Miaka 38 ya kutojua nani mmiliki wa mali alizoacha marehemu

Familia ya Mzee Bomboma iliyopo kijiji cha Kiyongwile kata ya Msalabani Wilaya ya Kilombero wameishi miaka 38 bila kujua nani mmiliki wa mali alizoacha marehemu baba yao Mzee Bomboma aliyefariki mwaka 1981, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Familia hiyo ina watoto watano ambao ni Ally Bomboma,Salma Bomboma,Rashid Bomboma,Zuber Bomboma na Pamela Bomboma,watoto hao walizaliwa na mama wawili tofauti ambao ni Mariamu Mateka na Zuhura Mohamed.

Wazazi wao, (wajane) Mariamu Mateka na Zuhura Mohamed walijaribu kuwashirikisha ndugu wote na viongozi wa serikali za vijiji lakini hawakufikia muafaka kuhusu mgawanyo wa mali zilizoachwa na Mzee Bomboma.

“Hali hii imejitokeza kutokana na Mzee Bomboma kufariki pasipo kuacha wosia juu ya umiliki wa mali. Ikumbwe “wosia ni tamko au maandishi anayotoa mtu akieleza jinsi mali zake zitakavyogawiwa kwa warithi wake baada ya kifo chake,"amesema.

Baada ya sintofahamu ya muda mrefu,Pamela mtoto wa marehemu alifika Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria Ifakara, kuomba ushauri wa kisheria kuhusu mgawanyo wa mali zilizoachwa na baba yao,alifika kituo hapo baada ya kupata taarifa kwamba kuna kituo kinatoa huduma na ushauri wa kisheria bure.

Mama Pamela alipofika ofisi ya Wasaidizi wa kisheria alieleza lengo la kufika kituoni hapo,alipenda kujua utaratibu wa kufungua mirathi,na alitaja mali zilizoachwa na baba yao kuwa ni mashamba ya hekari 15, Viwanja 7 na nyumba 2. Mali hizo zimedumu kwa takribani miaka 38 bila kuwa na mrithi halali.

“Tulishindwa kugawana mirathi kutokana na sisi kuzaliwa mama tofauti, hivyo baadhi yetu waliona wao wanahaki zaidi ya wengine,pia baadhi yetu tuliishi na kulima katika maeneo hayo bila kujua uhalali wa kumikili,"anasema Pamela.

Baada ya kusikilizwa,Wasadizi wa Kisheria,Kapaya na Amasha Sepela walichuku jukumu la kuita familia hiyo kwa lengo la kukaa pamoja na kutafuta suluhu kwa amani,baada ya kuona baadhi yao kungangania mali na kutojua sheria ya mirathi inavyofanya kazi.

Familia hiyo waliitika wito na kufika kituoni hapo,walipofika walipewa nafasi ya kuongea na kila mmoja alifanikiwa kusema anavyofahamu mali hizo na walizochukua kutatua mgogoro bila mafanikio.

Baada ya kusikilizwa,Msaidizi wa Kapaya na Amasha waliwapa elimu juu ya mirathi,umuhimu wa mirathi na madhara yatakayotokea kama hawata jipanga kufungua mirathi,pamoja na msimamizi wa mirathi kutambulika na familia na vyombo vya sheria.

“Msimamizi wa miradhi atakayependekezwa afungue miradhi katika mahakama ya mwanzo,hii itasadia kutambulika na vyombo vya sheria na kufanya mgawanyo wa mali akiwa na kibali maalumu,kila mtoto na mjane ana haki ya kupewa mali hizo,"anasema Kapaya.

“Ni mahakama pekee yenye uwezo wa kuteua msimamizi wa mirathi,ukoo au ndugu wa marehemu hutoa mapendekeozo tu juu ya mtu anayefaa kuwa msimamizi wa mirathi,”amesema.

Baada ya kupatiwa elimu,waliondoka na kwenda kuitisha kikao cha familia na kumchagua msimamizi wa mirathi,ambaye alichaguliwa John Lupia,na kuomba zoezi hilo lisimamiwe na kituo cha Wasadizi wa Kisheria Ifakara na viongozi wa serikali ya kijiji na lisipelekwe mahakamani kama sheria inavyosema.

Familia hiyo ilifanya kikao cha mgawanyo wa mali kwa kufuata utaratibu,chini ya uangalizi wa wasadizi wa kisheria na watoto wote walikubaliana na kikao hicho pamoja na utaratibu utakaotumika kugawa mali na kuomba kila kinachofanyika kiwekwe kwenye maandishi.

Mali hizo ziligawanywa kama ifuatavyo,Mariamu Mteka alipata nyumba moja,shamba ekari mbili,kiwanja kimoja, Zuhura Mohamed alipata shamba ekari tatu,viwanja mbili,Salma alipata nyumba, shamba ekari mbili,kiwanja kimoja,Ally alipata shamba ekari mbili na kiwanja kimoja,Rashid alipata shamba ekari mbili,kiwanja kimoja,na Zuber alipata shamba ekari mbili na kiwanja kimoja.

Mama Pamela ambaye ndiye aliyefikisha mgogoro huo Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria Ifakara alifanikiwa kupewa nyumba moja na shamba ekari mbili. Hivyo wanafamilia hao kwa sasa wanafuraha kwa sababu wanaendesha maisha yao kwa mali walizogawana,na kila mtoto anatumia mali aliyopata kwa ajili ya uzalishaji.

“Mgogoro wetu wa miradhi umedumu miaka 38, nakishukuru kituo cha msaada wa sheria Ifakara kuweza kushughulikia kikamilifu,kutuelekeza namna ya kufanya na tumeweza kugawana mirathi chini ya usimamizi wao,kila mmoja amepata haki yake”Anasema Pamela.

Katika mgawanyo wa mali hizo,Pamela alipata nyumba na shamba hekari mbili,kupitia shamba hilo analima mazao ya chakula,nyumba aliyopewa ina vyumba vitatu,amepangisha kwa shilingi 15,000/= na fedha hizo anatumia kununua vifaa vya shule vya watoto na kujikimu.

Familia hiyo hivi sasa inaishi kwa amani na kila mtoto anatumia mali aliyopata kwa kuzalisha,na hakuna anayemwingilia mwingine katika mali aliyopata au eneo alilopata kwa ajili ya kilimo,wasaidizi wa kisheria kwa kushirikiana na serikali ya kijiji wanaendelea kufuatilia familia hiyo lengo kuhakikisha wanaishi kwa amani na upendo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news