Rais Magufuli aokoa Bilioni 61/- za ushirika

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli imefanikiwa kurejesha mali za vyama vikuu vya ushirika Nyanza, Geita na Simiyu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 61 zilizokuwa zikilikiwa kinyume cha utaratibu, anaripoti Mwandishi Diramakini. 

Akikabidhi hati 37 kwa wenyeviti wa vyama vya Nyanza (NCU),Geita (GCU) na Simiyu (SIMCU) Novemba 23, 2020) jijini Mwanza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema kazi hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli aliyoyatoa mwezi Agosti mwaka 2016. 

“Leo nimekabidhi hati miliki 37 zinazojumuisha ardhi, majengo na mitambo yenye thamani ya shilingi Bilioni 61 zilizoporwa kinyemela na watu kutoka vyama vya ushirika Nyanza, Geita na Simiyu ambao ndio walikuwa wamiliki halali,"amesema Kusaya. 

Kusaya ameongeza kusema kuwa, kazi hiyo ya kufuatilia na kurejesha mali imefanywa na Timu Maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwaka 2016 baada ya agizo la Rais Magufuli alipofanya ziara mkoani Mwanza kuwa mali zote za chama kikuu cha ushirika Nyanza zifuatiliwe na kurejeshwa toka kwa waliozimiliki kinyume cha utaratibu. 
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,John Mongela ( kushoto) akikabidhi hati miliki 37 za mali zilizokuwa za vyama vikuu vya ushirika Nyanza,Geita na Simiyu kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia) jijini Mwanza. Mali hizo zilizorejeshwa zina thamani ya shilingi Bilioni 61. 
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya akikabidhi hati miliki kwa mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Nyanza, Bw. Benjamin Mikomangwa (kulia) katika hafla iliyofanyika Mwanza. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela. 
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya akikabidhi hati miliki tisa kwa Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Geita ( GCU), Bibi Zainabu Mahenge (kulia) jijini Mwanza. 

Ili kuhakikisha wanaushirika wananufaika na mali zao Katibu Mkuu Kusaya ametoa maagizo kwa viongozi wa vyama vya ushirika nchini kuwa kurejeshwa kwa mali hizo zitumike kwa manufaa ya wakulima ambao ndio wamiliki. 

Pili, Mrajis wa Ushirika nchini ahakikishe mali zilizorejeshwa zinakuwa salama na kuwa asitokee kiongozi yeyote atakayefanya ubadhirifu. 

Tatu, kwa watu wote ambao bado wanamiliki zilizokuwa mali za ushirika kinyume cha utaratibu wazirejeshe mara moja kwa serikali kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa kupitia Timu Maalum ya Waziri Mkuu. 

“Nyanza kuna jengo lipo Nansio Ukerewe linaitwa Pamba Hostel imebainika mkataba wake na Saad Songolo ulikiukwa. Tunataka lirudishwe Serikalini, hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tunaomba uruhusu vyombo vya dola vifanye kazi yake ili mali hii ya wakulima irejeshwe,”amesema Kusaya. 
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya akikabidhi hati miliki kwa mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Simiyu ( SIMCU), Bw. Emanuel Mboyi (kulia) katika hafla iliyofanyika Mwanza. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela. 
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akiongea kwenye hafla ya kukabidhi mali za vyama vikuu vya Ushirika vya Nyanza, Geita na Simiyu ambazo ziliporwa kinyume cha utaratibu kazi iliyofanywa na Timu Maalum Waziri Mkuu. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya na kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Bw. Emanuel Tutuba.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela ametoa pongezi kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa uthubutu wao na uzalendo wa kutaka mali zote za wanashirika zilizochukuliwa kinyemela kurejeshwa kwa wamiliki ambao ni wakulima. 

Mongela amesisitiza kuwa mkoa wa Mwanza tangu agizo lilipotolewa viwanja vya Furahisha tarehe 11 Agosti, 2016 umeshirikiana na Timu Maalum ya Waziri Mkuu kwenye ufuatiliaji na hatimaye kufanikiwa leo kurejesha mali hizi 27 za chama kikuu cha Nyanza na zingine za Simiyu na Geita. 

“Leo tunamshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajali wakulima, wafugaji na wavuvi wa nchi hii hata kuagiza uchunguzi wa mali zao zilizoporwa na wajanja wachache kwenye ushirika,” amesisitiza Mongela 

Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela alimpongeza Mwenyekiti wa kwanza wa Timu Maalum ya Waziri Mkuu ambaye sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya kwa kazi nzuri ya kufuatilia urejeshwaji mali hizo kazi iliyokamilisha na timu ya pili chini ya Asangye Bangu. 
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya mali zilizokuwa za ushirika zilizorejeshwa serikalini jijini Mwanza ambapo julma ya hati 37 zenye thamani ya shilingi Bilioni 61 zimekabidhiwa tena kwa Nyanza, Geita na Simuyu. 
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela (kushoto) akipokea hati miliki za ardhi,majengo na mitambo zilizorejeshwa kwa vyama vya ushirika toka kwa Mwenyekiti wa Timu Maalum ya Waziri Mkuu Bw. Asangye Bunga ( kulia) jijini Mwanza. Timu hiyo maalum iliundwa na Waziri Mkuu ikiwa ni agizo alilotoa Rais Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Agosti 2016. 
Picha ya pamoja ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella (katikati) na Katibu Mkuu Kilimo, Bw. Gerald Kusaya wakiwa na viongozi wa vyama vikuu vya ushirika vya Nyanza, Geita na Simiyu wakati wa hafla ya urejeshwaji mali za ushirika zilizorejeshwa kupitia Timu Maalum ya Waziri Mkuu. (Picha na Wizara ya Kilimo). 

Aidha Mongela ametoa onyo kwa Viongozi wa Nyanza Cooperative Union kuwa wasimamie vizuri mali hizi ili zisije tena kuuzwa kwa watu kinyume cha utaratibu na kuwa sasa Nyanza inatakiwa kuwa na Mtendaji Mkuu mwenye weledi na ujuzi wa kusimamia ushirika. 

Mongela ameiomba wizara ya kilimo “ ifanye kazi ya kuhakikisha vyama vikuu vya ushirika vinapata na kuajili mameneja wakuu wenye weledi, taaluma, ujuzi na uadilifu kuongoza ushirika ili vijiendeshe kibiashara badala ya kutumia uzoefu tu usio na tija” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. 

Akiwasilisha taarifa Mwenyekiti wa Timu Maalum ya Waziri Mkuu Asangye Bangu alisema mali hizo zilizorejeshwa ni sehemu ya zoezi endelevu la kufuatilia watu wote waliojimilikisha au kuuziwa zilizokuwa mali za ushirika kinyume cha utaratibu. 

Bangu alitaja mali zilizorejeshwa kwa vyama vikuu vya ushirika Nyanza kuwa ni 27, Geita 9 na Simiyu 2 zikiwamo viwanja, majengo na mitambo na kuwa timu yake inaendelea kufuatilia mali zingine kwenye vyama hivi na vingine ikiwemo Kilimanjaro( KNCU) Shinyanga (Shirecu) na maeneo mengine. 

Akitoa shukrani kwa niaba ya wanaushirika nchini Mrajis wa Ushirika Dkt. Benson Ndiege amesema kurudishwa kwa mali za ushirika kutasaidia kufufua na kuimarisha utendaji kazi wa vyama vya ushirika nchini. 

Dkt. Ndiege amesema atahakikisha mali zilizorejeshwa zinatumika kwa manufaa ya wakulima ili ziwasaidie kuondokana na umasikini wa kipato .

Post a Comment

0 Comments