TANZANIA YANG’ARA TUZO YA VIVUTIO BORA VYA UTALII DUNIANI

Tanzania imepata mafaniko makubwa kwa kuwa na vivutio bora zaidi vya utalii duniani ambapo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, imepigiwa kura na kushinda kuwa mbuga bora zaidi ya hifadhi ya wanyamapori duniani, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Morogoro).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameyasema hayo mjini Morogoro katika maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani yaliyokwenda sambamba na mkutano wa wadau wa sekta ya utalii

Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Ndumbaro amesema Tanzania imeshinda tuzo hiyo na kuwa ya kwanza kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, huku Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Mlima Kilimanjaro zikiwa zimeshika nafasi za juu katika tuzo hizo ambazo hutolewa na taasisi ya Chief Traveler Award (CTA).

“Yalichaguliwa maeneo 25 yanayovutia zaidi kwa utalii kote duniani, katika hayo maeneo matatu yametoka Tanzania, ambapo eneo la kwanza lililopigiwa kura na kushinda kwa kuwa kivutio cha kwanza bora zaidi duniani ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, huku hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na Tarangire zikiwa ni miongozi mwa maeneo bora zaidi vivutio vya utalii,"amesema Dkt. Ndumbaro.

Dkt. Ndumbaro amesema kuwa mafaniko hayo hayakuja tu bali yametoka na mikakati ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi shupavu wa Rais John Magufuli, katika uwekezaji na usimamizi madhubuti wa hifadhi zetu za Taifa.

Dkt. Ndumbaro alitoa wito kwa watanzania, kujivunia mafanikio hayo huku wakifanya kila linalowezekana kuvitangaza vivutio hivyo vya utalii mahali pote duniani kwa lengo la kuzidi kukuza utalii na kuueleza ukweli Ulimwengu juu ya ubora wa vivutio vilivyopo nchini kwetu.

Katika hatua nyingine,Dkt. Ndumbaro, amesema kuwa kiwango cha ujangili kwa wanyamapori na mazao ya misitu kimepungua na kufika asilimia 90, ambapo aliwaonya watu wote wanaofanya shughuli za kibinadamu maeneo ya hifadhi, ikiwa ni kilimo au ufugaji, kuacha mara moja kwani serikali itakapowabaini itawachukulia hatua kali za kisheria.

“Sisi kama wizara tumejipanga, tukimkamata jangili halali yetu, ama zake ama zetu. Itakapohitajika kupiga ngumi, tutapiga ngumi, kupiga katafunua tutapiga katafunia, ili atakayeingia kwenye maeneo ya hifadhi na kutaka kuharibu ikolojia na uhifadhi ashughulikiwe kikamilifu na hatutakuwa na huruma na mtu yeyote,"amesema Dkt.Ndumbaro.

Naye Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya siku ya Wanyapori Duniani amesema kuwa, anazishukuru taasisi zote zilizo chini Wizara za Maliasili na Utalii, ikiwemo TAWA na TANAPA kwa ushirikiano mkubwa ambao wanawapatia hususani wakati ambao wanyamapori wanaingia kwenye makazi ya watu.

Loata amesema kuwa, mkoa wake utaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuhakikishakuwa misitu, wanyamapori, mabonde oevu na maeneo yote ya akiba na tengefu yanalindwa a kutuzwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news