Rais Magufuli: Hakika yajayo Zanzibar ni neema tupu, hongereni sana

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewahakikishia wananchi wa Zanzibar pamoja na viongozi wake kwamba ataendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha umoja na maelewano yaliopo yanaendelezwa sambamba na kuiimarisha Serikali ya Umoja wa Kaitaifa ili Zanzibar izidi kupata maendeleo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad mara baada ya mazungumzo yao katika Ikulu ndogo ya Chato mkoani Geita leo tarehe 14 Januari 2021. (Picha na Ikulu).

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Januari 14, 2021 katika hotuba yake fupi mara baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwiyi pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad huko Chato mkoani Geita. 

Rais Magufuli amewapongeza viongozi hao pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla kwa kuanza kuona mwanga wa maendeleo na kusema kuwa amekutana nao kutokana na viongozi hao kuwa pamoja kwani hakuna Zanzibar bila ya Tanzania.

Katika hotuba yake hiyo amewataka Wazanzibari kuendelea kuchapa kazi na kuwahakikishia kwamba ataendelea kuwaunga mkono katika maendeleo ya Zanzibar na kamwe hatowaacha kwani ameziona jitihada zao za kuhubiri amani.

Rais Magufuli amesema kuwa, hivi sasa Wazanzibari wote wanahubiri amani kutokana na kurejesha umoja wao ambapo hapo siku za nyuma hata ndoa zipo zilizovunjika kutokana na itikadi za kisiasa.

“Mambo ya vyama yasitusumbue sana kwani Maalim Seif hata ukitaka kuja kuoa Chato, ruhusa njoo tu,”amesema Rais Magufuli huku akionesha furaha aliyonayo kwa kukutana na viongozi hao.

Aidha, Rais Magufuli ameeleza kuwa, mara nyingi maadui wasingependa kuona Zanzibar inakuwa moja na badala yake waangependa kuweko kwa machafuko, lakini viongozi wa Zanzibar wamechukua juhudi za makusudi kurejesha umoja hasa kwa vile viongozi wote wa Zanzibar hawana nia ya kuvunja Umoja wa Kitaifa walionao.

Amesema kuwa, Maalim Seif na Dkt.Mwinyi wamewafanyia mema Wazanzibari na kusisitiza kwamba hivi sasa Upemba na Uunguja utaondoka huku akiwataka viongozi hao kuendelea kuhubiri umoja.

Rais Maufuli amempongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa kupenda umoja hasa ikifahamika kwamba yeye anatoka Unguja, lakini Makamu wake wa Kwanza na Makamu wake wa Pili wote wanatoka Pemba hali ambayo inamaana kubwa katika uongozi na kumpongeza kwa kujenga upendo mkubwa.

Amewashukuru na kuwapongeza viongozi hao sambamba na kujadili mambo mengi zikiwemo changamoto zinazohusu maendeleo yakiwemo masuala ya ujumla ya kujenga Taifa, uimarishaji wa miradi mbalimbali ukiwemo ule wa Kigongo Musisi, ambao mapema Maalim Seif aliutembelea.

Katika hatua yake hiyo, Rais Magufuli ametoa shukurani kwa maadhimisho mazuri ya sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo yamesherehekewa kwa aina ya pekee na kupongeza viongozi hao kwa hatua hizo walizozichukua kwa kuhakikisha fedha zinatumika vizuri zaidi.

Amempongeza Maalim Seif Sharif Hamad kwa kukubali kuwa miongoni mwa viongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Rais Dkt.Hussein Mwinyi.

Rais Magufuli amesema kuwa, uzoefu wa Maalim Seif Sharif Hamad ni mkubwa na umajikita katika uongozi uliopo hivi sasa Zanzibar huku akimpongeza kwa maamuzi yake ambayo ni ya kishujaa ambayo yana maelewano ambayo ni maamuzi ya Mwenyezi Mungu.

Amesema kuwa, nchi nyingi duniani zinashindwa kuendelea kutokana na kutoelewana hivyo wananchi wa Tanzania na Zanzibar kwa jumla wanahitaja maendeleo na maelewano makubwa.

Rais Magufuli amempongeza Maalim Seif kwa kuacha matakwa yake ya kisiasa na kufuata matakwa ya Zanzibar.

Ameeleza jinsi anavyomfahamu Rais Dkt. Mwinyi kutokana na uchapa kazi wake mkubwa na kusema kuwa anaimani kubwa kwamba Zanzibar chini ya uogozi wa Dkt.Mwinyi itakuwa ya tofauti.

Ameongeza kuwa, Rais Dkt.Mwinyi ni jasiri, mchapa kazi na kusema kwa hatua yake ya mwanzo alioionesha katika kuiongoza Zanzibar ikiwa ni paoja na kushughulikia ufisadi kwa kuhakikisha kila senti ya Zanzibar inatumika kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar.

Rais Magufuli alimuhakikishia Maalim Seif kwamba yuko katika Serikali salama na kwamba yuko tayari hata kumualika akafungue mradi wowote huku akipongeza kura nyingi alizozipata Pemba na Unguja na kusema kuwa ataandaa ziara ya kutoa shukurani zake kwa ushindi waliompa.

Amesema kuwa, yuko pamoja na wananchi wa Zanzibar na viongozi wake na kumpongeza Rais Mwinyi kwa kuanza vizuri uonozi wake na kumtaka asiogope kutumbua majipu kwa wale wanaokwamisha miradi ya serikali na kumsisitiza aendelee.

Sambamba na hayo, Rais Magufuli amemtataka Maalim Seif kumsaidia Rais Dkt.Mwinyi katika kuhakikisha mali za wanyonge na Watanzania zinasimamiwa vizuri huku akieleza matumaini yake makubwa kwa Zazibar katika suala zima la uwekezaji.

Rais Magufuli amelipokea ombi la Dkt. Miwnyi la kuweka wanyama mbalimbali katika sehemu maalum kwa vile sheria zinaruhusu ili kusudi iwe kivutio cha watalii kwa upande wa Zanzibar. 

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa upande wake alitoa shukurani kwa Rais Magufuli kwa kufanyika kikao hicho kilichomshirikisha yeye pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Amesema kuwa, kikao hicho kilikuwa kizuri ambacho kilikuwa na madhumuni ya kuijenga Tanzania na kumshukuru Rais Mafuguli kwa utayari wake wa kufanya kazi na viongozi wa Zanzibar ambapo yeye na Maalim Seif wako pamoja katika kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Amempongeza Rais Magufuli kwa kuwa mstari wa mbele kwa kutaka Zanzibar iwe pamoja na akiwa Mwenyekiti wa CCM amekuwa akimuunga mkono katika suala zima la kuleta umoja.

Amesema kuwa, Wazanzibari wote wana muelekeo wa kuwa wamoja na tofauti zao za kisiasa wamezeweka pembeneni na hivi sasa wanaijenga nchi yao.

Ametoa shukurani kwa kukutana na Rais Magufuli na kupongeza na kumshukuru kwa maelezo yake ya kwamba yuko tayari kuijenga Zanzibar ambapo hivi karibuni alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Wang Yi ambapo alimpa ombi la ujenzi wa barabara za kilomita 148 wenye kutumia Dola milioni 73 za Marekani ambapo kwa fedha hizo barabara nyingi za Unguja na Pemba zitajengwa na kuzisifu juhudi zake hizo.

Rais Dkt.Mwinyi amemuhakikishia Rais Magufuli kwamba yeye na Maalim Seif wanafanya kila linalowezekana kuwa pamoja kwa lengo la kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar na kusema wao wataendeda na hatua hiyo ndani ya miaka mitano watapata maendeleo makubwa.

Amemshukuru Rais Magufuli kwa kutoa fursa hiyo ili kupanga mambo ya kusaidia kujijenga nchi na kumuahidi kwamba yeye na Maalim Seif wataendelea kuleta na kuudumisha Umoja wa Kitaifa na kuijenga Zanzibar kwa mustakabali wa wananchi wote.

Amewaeleza wananchi kwamba mazungumzo yao yametoa nguvu mpya na ari ya kuleta maendeleo makubwa na kumuomba Mwenyezi Mungu kuleta baraka zaidi katika mazungumzo hayo.

Mapema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alitoa shukurani kwa kufika Chato na kuonana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumshukuru kwa kuwakaribisha Chato ili kuiona sambamba na kupata fursa wa kutembelea mradi mkubwa wa mkakati wa Daraja la Magufuli walimtembeza na kumueleza na kueleza kuvutiwa kwake na mradi huo.

Amesema kuwa, mradi huo sio tu utaunganisha mikoa mbalimbali ya Tanzania pia, utaunganisha nchi za Afrika Mashariki na kati, hivyo alimpongeza kwa muono wake kwamba mradi huo ukimalizika utakuwa muhimu sana kwa Tanzania.

Maalim Seif amemshukuru Rais Magufuli kwa kukaa pamoja na kubadilishana mawazo juu ya Tanzania na juu ya mambo ambayo yanawaunganisha Watanzania na kushauriana namna bora zaidi ya kuweza kuwatumikia Watanzania.

Amesema kuwa, mazungumzo hayo yalikuwa mazuri ya kidugu ambayo yamempa matumiini kwamba Rais Magulfuli yuko pamoja na viongozi wenzake wa Zanzibar hasa kwa kuimarisha upendo na maelewano.

Mapema asubuhi Rais Dkt. Mwinyi ametua uwanja wa ndege wa Chato na kupokewa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na Serikali ambapo pia alipata fursa ya kuangalia ngoma za utamaduni.leza kuwa atawaunga mkono.

Aidha, amempongeza Rais Dkt.Mwinyi na kumsifu Rais Magufuli kwa kuwapa matumaini makubwa zaidi ya kuwafanya Wazanzibari kuwa wamoja zaidi.

Post a Comment

0 Comments