Tanzania yaahidi kuendelea kuisaidia Congo DRC kulinda amani

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuendelea kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kulinda amani na kuhakikisha changamoto za ulinzi na usalama zinazoikabili nchi hiyo zinatatuliwa ili kuimarisha hali ya amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) alipokuwa akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika Mkutano wa Nane wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika kwa njia ya video (Video Conference).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akifuatilia Mkutano wa Nane wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika kwa njia ya video (Video Conference) jijini Dodoma. Rais wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo, Mhe. Felix Tshisekedi akizungumza katika mkutano wa Nane wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR).

“Tanzania tutaendelea kusaidia juhudi za kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo la mashariki mwa Congo – DRC kwani kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kiusalama kwa nchi hiyo kunahatarisha usalama wa eneo lote la Jumuiya nzima ya ICGLR nayo itakuwa salama,” amesema Prof. Kabudi.

Ameongeza kuwa, Congo Brazaville ilikuwa ikikabiliwa na uasi kutoka kundi la Ninja lililokuwa likiisumbua Serikali kwa miaka mingi hata hivyo hadi kufikia katikati ya mwaka 2019 uasi ulitulia kufuatia mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya kundi hilo na Serikali.

Amesema, Congo-Kinshasa na Congo-Brazaville ni muhimu katika eneo la maziwa makuu kutokana na kuwepo kwa asilimia kubwa ya rasilimali za misitu, maji na madini ambavyo vinahitajika sana duniani na kuongeza kuwa umuhimu zaidi unahitajika kutokana na ukweli kuwa kuna haja kubwa ya kutunza mazingir
a, kuzalisha nishati na kukuza uchumi wa dunia.

Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa, Bw. António Guterres akizungumza katika mkutano wa Nane wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR).

“Nchi hizi mbili za DRC na Congo Brazaville ni nchi muhimu sana katika eneo la Maziwa Makuu kutokana na kuwepo kwa asilimia kubwa ya rasilimali, baadhi ya rasilimali hizo kama misitu, maji na madini zinahitajika sana duniani kwa sasa kutokana na umuhimu wake, umuhimu ambao unatokana na haja ya kutunza na kulinda mazingira, uzalishaji wa nishati na kukuza uchumi wa dunia,”amesema.

Waziri ameongeza kuwa, kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kiusalama katika nchi hizi kunahatarisha usalama wa eneo lote la Maziwa Makuu ikiwemo na usalama wa dunia kutokana na uwezekano wa baadhi ya mataifa makubwa kugombea rasilimali hizo.

Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya ICGLR umepokea na kujadili taarifa mbalimbali kuhusu jumuiya hiyo, mbali na hali ya kisiasa na kiusalama katika ukanda huo umeangalia pia suala la michango ya wanachama katika bajeti ya Sekretariat na Mfuko Maalum wa maendeleo, taarifa ya mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya, taarifa ya mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi kuhusu hali ya usalama wa Ukanda wa Maziwa Makuu na taarifa ya mkutano wa Mawaziri wa Afya. Rais wa Jamhuri wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame akizungumza katika mkutano wa Nane wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR).

Nchi wanachama wa ukanda wa maziwa makuu ni pamoja na Angola, Burundi, Jamhuri ya Kati, Demokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kongo, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudani Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia.

Oktoba 2019, Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ulifanyika nchini Congo Brazzaville.

Katika tukio jingine, Prof. Kabudi amekutana na kumuaga Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Bw. Alex Mubiru ambapo pamoja na mambo mengine amemshukuru Bw. Mubiru kwa mema aliyoyafanya hapa nchini hasa katika kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua kimaendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news