Ukarimu ni tiba bora kwa waathirika wa dawa za kulevya, DCEA yataja mikakati

NA GODFREY NNKO

CHANGAMOTO ya unyanyapaa dhidi ya watu walioathirika na dawa za kulevya hususani kwa wanawake nchini, imetajwa kuwa moja wapo ya sababu kubwa ya wanawake wengi ambao wameathiriwa na dawa hizo kushindwa kufika katika vituo vya matibabu.
Hayo yamebainika ikiwa pia Novemba 10, 2021 katika kikao kazi cha waandishi wa habari za Kidigitali kilichoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) mkoani Morogoro msisitizo ulitolewa kwa jamii kutokuwanyanyapaa waathirika wa dawa za kulevya, badala yake ijenge ukaribu nao na kuendelea kuwapa elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa hizo ili waweze kuondokana na hali hiyo.

Moza Makumbuli ambaye ni Kamishina Msaidizi Kinga na Huduma za Jamii wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) alitoa msisitizo huo wakati akiwasilisha mada katika kikao hicho.

Amesema, kila mmoja akifanikiwa kujenga ukaribu na watu ambao wameathirika na dawa hizo na hatimaye kumuongoza hadi kujinasua katika hali hiyo, hatua hiyo itasaidia kwa kiwango kikubwa kuyadhibiti madhara mbalimbali ambayo yamekuwa yakisababishwa na matumizi au biashara ya dawa hizo.Zinazohusiana soma,tuleteeni taarifa zinazohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya>>>

Amesema, madhara ya dawa za kulevya katika jamii yamegawanyika katika nyanja mbalimbali ikiwemo kiafya, kiuchumi, kimazingira, rushwa, ajali na mambo mengine mengi.

Siku ya Pili

Aidha, katika siku ya pili ya kikao kazi hicho kilichofanyika Novemba 11, 2021 msisitizo umeendelea kutolewa kwa jamii kutowanyanyapaa hususani wanawake, kwani utafiti umeonesha kuwa kati ya wanawake 100 wanaotumia dawa za kulenya nchini 61 kati yao wameambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutokana na kuchangia sindano za kujidunga.
Kamishina wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Dkt. Peter Mfisi ameyasema hayo alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi hicho huku akibainisha kuwa, utafiti huo ulifanyika mwaka 2014 ambapo mpaka sasa bado haujafanyika utafiti mwingine ili kujua ukubwa wa tatizo.

Dkt.Mfisi amesema kuwa, kutokana na tatizo hilo,DCEA imejipanga kuanzisha kliniki maalumu za waraibu wa dawa za kulevya zitakazowasaidia waraibu wanawake kupata matibabu kwa wakati na kliniki hiyo itawaondolea tatizo la kuwa na hofu ya kunyanyapaliwa.

Kamishina huyo amesema kuwa, lengo kuu la kikao kazi hicho ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari za Kidigitali kuihabarisha jamii ya Kitanzania hususani waathirika wa dawa za kulevya pamoja na VVU ili kuchukua hatua stahiki za kimatibabu.
Mkufunzi wa masuala ya maudhui ya kidigitali, Dotto Mnyadi akiwasilisha mada katika siku ya pili ya kikao kazi hicho na waandishi wa habari za kidijitali kilichoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) katika Hoteli ya Queen mkoani Morogoro Novemba 11, 2021.

“Lengo kuu la kikao kazi hiki ni kutaka kuifikia jamii kupitia ninyi wanahabari ili kuihabarisha jamii ifahamu juhudi za mamlaka katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na nini wanapaswa kufanya hasa wanapoona kuna waathirika miongoni mwao. Pia kusaidia kutafuta mbinu za kuwashawishi wanawake wafike kwenye maeneo ya tiba na kujiunga na vituo vya matibabu, maana tunajua wapo na wameathirika na dawa za kulevya, lakini kwa sababu ya unyanyapa wanaogopa kujitokeza katika vituo,"amesema Dkt.Mfisi.

Wakati huo huo,Dkt.Mfisi amesema, kwa sasa idadi ya wanawake wanaotumia dawa za kulevya wanaokwenda katika vituo vya matibabu ni wachache.

"Kwa mfano ukiangalia katika Sober House (nyumba za upataji nafuu) unakuta kiwango cha wanawake wanaojitokeza kupata matibabu ni kidogo sana na hata ukichukua ile jumla ya matibabu wanawake bado wako chini ya asilimia tano. Katika kliniki nyingine unakuta wako asilimia tatu au asilimia nne kwa uwakilishi wa wanawake ni mdogo.

"Pia hawaendi kwenye vituo vya matibabu, kwa hiyo mamlaka tuna kila sababu ya kuweka vituo maalumu ili kuwafanya wanawake nao wajitokeze katika matibabu kwa wale ambao wamekuwa na uraibu wa dawa za kulevya, sehemu ya vivutio hivyo labda kutafuta kliniki itakayokuwa na mahitaji maalum ya wanawake ili wajitokeze kwa wingi.

Kamishina huyo amesema kuwa, kliniki hizo zitakuwa na uwezo wa kuwahudumia watoto wadogo waliozaliwa na uraibu na ambao kwa kiasi kikubwa huwa wanazaliwa wakiwa na tatizo la arosto kutokana na matumizi ya dawa za kulevya kwa mama mjamzito.Pia hii inahusiana,DCEA yasisitiza uvutaji wa shisha ni kirusi hatari, Dkt.Mlondo afichua yaliyofichika >>>

"Watoto wengi wanaozaliwa na akinamama wanaotumia dawa za kulevya wanakuwa na arosto, kliniki hizo zitakuwa na uwezo wa kuwasaidia watoto wote waliozaliwa na tatizo hilo.Pia kliniki hizo zinaweza kuwa na meneo ya kucheza watoto, kama mama amekuja na mtoto basi anampeleka kucheza au kunakuwa na elimu ya mama na mtoto, inakuwa zaidi ya ile kliniki ambayo mama anakwenda na kuondoka , ukiacha kutibu hiyo arosto ambayo mtoto anakuwa nayo, lakini kunakuwa na vitu vingine,"amesema.

Dkt.Mfisi amesema, pia kuna baadhi ya wanawake wanashindwa kwenda kupata matibabu kwa sababu ya muda, kwani mara nyingi matibabu yanaanza saa kumi na mbili asubuhi hadi saa tano asubuhi.

"Kutokana na changamoto hiyo, tunadhani ni vema wakaangalia na muda mwingine ili wawepo wanaokwenda asubuhi na wanaokwenda jioni kulingana na ratiba zao ili waweze kupata matibabu,"amesema.

WANASEMAJE?

Kwa nyakati tofauti baadhi ya waathirika wa dawa za kulevya ambao wapo chini ya uangalizi wa nyumba ya upataji nafuu (sober house) ya Free at Last iliyopo mjini Morogoro wamesema, unyanyapaa ni moja wapo ya sababu kubwa inayowafanya waumie nafsi zao.
Mmoja wa waraibu Abel Leonard ambaye anaendelea na uangalizi kutoka mkoani Mbeya anasema kuwa, hawafurahi kuwa katika hali hiyo, kwani hata yeye alijikuta ameangukia katika janga hilo baada ya kupoteza wazazi wote na kukosa marafiki wema wa kumuongoza.

Amesema, anajutia kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, kwani yamemvurugia mfumo wa maisha yake na anaamini akipona ataenda kuwa balozi mwema huko mtaani, kwa kuwa matumizi ya dawa hizo hayana faida badala yake amepoteza muda na kila kitu.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya waandishi wa habari wanaoendelea na kikao kazi cha siku tatu kuanzia Novemba 10 hadi 12, 2021 cha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) mjini Morogoro.

Ziara hiyo ya Novemba 11, 2021 ilikuwa sehemu ya mafunzo ambapo msimamizi wa nyumba ya Free At Last, Michael Cassian amesema, jamii ikifanikiwa kuushinda unyanyasaji na unyanyapaa kwa waathirika wa dawa za kulevya huo utakuwa ni uponyaji tosha kwao.
Pia amesema, ukosefu wa elimu sahihi kwa jamii kuhusu watu waliothiriwa na dawa za kulevya umesababisha kukithiri kwa matukio ya udhalilishaji kwa waathiriwa hao ikiwemo kuigizwa na kuitwa majina yasiyofaa kama vile mateja na mengine mengi jambo ambalo halipaswi kuungwa mkono.

"Huko mitaani jamii inatuita majina ya kila aina na wengine hata wanatuigiza jambo ambalo siyo sahihi kwani linazidi kutukandamiza sisi waathiriwa,mimi nadhani hii inatokana na jamii kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu tatizo la uraibu wa dawa za kulevya,"amesema.

JE? MRAIBU ANAPELEKWA JELA?

Kamishna wa Tiba na Kinga wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya,Dkt.Peter Mfisi amesema, sheria inatambua kuwa uraibu ni ugonjwa, hivyo hukumu pekee ni kumpeleka mraibu hospitali na siyo jela kama jamii inavyofikiria.
Dkt.Mfisi anasema kuwa,Jeshi la Polisi limekuwa likitumia weledi mkubwa wanapowakamata waraibu wa dawa za kulevya ambapo hushirikiana na familia zao kuwasainisha matibabu ya lazima ya kuondokana na uraibu kwa muda wa miezi sita.

"Jambo la kushangaza,wengi wao wamekuwa hawafuati adhabu hiyo na kurudi kwenye matumizi ya dawa hizo haramu,"amesema.

Dkt.Mfisi anasema kuwa, adhabu hiyo ni kwa wale waraibu wanaokamatwa na makosa ya kukutwa wakitumia dawa hizo na siyo wale wanaokamatwa wakifanya uhalifu mwingine baada ya kutumia dawa za kulevya.

"Kwa hao wengine wanaokamatwa kwa tuhuma za wizi au kumdhuru mtu,sheria huchukua mkondo wake kama kawaida ila nafikiri wakati mwingine polisi hutumia busara na kulazimika kuwaachia kutokana na hali zao kiafya kushindwa kuhimili kukaa mahabusu kwa muda mrefu hususani wanapopatwa na arosto,"ameongeza

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news