazalishaji, wajasiriamali na wafanyabiashara nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi ameyasema hayo leo Oktoba 27, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari nchini, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR).
Mafanikio hayo yanajumuisha uwekezaji katika ujenzi wa maabara na ofisi za kanda, uandaaji wa maelfu ya viwango vya kitaifa, utoaji wa vyeti na leseni za ubora kwa wazalishaji.
Vilevile, usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi na matumizi ya mifumo ya TEHAMA kurahisisha utoaji wa huduma.
Dkt. Katunzi amesema, katika kipindi hicho, shirika hilo limeendelea kutekeleza jukumu lake la kulinda afya na usalama wa walaji kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazoingizwa kutoka nje zinakidhi matakwa ya viwango vinavyotakiwa.
Amesema, hatua hiyo inachangia ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Dkt. Katunzi amesema kuwa, pia Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za viwango ili kuzisogeza karibu na wananchi na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesema, TBS ilianzishwa kama sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha sekta za viwanda na biashara kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa. Shirika hilo linatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Viwango, Sura ya 130.
UWEKEZAJI WA MABILIONI KATIKA MIUNDOMBINU
Katika hatua ya kusogeza huduma karibu na wananchi, Serikali kupitia TBS imewekeza katika ujenzi na uboreshaji wa ofisi na maabara katika maeneo mbalimbali nchini, ili kupunguza umbali na gharama za kupata huduma za upimaji na uthibitishaji wa ubora wa bidhaa.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa ofisi na maabara katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma unaojulikana kama Viwango House jijini Dodoma, wenye thamani ya Shilingi bilioni 24.7.Amesema, maabara hizo zinatarajiwa kuhudumia Dodoma na mikoa jirani, hususan Singida na Tabora, hivyo kupunguza utegemezi wa huduma kutoka maeneo ya mbali na kuongeza ufanisi wa upimaji wa sampuli.
Aidha, TBS inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa ofisi na maabara katika eneo la Kiseke Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza. Mradi huo wa Viwango House jijini Mwanza unakadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 12.1.
Ukikamilika, amesema kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia mikoa sita ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.
Wakati huo huo, Dkt. Katunzi amesema, shirika hilo limeanza maandalizi ya awali ya ujenzi wa ofisi na maabara jijini Arusha, hatua inayolenga kupanua wigo wa huduma za viwango na kuimarisha uwezo wa taasisi hiyo kuwafikia wadau wengi zaidi.
Mbali na miradi hiyo mikubwa, Serikali imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 9.8 kuimarisha ofisi tisa za kanda za TBS zilizopo Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Pwani na Geita, pamoja na vituo vya ukaguzi katika mipaka, bandari na viwanja vya ndege.
Amesema, uwekezaji huo umehusisha uboreshaji wa ofisi, kuongeza wafanyakazi na upatikanaji wa vitendea kazi kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha ukaguzi wa bidhaa sokoni na katika maeneo ya kuingilia bidhaa nchini.
Hatua hiyo inalenga kupunguza upatikanaji wa bidhaa zisizokidhi viwango, huku ikihakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na salama kwa matumizi yao.
VIWANGO 3,901 VYAANDALIWA KUIWEZESHA BIASHARA
Pia, katika eneo la kuwezesha biashara, Dkt. Katunzi amesema, TBS imefanikiwa kuandaa viwango 3,901 katika sekta mbalimbali wakati wa kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, kwa kuzingatia mahitaji ya soko na mabadiliko ya teknolojia na uzalishaji.
Amesema, uandaaji wa viwango hivyo unasimamiwa na kamati za kitaalamu 117 zinazohusika na sekta za chakula, kemikali, uhandisi wa mitambo, umeme na ujenzi, nguo na ngozi, madini na vifaa vya uchimbaji madini, mazingira, pamoja na taaluma mtambuka.
Katika mchakato huo, TBS hushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo vyuo vikuu, taasisi za utafiti, wafanyabiashara, wazalishaji, vyama vya walaji, vyama na bodi za kitaalamu, taasisi za udhibiti na watunga sera.
Ushirikishwaji huo unalenga kuhakikisha viwango vinavyoandaliwa vinaendana na mahitaji halisi ya sekta husika na kusaidia wazalishaji kutengeneza bidhaa zinazokidhi matakwa ya ubora na usalama.
Mkurugenzi huyo amesema, viwango hivyo vina umuhimu mkubwa katika kukuza ushindani wa bidhaa za Tanzania, kuongeza imani ya walaji na kufungua fursa za biashara katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, TBS imetoa jumla ya vyeti na leseni za ubora 3,940 kwa wazalishaji, wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,683.
Mbali na hayo, amesema Serikali imekuwa ikitenga zaidi ya Sh milioni 300 kila mwaka kwa ajili ya kuwahudumia wajasiriamali wadogo bila malipo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha kuboresha bidhaa zao na kushiriki kikamilifu katika uchumi.
Kupitia utaratibu huo, wajasiriamali wanapata fursa ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, kuongeza imani ya wateja na kupanua masoko, ikiwemo uwezekano wa kuingia katika biashara za kimataifa.
Hatua hiyo pia inachangia kukuza viwanda vidogo na vya kati, kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kuimarisha nafasi ya wazalishaji wa ndani katika ushindani wa kibiashara.
BIDHAA 9,731 ZASAJILIWA
Aidha, katika kuhakikisha bidhaa zinazotumika na wananchi zinakidhi matakwa ya ubora na usalama, TBS imeendelea kusajili bidhaa za chakula na vipodozi pamoja na maeneo yanayohusika na uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa bidhaa hizo.
Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, jumla ya bidhaa 9,731 zimesajiliwa huku maeneo 80,836 yakisajiliwa nchni.
Amesema, usajili huo ni sehemu ya mfumo wa udhibiti unaolenga kuhakikisha bidhaa zinazowafikia walaji zinakidhi matakwa ya viwango, huku maeneo ya biashara na uzalishaji yakizingatia masharti yanayohusika.
Dkt. Katunzi amesema, udhibiti huo ni muhimu katika kuzuia bidhaa zinazoweza kuhatarisha afya za walaji na kuongeza uwajibikaji kwa wazalishaji, wasambazaji na wafanyabiashara.
ZAIDI YA SHEHENA 610,000 ZAKAGULIWA
TBS pia imeimarisha ukaguzi wa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka masoko ya nje ili kuhakikisha Tanzania haigeuzwi kuwa soko la bidhaa duni zisizokidhi viwango.
Katika kipindi husika, jumla ya shehena za bidhaa 183,186 zilikaguliwa kabla ya kusafirishwa kuja nchini kupitia mfumo wa Pre-Shipment Verification of Conformity (PVoC).
Aidha, shehena nyingine 426,842 zilikaguliwa baada ya kuwasili nchini kupitia mfumo wa Destination Inspection (DI).
Kwa ujumla, idadi hiyo inafikia shehena 610,028 zilizokaguliwa kupitia mifumo hiyo miwili.
Mbali na ukaguzi wa shehena, TBS ilikagua magari yaliyotumika 249,386 kabla ya kuingizwa nchini, hatua inayolenga kuhakikisha yanakidhi matakwa ya ubora na usalama yanayotakiwa.
Dkt. Katunzi amesema, ukaguzi huo unasaidia kuzuia uingizaji wa bidhaa zisizokidhi viwango, kulinda afya za watumiaji na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwa mazingira kutokana na matumizi ya bidhaa zisizofaa.
Pia, hatua hizo zinaimarisha mazingira ya ushindani wa haki kwa wafanyabiashara wanaozingatia viwango dhidi ya wale wanaoweza kuingiza bidhaa zisizokidhi matakwa yaliyowekwa.
WADAU 6,824 WAPATIWA MAFUNZO
Katika kuimarisha uelewa wa wadau kuhusu viwango na udhibiti wa ubora, TBS imetoa mafunzo kwa washiriki 6,824, wakiwemo wazalishaji wa bidhaa za viwandani na wasindikaji.
Mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa viwango katika uzalishaji, usimamizi wa ubora na usalama wa bidhaa, pamoja na kuwajengea uwezo wazalishaji kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
Mkurugenzi huyo amesema, kupitia mafunzo hayo, wadau wanapata uelewa unaoweza kuwasaidia kuboresha taratibu za uzalishaji, kupunguza makosa yanayoweza kuathiri ubora wa bidhaa na kuongeza uwezo wa kushindana katika masoko yenye mahitaji makubwa ya bidhaa bora.
TBS pia imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia kliniki za viwango zinazofanyika katika maeneo mbalimbali, makongamano, maonesho, warsha, semina na mikutano ya wadau.
Amesema, elimu hiyo hutolewa pia kupitia kampeni za wilaya na vyombo mbalimbali vya habari, vikiwemo redio za jamii na za kitaifa, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii.
Njia nyingine zinazotumika ni matangazo, majarida na vipeperushi vinavyolenga kuwafikia wananchi wa makundi mbalimbali.
Dkt. Katunzi amesema, juhudi hizo zina umuhimu katika kujenga utamaduni wa kuzingatia viwango, kuwawezesha walaji kutambua bidhaa bora na kuhamasisha wazalishaji kuzingatia ubora katika kila hatua ya uzalishaji.
MAABARA 14 ZAPATA ITHIBATI YA UMAHIRI
Wakati huo huo, katika kuimarisha uwezo wa kitaalamu wa upimaji na uthibitishaji wa bidhaa, TBS imefanikiwa kuhakikisha maabara zake zote 14 zinapata ithibati ya umahiri wa kimataifa.
Ithibati hiyo inathibitisha kuwa maabara husika zinakidhi matakwa ya viwango vya kimataifa katika wigo wa shughuli zilizoidhinishwa, jambo linaloongeza uaminifu wa matokeo ya vipimo na kurahisisha kukubalika kwake katika mazingira ya biashara.
Amesema, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, maabara hizo zilipima sampuli zaidi ya 188,952 na kufanya ugezi wa vifaa 54,396.
Ugezi wa vifaa ni mchakato muhimu wa kuthibitisha usahihi wa vipimo kwa kulinganisha matokeo ya kifaa na viwango vya marejeo vinavyotambulika.
Dkt. Katunzi amesema, hatua hiyo husaidia kuhakikisha vipimo vinavyofanywa vinaaminika na vinatoa matokeo sahihi.
Kwa upande mwingine, Serikali imetumia kiasi kisichopungua Shilingi bilioni 12.9 kununua na kuimarisha upatikanaji wa mashine na vifaa vya kisasa vya maabara.
Miongoni mwa vifaa hivyo ni mashine ya Hydrostatic Pressure Test, inayotumika kupima uwezo wa mabomba ya maji kustahimili shinikizo.
Amesema, mashine hiyo ina uwezo wa kupima mabomba yenye kipenyo cha milimita 12 hadi milimita 800, sawa na inchi 0.5 hadi 32, na inaweza kupima sampuli 120 kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi huyo amesema, teknolojia hiyo inapatikana katika nchi tano tu kati ya nchi 54 za Afrika ikiwemo Tanzania.
Ametaja mashine nyingine kuwa ni Automatic Conductor Resistance Tester, inayotumika kupima upinzani wa umeme katika nyaya za aina mbalimbali zenye kipenyo kinachofikia milimita 40, sawa na eneo la sehemu ya msalaba la milimita za mraba 1,200.
Mashine hiyo ya kidijitali ina uwezo wa kufanya vipimo na kutoa matokeo kwa haraka, hivyo kusaidia kuimarisha ukaguzi wa ubora wa nyaya za umeme zinazozalishwa au kuuzwa nchini.
Aidha, TBS ina mashine ya Solar Simulator, inayotumika kupima paneli za sola bila kutegemea uwepo wa mwanga wa jua wa moja kwa moja.
Dkt. Katunzi amesema, mashine hiyo inapatikana Tanzania pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Upatikanaji wa vifaa hivyo, amesema unaongeza uwezo wa nchi kupima bidhaa na vifaa vya kiufundi kwa kutumia teknolojia za kisasa, kupunguza utegemezi wa huduma kutoka nje na kuimarisha uaminifu wa matokeo ya vipimo.
MIFUMO YA TEHAMA YAIMARISHA HUDUMA
Katika kuboresha utoaji wa huduma na kupunguza urasimu, TBS imeendelea kutumia mifumo ya TEHAMA katika shughuli mbalimbali za udhibiti wa ubora.
Mifumo hiyo inahusisha utoaji wa leseni za ubora, ukaguzi wa shehena za bidhaa zinazoingizwa nchini na usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi, pamoja na maeneo na vyombo vinavyohusika na uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa bidhaa hizo.
Miongoni mwa mifumo inayotumika ni Online Application System (OAS) na Integrated Standards Quality Management System (i-SQMT).
Dkt. Katunzi amesema, TBS pia imeunganisha mfumo wake wa maombi ya huduma kwa njia ya mtandao na mfumo wa Dirisha Moja la Huduma za Kielektroniki Tanzania unaojulikana kama Tanzania Electronic Single Window System (TeSWS).
Kupitia muunganiko huo, amesema wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa nchini wanaweza kuwasilisha maombi na kupata huduma za taasisi mbalimbali zinazoshiriki katika mfumo huo.
Uboreshaji huo unalenga kurahisisha taratibu za kibiashara, kupunguza muda wa kushughulikia maombi na kuongeza ufanisi katika huduma zinazotolewa kwa wafanyabiashara.
TBS YAUNGA MKONO MATUMIZI YA NISHATI SAFI
Vilevile, katika kuunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, TBS kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na washirika wa maendeleo imeanza mchakato wa kuandaa viwango vya ufanisi wa nishati kwa vifaa vya umeme vinavyotumika majumbani.
Dkt. Katunzi amesema, hatua hiyo inalenga kuhakikisha vifaa vinavyouzwa sokoni vinakidhi viwango vya ufanisi wa matumizi ya nishati na vinakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi unaotakiwa.
Sambamba na uandaaji wa viwango hivyo, shirika linaendelea kuimarisha uwezo wa maabara kwa kupata vifaa vya kisasa vitakavyotumika kupima na kuthibitisha ubora wa vifaa vinavyoingia sokoni.
Juhudi hizo zinatarajiwa kusaidia kupunguza upotevu wa nishati, kupunguza gharama za matumizi kwa wananchi na kuchangia uhifadhi wa mazingira kupitia matumizi ya teknolojia zenye ufanisi zaidi.
Pia, zinaunga mkono juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhamasisha matumizi ya suluhisho endelevu katika sekta ya nishati.
TBS YAVUNA TUZO ZA KITAIFA NA KIMATAIFA
Mafanikio ya TBS katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita yameambatana na kutambuliwa na taasisi mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa kutokana na utendaji wake katika usimamizi wa viwango, uthibitishaji wa ubora na uboreshaji wa huduma.
Dkt. Katunzi amesema, mwaka 2022, shirika lilipata ithibati ya kimataifa katika uthibitishaji wa mifumo kwa kuzingatia kiwango cha ISO 17021-1, iliyotolewa na Shirika la Ithibati la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADCAS).
Mwaka 2023, TBS pia ilitambuliwa kuwa Taasisi Bora ya Udhibiti Barani Afrika na The African Business Leadership Awards ya Uingereza.
Katika mwaka huo huo, amesema Tanzania kupitia TBS, ilifikia ngazi ya nne kati ya tano katika tathmini ya utekelezaji wa Kanuni za Kimataifa za Afya katika eneo la usimamizi wa usalama wa chakula, kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa kuhusu tathmini ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Aidha, wataalamu wa TBS walitambuliwa kupitia tuzo ya ISO Next Generation Award kwa mchango wao katika uandaaji wa viwango vinavyochangia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.
Mwaka 2024, TBS ilipata mafanikio mengine baada ya kuwa taasisi ya kwanza katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kupata ithibati ya kimataifa ya uthibitishaji wa bidhaa katika wigo mpana (wide scope), na kuwa taasisi ya tatu kupata ithibati hiyo ndani ya jumuiya hiyo, kwa mujibu wa taarifa ya shirika.
Mkurugenzi huyo amesema, mwaka 2025, TBS ilitambuliwa kuwa taasisi ya kwanza Tanzania na ya pili Afrika Mashariki kupata ithibati ya umahiri katika mifumo ya ukaguzi kwa kuzingatia kiwango cha kimataifa cha ISO 17020.
Pia, ikawa taasisi ya kwanza katika SADC kupata ithibati ya umahiri katika mfumo wa usimamizi wa chakula kwa kuzingatia kiwango cha kimataifa cha ISO 22003:2022.
Katika kipindi hicho, shirika lilitambuliwa pia kama taasisi inayoibukia katika ufuatiliaji wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa (Antimicrobial Resistance-AMR) katika usalama wa chakula.
Utambuzi huo ulitolewa na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) kwa kushirikiana na Tume ya Umoja wa Afrika inayohusika na rasilimali za wanyama (AU-IBAR).
Aidha, TBS ilipata tuzo ya Taasisi Bora ya Udhibiti nchini kupitia Public Service Innovation Awards.
Mwaka 2026, mafanikio hayo yaliendelea kuongezeka. TBS ilitambuliwa kuwa taasisi ya pili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kutambuliwa uwezo wake wa vipimo katika ngazi ya kimataifa kwa kuchapisha machapisho 18 ya uwezo wa vipimo, yakiwemo 17 yanayohusu joto na moja linalohusu ujazo. Utambuzi huo ulihusishwa na Shirika la Vipimo Duniani (BIPM).
Katika mwaka huo huo, TBS ilitambuliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa mchango wake katika elimu jumuishi.
Shirika hilo pia lilishika nafasi ya tatu katika kuimarisha usimamizi wa utawala na rasilimali watu katika utumishi wa umma, kwa mujibu wa utambuzi uliotolewa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
TBS ilipata pia tuzo ya Taasisi Bora ya Udhibiti Afrika Mashariki kupitia East Africa Public Services Awards.
Vilevile, amesema Msajili wa Hazina alilitambua shirika hilo kama taasisi ya tatu bora ya Serikali iliyofanya maboresho makubwa ya utendaji kwa mwaka hadi mwaka, sambamba na kuongeza gawio lililochangia mfuko wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema, katika mafanikio mengine ya mwaka 2026, TBS ilitambuliwa kuwa taasisi ya pili Afrika Mashariki na ya saba barani Afrika katika kuoanisha mfumo wa udhibiti ubora wa nchi na ule wa bara la Afrika, kwa mujibu wa taarifa ya shirika na utambuzi uliotolewa na ARSO.
Aidha, ilipata tuzo ya Taasisi Bora ya Mfano ya Viwango Barani Afrika kupitia Africa Business and Economy Impact Awards 2026.
Shirika hilo pia lilitambuliwa na Shirika la Viwango Duniani (ISO) miongoni mwa taasisi zinazoongoza duniani katika kuhamasisha elimu kuhusu mbinu bora za uandaaji wa viwango.
Tuzo na utambuzi huo unaashiria maendeleo ya uwezo wa kitaalamu wa TBS na kuimarika kwa nafasi yake katika mifumo ya viwango na udhibiti wa ubora katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.
Pia, unatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za udhibiti, kubadilishana ujuzi na kutumia mbinu zinazokubalika kimataifa katika kulinda afya na usalama wa walaji.
MCHANGO KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA YA 2050
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) imelitaja Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa taasisi ya kimkakati katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kujenga uchumi shindani unaotegemea ubora wa bidhaa na huduma.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa OTR, Bw. Sabato Kosuri ameyasema hayo alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Hazina katika kikao kazi hicho.
Bw. Kosuri amesema, viwango vya ubora vina nafasi muhimu katika kuimarisha ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa, hivyo kuifanya TBS kuwa miongoni mwa taasisi zenye mchango mkubwa katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.
Amesema, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji kujengwa kwa mnyororo imara wa thamani unaounganisha wazalishaji, wafanyabiashara na masoko ya Tanzania, Afrika Mashariki na maeneo mengine ya dunia.
Bw. Kosuri amesema, azma hiyo haiwezi kufikiwa kikamilifu endapo bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini hazitazingatia viwango vinavyokubalika katika masoko husika.
“Bila mifumo imara ya kuhakikisha ubora, itakuwa vigumu kwa bidhaa zetu kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa. Ndiyo maana tunaiona TBS kama taasisi ya kimkakati katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema Bw Kosuri.
Ameongeza kuwa, sekta binafsi inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kufanikisha dira hiyo, lakini mafanikio yake yatategemea pia uwepo wa mazingira yanayowezesha biashara, uzalishaji wenye tija na mifumo madhubuti ya udhibiti wa ubora.
KUENDELEA KUIMARISHA HUDUMA
TBS imeeleza kuwa, itaendelea kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau wengine katika kutekeleza mikakati ya kuimarisha viwango na udhibiti wa ubora.
Juhudi hizo zinalenga kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazoingizwa kutoka nje zinakidhi viwango vinavyotakiwa, huku wazalishaji na wafanyabiashara wakipata huduma zinazowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Uongozi wa shirika hilo pia umeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa usimamizi na kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.
Dkt. Katunzi amesema, ushirikiano kati ya Serikali, uongozi, bodi, wafanyakazi na wadau wa sekta ya viwanda na biashara umekuwa sehemu muhimu ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha 2021 hadi 2026.
Tags
Ashura Katunzi
Bidhaa 9731
Dira 2050
Habari
Msajili wa Hazina
Serikali Awamu ya Sita
TBS
Viwango 3901
Viwango Tanzania









