Dira ya 2050, Balozi Omar aeleza mpango wa uchumi wa dola trilioni 1

DAR ES SALAAM- Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema, upatikanaji wa mitaji, uwekezaji katika viwanda na uboreshaji wa mazingira ya biashara ni muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira 2050, inayolenga kukuza uchumi wa Tanzania kutoka takribani dola za Marekani bilioni 100 hadi dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Ameyasema hayo katika mkutano wa Wadau wa Mpango wa Fedha Mbadala na Ubunifu uliofanyika wakati wa kongamano la Tanzania Startup Week 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Mhe. Balozi Omar amesema, Serikali inaendelea kuweka mazingira yatakayowezesha wawekezaji na wafanyabiashara kuwa na shauku na ujasiri wa kuwekeza mitaji, kwa kuzingatia uelewa wa watu wanaosaidiwa pamoja na sheria zinazosimamia shughuli hizo.

Ameeleza kuwa, kufikia malengo ya Dira 2050 kunahitaji mabadiliko ya kiuchumi na kimuundo yatakayoongeza uzalishaji na kuimarisha sekta zenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Kwa sasa, kilimo kinachangia takriban asilimia 24 ya uchumi wa Tanzania, huku sekta ya viwanda ikichangia asilimia nane, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza mchango wa viwanda katika muundo wa uchumi,”amesema Mhe. Balozi Omar.

Kuhusu mwenendo wa uchumi amesema, uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.6 mwaka 2024 na kufikia asilimia 5.9 mwaka uliofuata, huku lengo likiwa kufikia ukuaji wa asilimia 6.3 mwaka 2026.

Amebainisha pia kuwa, mfumuko wa bei umeendelea kuwa chini ya asilimia tano, sambamba na utulivu wa viwango vya ubadilishaji fedha na nakisi ya bajeti.
Katika eneo la mikopo amesema, mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 33 kwa mwaka ulioishia Agosti, huku sekta ya viwanda ikiwa haijaonesha maendeleo makubwa katika kunufaika na mikopo hiyo.

Balozi Omar amesema, jambo hilo linaloonesha umuhimu wa kuimarisha njia mbadala za upatikanaji wa mitaji, ikiwemo mitaji ya ubia (venture capital) na uwekezaji wa hisa binafsi (private equity).
Aidha, Mhe. Balozi Omar ameeleza kuwa, Serikali imejidhatiti kuendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia mageuzi ya sera na mifumo ya kodi, ikiwemo likizo ya kodi ya mwaka mmoja kwa biashara changa (startups) mpya na mabadiliko ya vizingiti vya kodi, hatua inayolenga kuchochea ukuaji wa biashara changa na kuongeza uwekezaji nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia malengo ya Dira 2050.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here