Waziri Homera aagiza uzinduzi wa Kampeni ya Washa Umeme Vitongojini nchi nzima

NAMTUMBO- Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha Kampeni ya “Washa Umeme Vitongoni” inazinduliwa katika kila mkoa nchini, kwa lengo la kuhakikisha vitongoji vyote vinafikiwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.
Amesema, katika kila mkoa, Meneja wa REA anapaswa kuandaa uzinduzi wa kampeni hiyo utakaoongozwa na Mkuu wa Mkoa husika, ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme na kuhakikisha vitongoji vyote vinapata huduma hiyo ifikapo mwaka 2030.

Mhe. Homera ametoa agizo hilo leo, Oktoba 25, 2026, wakati akiunganisha umeme katika Kitongoji cha Lindi B, Kijiji cha Kumbara, Kata ya Litola, Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma.
Amesema, jumla ya Shilingi milioni 95.4 zimetumika kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika kitongoji hicho, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.

Akizungumzia hali ya usambazaji wa umeme katika Wilaya ya Namtumbo, Mhe. Homera amesema wilaya hiyo ina jumla ya vitongoji 424, ambapo zaidi ya vitongoji 300 tayari vimepata umeme, vitongoji 72 viko katika mpango wa kuunganishiwa umeme, huku vitongoji 38 pekee vikiwa vimesalia.
Amesisitiza kuwa, Serikali inalenga kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinapata huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030, huku kampeni hiyo ikilenga kuimarisha uhamasishaji, uratibu na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya umeme katika ngazi ya mikoa na wilaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here