Rais Dkt.Mwinyi ateta na Balozi wa Morocco katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza azma ya Zanzibar kukuza na kuimarisha uhusiano kati yake na Morocco hasa katika sekta ya utalii, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Dkt. Hussein ameyasema hayo Novemba 19,2029 katika mazungumzo kati yake na Balozi wa Ufalme wa Morocco katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdelilah Benryane, mazungumzo yaliofanyika Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Hussein amesema kwamba kutokana na Morocco kupata mafanikio makubwa katika sekta ya utalii, ni vyema Zanzibar ikapanua wigo kutoka nchi hiyo.

Amesema kuwa kwa vile Zanzibar inategemea sana sekta ya utalii katika uchumi wake itakuwa vyema kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja kati ya pande mbili hizo ili Zanzibar ipate mafanikio kama yale iliyoyapata Morocco katika sekta hiyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Balozi wa Morocco nchini Tanzania,Abdelilah Benryane alipofika Ikulu Mjini Zanzibar.

Dkt. Hussein alirejesha salamu za pongezi zilizotoka kwa kiongozi wa Morocco kupitia Balozi huyo Mfalme Mohammed VI, zilizomtakia kazi njema na mafanikio katika uongozi wake mpya wa Urais wa Zanzibar huku akiahidi kuzidisha ushirikiano wake kwa nchi hiyo.

Aidha, Dk. Hussein alimueleza kiongozi huyo juhudi zitakazochukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kuimarisha sekta ya utalii na kusisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja katika sekta hiyo hasa ikizingatiwa kwamba Morocco ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika iliyopiga hatua kubwa katika sekta ya utalii.

Pamoja na hayo, Dk. Hussein alimueleza Balozi huyo umuhimu wa kushirikiana katika sekta nyenginezo za maendeleo hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ina kiu kubwa ya maendeleo hivi sasa.

Sambamba na hayo, Dk. Hussein alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa Morocco kuja kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo.

Nae Balozi wa Morocco katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Abdelilah Benryane, alianza kwa kumfikishia salamu za pongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kutoka kwa Mfalme wa Morocco Mohammed VI, kufuatia ushindi wa kishindo wa Urais wa Zanzibar.

Balozi huyo alimueleza Rais Dk. Hussein kwamba Morocco inajivunia uhusiano na ushirikiano mwema uliopo kati yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Balozi Abdelilah Benryane, alisema kuwa Morocco iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika sekta ya utalii, pamoja na sekta nyengine zote muhimu huku akieleza azma ya nchi yake ya kutoa nafasi za masomo katika kada mbali mbali kwa wanafunzi wa elimu ya juu wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na nafasi za masomo ya elimu ya dini.

Balozi huyo pia, alieleza utayari wa nchi yake katika mashirikiano kupitia mafunzo ya masuala ya kitalii kupitia chuo chake ambacho kina mahusiano na nchi kadhaa za Ulaya na nyenginezo duniani
Aidha, alieleza haja ya kuwepo mashirikiano ya kubadilishana uzoefu na utaalamu kwa wanafunzi wa Zanzibar na wale wa nchi yake kutokana na nchi hiyo kuwa na vyuo vingi vinavyotoa mafunzo kadhaa.

Akizungumzia juu ya sekta ya utalii, alisema kuwa nchi yake imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo na kupokea wageni wengi hasa katika program ijulikanayo ‘Azur Blue’ iliyoanzishwa na kiongozi wa nchi hiyo Mfalme Momamed VI.

Hivyo, alieleza kuwa nchi yake itakuza uhusiano na Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo hasa ikizingatiwa kuwa nchini mwake kuna miundombinu mingi ya kuimarisha sekta hiyo vikiwemo vyuo vya mafunzo ya kitalii.

Mapema Rais Dk. Hussein Mwinyi alikutana na uongozi wa Benki ya Standard Chartered ukiongozwa na Bwana Sanjay Rughani ambapo katika maelezo yake Rais Dk. Hussein aliueleza uongozi huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imeahidi kufanya mambo mengi kwa wananchi hasa kwa kushirikiana na Sekta binafsi.

Alisema kwamba Serikali iko tayari kushirikiana na Taasisi mbali mbali zimkiwemo za binafsi huku akisisitiza kwamba miongoni mwa taasisi hizo sekta ya benki ni muhimu sana.

Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imeahidi mambo mengi kwa wananchi hivyo, mashirikiano na Benki ikiwemo Benki hiyo ya Kimataifa ya ‘Standard Chartered’ ni muhimu katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.

Alieleza kwamba iwapo ipo fursa ya kukaa pamoja na kujadili miradi ipi ya kutekelezwa kwa pamoja Serikali iko tayari hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar inahitaji wawekezaji kuja kuekeza katika maeneo mbali mbali.

Nae kiongozi huyo wa ujumbe huo Sanjay Rughani alimpongeza Rais Dk. Hussein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na kueleza matarajio yake makubwa kutokana na ari na hamu ya Rais huyo kuiletea maendeleo Zanzibar.

Kiongozi huyo alieleza kazi za Benki hiyo na namna inavyofanya kazi zake ndani nan je ya Tanzania huku akieleza azma ya Benki hiyo ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Sambamba na hayo, kiongozi huyo alieleza jinsi Benki hiyo inavyofanya kazi na Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wizara ya Fedha ya Zanzibar pamoja na Benki mbali mbali hapa nchini ikiwemo Benki Kuu (BOT).

Pamoja na hayo viongozi hao walieleza shughuli mbali mbali zinazofanywa na Benki hiyo katika kuisaidia jamii ikiwemo kutoa huduma za tiba ya macho, kuwasaidia watoto wa kike, uwekaji hakiba wa kifedha pamoja na mambo mengineyo.

Post a Comment

0 Comments