Katibu CWT Taifa asafiri kilomita 540 kupiga kura

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Taifa, Mwalimu Deus Seif amelazimika kusafiri zaidi ya kilomita 540 kutoka jijini Dodoma kuja Geita kupiga kura katika kituo cha kupigia kura katika Shule ya Msingi Nyanza katika Jimbo la Uchaguzi la Geita Mjini, ambalo ndilo eneo alipojiandikisha kwa ajili ya kupiga kura,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Taifa,Mwalimu Deus Seif baada ya kumaliza kupiga kura katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Nyanza Geita Mjini leo Oktoba 28,2020. (DIRAMAKINI).

Mwalimu Deus Seif amesema, amelazimika kusafiri umbali mrefu, hivyo ili kuja Geita kupiga kura kutimiza haki yake ya kuchagua viongozi anaowaona wanafaa kwa ngazi ya Urais,Ubunge na Udiwani baada ya kuona asipofanya hivyo atapoteza haki ya kuchagua viongozi wanafaa kwa sababu kila mpiga kura anastahili kupigia kura katika kituo alichoandikishiwa.

Katibu huyo wa Chama cha Walimu Taifa amewasihi wananchi wengine kujitokeza kupiga kura ili kutimiza haki yao ili kupata kiongozi bora wa kuwaongoza kwa maslahi ya taifa na kwa maslahi na maendeleo yao.

Katibu huyo wa Chama cha Walimu Taifa amepongeza wananchi kwa namna wanavyoendelea kushiriki zoezi hilo kwa hali ya amani na utulivu katika vituo vya kupigia kura hasa katika Jimbo la Geita Mjini ambalo yeye ameshiriki kupiga kura.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa hali ya mkoa wa Geita ni tulivu na wananchi wamejitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura na kusisitiza kuwa hali ya usalama na amani imetawala katika mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel (katikati) akiwa kwenye mstari wa kuingia kwenye kituo cha kupigia kura Shule ya Msingi Nyanza Jimbo la Geita Mjini leo Oktoba 28,2020 (DIRAMAKINI).

Amesema hayo akiwa katika mstari wa kuingia katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Nyanza Geita Mjini ambapo amesema wananchi wa mkoa wa Geita wameonyesha utulivu wa kutosha wa kushiriki zoezi hilo kwa amani.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Geita Mjini amesema kuwa, jumla ya wapiga kura 146,503 katika jimbo la Geita Mjini wanatarajiwa kujitokeza kupiga kura za kuwachagua madiwani,wabunge na Rais katika vituo 371 vya kupiga kura ambavyo mapema leo asubuhi vimefunguliwa vyote ili wananchi watumie haki yao ya msingi kwa kuwapigia kura viongozi wanaowataka ili wakatumikie katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katika Jimbo la Geita mjini jumla ya vyama vya siasa sita ambavyo ni CHADEMA, CCK, CCM, CUF, NCCR MAGEUZI, pamoja na ACT WAZALENDO vimesimamisha wagombea ubunge na udiwani katika kata 13 ambapo mwitikio wa wananchi kujitokeza kwenye vituo vya kupigia kura ni mkubwa katika maeneo mbalimbali.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Geita Mjini, Costantine Kanyasu aliyepiga kura katika kituo cha kupigia kura cha Ofisi ya Mtaa Katoma amesema, zoezi linaendelea vizuri na mwitikio wa wananchi ni mzuri.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Geita Mjini, Costantine Kanyasu akiwa katika mstari wa kuingia kwenye chumba cha kupigia kura cha Ofisi ya Mtendaji wa Mtaa Katoma Jimbo la Geita Mjini leo Oktoba 28,2020. (DIRAMAKINI).

Kanyasu amesema kuwa,kulikuwa na dosari za mawakala wa vyama vya siasa barua zao za utambulisho kupelekwa kwenye vituo tofauti na vituo vyao walivyo pangiwa lakini anasema msimamizi wa uchaguzi alilitatua haraka.

Ngusa Juda ambaye ni mkazi wa Geita Mjini amesema kuwa, katika zioezi la kupiga kura kumekuwa na usumbufu kwa wapiga kura baada ya baadhi ya wananchi kukuta majina yao yamehamishiwa kwenye vituo vingine vilivyogawanywa na tume tofauti na walipoandikishwa awali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news