Amnyonga mke na kumning'iniza jikoni, chanzo kuugua muda mrefu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Maria Kishiwa (57) mkazi wa Kitongoji cha Guluhuma Kijiji cha Isalalo Kata ya Utwigu Tarafa ya Puge wilayani Nzega mkoani Tabora amekutwa amekufa huku mwili wake ukiwa umening’inizwa kwenye nguzo ya jiko.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Tabora, ACP Safia Jongo amethibitisha kutokea mauaji hayo na kubainisha kuwa watu watatu wanashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo na uchunguzi unaendelea.

Amesema, tukio hilo lilitokea Agosti 3, mwaka huu majira ya saa nane usiku ambapo mwili wa marehemu ulikutwa umefungwa kamba shingoni huku umening’inizwa kwenye nguzo ya jiko.

Kamanda huyo amebainisha kuwa, chanzo cha mauaji hayo ni kuugua maradhi kwa muda mrefu ambapo mume wake akishirikiana na watoto wake wawili waliamua kumnyonga kwa kumfunga kamba shingoni na kumning’iniza ili ionekane kajinyonga mwenyewe.

Ameongeza kuwa, eneo aliloning’inizwa walikuta kinu na kigoda ili ionekane kuwa alipanda ili kutekeleza kitendo hicho wakati ni vigumu kwa mtu kupanda hadi kuwe na msaada wa watu wengine na jambo ambalo lilileta mashaka.

Kamanda Safia amesema kuwa, marehemu alikuwa analala na mtoto wake na walipomhoji mtoto huyo alithibitisha kuwa baba alikuja usiku na watoto wake wa kiume na kumfunga kamba kabla ya kumnyonga.

Ameongeza kuwa, baada ya mwili huo kufanyiwa uchunguzi wa kina na daktari ilibainika kuwa amekufa kwa kunyongwa na watuhumiwa watatu waliokamatwa walikiri kuhusika na mauaji hayo kwa sababu ya kuugua kwa muda mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news