NA DIRAMAKINI
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Elie Mpanzu amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/27, huku kocha wake, Steven Barker, akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 5, 2026 na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Mpanzu alionesha kiwango bora na cha mwendelezo, akiwashinda Idi Selemani wa Azam FC na Nathaniel Chilambo wa Simba, ambao walifika naye fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi unaofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mpanzu alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Simba mwezi huo, baada ya timu yake kucheza michezo mitatu na kushinda yote, huku yeye akifunga mabao matatu.
Kwa upande wake, Barker aliwashinda Florent Ibenge wa Azam FC na Juma Mgunda wa Namungo, walioingia naye fainali. Chini ya uongozi wake, Simba ilishinda michezo yote mitatu iliyochezwa mwezi Oktoba na kupanda kutoka nafasi ya pili hadi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mabao Bora ya Mwezi
Kamati ya Tuzo pia imeteua mabao matatu bora yatakayopigiwa kura na mashabiki ili kupata Bao Bora la Mwezi Oktoba.
Mabao hayo ni la Hassan Mubiru katika mchezo wa Azam dhidi ya Mbeya City, la Elie Mpanzu katika mchezo wa Simba dhidi ya Young Africans, na la Selemani Bwenzi katika mchezo wa Simba dhidi ya Mashujaa.
Meneja Bora wa Uwanja
Kamati hiyo imemteua Meneja wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Jackson Mwendwa, kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa Mwezi Oktoba, kutokana na kufanya vizuri katika usimamizi wa matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu ya uwanja huo.
Ligi ya Championship
Katika Ligi ya Championship ya NBC, Kamati ya Tuzo imemchagua Ramadhan Kalanje wa KMC kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba, akiwashinda Abdulkarim Segeja wa Kigamboni na Hamdani Ally wa Transit Camp, walioingia naye fainali.
Aidha, kwa upande wa Kocha Bora wa ligi hiyo, kamati ilimchagua Awadh Juma wa Mtibwa Sugar, aliyewashinda Habibu Kondo wa Bandari na Mohamed Muya wa KMC, walioingia naye fainali katika mchakato huo.
