Yanga SC, Dodoma Jiji FC zatamba kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Fiston Kalala Mayele na Jesus Ducapel Moloko wameipa Yanga SC ushindi wa 2-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Ni katika mtanange wa aina yake ambao umepigwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Vijana hao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo dakika ya 36 alianza Mayele kuzichakaza nyavu za Azam FC baada ya kumalizia kazi nzuri ya beki mzawa, Kibwana Shomari.

Kwa upande wake Moloko alitumia kipindi cha pili ndani ya dakika ya 73 kufanya mashambulizi akimalizia pasi ya mshambuliaji Mburkinabe, Yacouba Sogne.

Yanga SC kwa ushindi huu inafikisha alama 12 baada ya kucheza mechi nne na kuendelea kuongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa alama mbili zaidi ya Dodoma Jiji FC ambayo pia imecheza mechi moja zaidi.
Vijana wa Dodoma Jiji walianza kuharibu mipango ya wakata miwa, Mtibwa Sugar baada ya kuwachapa 1-0 katika michuano hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Seif Abdallah Karihe ndiye aliyewainua vijana hao wa makao makuu ya nchi katika dakika ya 61 kwa kupachika bao safi katika dimba la Uhuru lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Jana Meshack Abraham ndani ya dakika ya 16 ameipa Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, KMC katika dimba la Uhuru lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Mtanange mwingine wa Ligi Kuu, Mbeya Kwanza imelazimishwa sare ya 1-1 na Biashara United jana katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Ramadhani Suleiman Chombo (Redondo) alianza kuifungia Biashara United dakika ya 13, kabla ya mshambuliaji Hamisi Kanduru kuisawazishia Mbeya Kwanza dakika ya 81.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news