Mheshimiwa Othman asisitiza kutekeleza dhamira aliyokuwa nayo Hayati Maalim Seif

NA MWANDISHI MAALUM

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameeleza dhima aliyonayo katika kuutumikia umma wa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, ili kutekeleza azma ya kuyafikia matarajio yao makubwa ya kujikwamua kimaisha na kujiletea maendeleo.
Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo Novemba 21,2021 huko Kojani Mjini wakati akiongea na Wazee, Wanachama, Wafuasi wa ACT-Wazalendo na wakazi wa kisiwa hicho, katika ziara yake Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema, anaelewa tofauti iliyopo kati yake na mtangulizi wa nafasi hiyo, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad, bali atahakikisha anatekeleza dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wote wa Visiwa vya Unguja na Pemba na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiongelea juu ya upekee wa Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, Mheshimiwa Othman ametaja kipaji katika kutetea haki, vita dhidi ya dhuluma na uzalendo wa kweli, na kwamba atakuwa tayari kuyaendeleza hayo kwa ajili ya maslahi ya wananchi wote.

Mheshimiwa Othman amesisitiza umuhimu wa amani, utulivu, umoja na mshikamano katika jamii ili kuandaa mazingira bora yatakayotoa fursa kwa Serikali kutekeleza mipango yake kwa ufanisi na hatimaye wananchi kupata maendeleo.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar ambaye pia ni Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto hapa visiwani, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui amesema Serikali inao wajibu wa kukabiliana na kero za wananchi, huku akiahidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto thakili za kisiwa hicho, zikiwemo upungufu wa huduma za matibabu na ukosefu wa madaktari.

Nao Wazee wa Kojani ambao wamemkabidhi rasmi Mheshimiwa Othman kisiwa hicho, wameeleza matumaini waliyonayo na kwamba wamempokea kiongozi huyo kwa moyo wote, wakitaraji utekelezaji wa dhamira na heshima ya dhati kwao kama ilivyokuwa kwa Maalim Seif zama za uhai wake.

Wakibainisha changamoto zinazowakabili, Mzee Faki Mwinyimkuu Hassan, Bakari Juma Maua, Mjaka Hamad Mjaka na Bi Shine Mfaki, wametaka kuelewa hatua za utekelezaji wa dhati wa makubaliano kati ya Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dokta Hussein Ali Mwinyi, katika kufanikisha maridhiano ya kweli ya kisiasa hapa visiwani.

Katika ziara yake ya kwanza kisiwani humo iliyopokelewa kwa mapokezi makubwa na Wakaazi wa Kojani, vikundi vya burudani na kuwakagua wagonjwa, Mheshimiwa Othman aliongozana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, Katibu wa Oganaizesheni wa ACT-Wazalendo Ndugu Omar Ali Shehe, Wajumbe wa Kamati kuu, Wawakilishi, Wabunge, na viongozi mbali mbali wa chama hicho.

Wakati huo huo Mhe.Othman alishiriki katika shughuli ya maziko ya Bwana Ali Kombo Hassan, ambayo yalifanyika jioni katika kijiji cha Kambini Mchanga mdogo, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Post a Comment

0 Comments