Watumishi wampongeza Waziri Jenista Mhagama kwa kuunda Timu ya Wataalam itakayopendekeza mfumo mpya wa kupima utendaji kazi wao

NA JAMES K.MWANAMYOTO

WATUMISHI wa Umma mkoani Mwanza wamempongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kwa hatua yake ya kuunda kikosi kazi maalum cha wataalam wabobezi kinachofanya mapitio na kuainisha mapungufu yote ambayo yamejitokeza kwenye Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji Kazi wa watumishi (OPRAS), kwa lengo la kupendekeza mfumo mpya wa kielektroniki wa wazi na rafiki ambao utatumika kupima utendaji kazi wao bila kuwepo upendeleo au udanganyifu wa aina yoyote.
Afisa Serikali za Mitaa Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Fabian Gapchojiga akizungumzia uamuzi wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuunda kikosi kazi maalum cha wataalam wabobezi kwa ajili ya kuainisha mapungufu yalijitokeza kwenye Mfumo wa OPRAS na kupendekeza mfumo mpya utakaotumika kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma.(Picha na OR-UTUMISHI).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Mwanza, wakati wa mahojiano maalum na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Ofisi ya Rais-UTUMISHI, watumishi hao wamesema hatua hiyo ya haraka ya Mhe. Jenista Mhagama kuunda kikao kazi hicho ili kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imeleta faraja kubwa miongoni mwao kwani itaondoa changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo wakati wa kupimwa utendaji kazi wao kupitia mfumo wa OPRAS.

Afisa Utumishi Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bi. Francisca Mmari amesema kuwa, hatua ya Mhe. Jenista kuunda timu hiyo itakuwa ni msaada mkubwa kwa Watumishi wa Umma kutambua kwamba Mfumo wa Upimaji wa Utendaji kazi haupo kwa ajili ya kuwapandisha vyeo tu bali upo kwa ajili ya kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Serikali na Taasisi zake kupitia mipango mikakati yanafikiwa kwa wakati.

Bi. Francisca Mmari ameongeza kuwa, Watumishi wa Umma wanatarajia mfumo huo mpya utakaopendekezwa na timu iliyoundwa na Mhe. Jenista Mhagama utamfanya mtumishi awe na imani nao na kumuwezesha kutambua wajibu wake ikiwa ni pamoja na kutambua ulazima wa kupimwa na mfumo huo.

Kwa upande wake, Afisa Serikali za Mitaa Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Fabian Gapchojiga amesema mfumo wa OPRAS ulikuwa hauleweki vizuri na Watumishi wa Umma, hivyo uamuzi wa Mhe. Jenista Mhagama kuunda timu ya kuupitia ana imani kuwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika mfumo huo hayatajitokeza tena katika mfumo mpya utakaopendekezwa kupima utendazi kazi wa Watumishi wa Umma.

“Mfumo wa OPRAS wa sasa una mapungufu ambayo hayampi Mtumishi wa Umma furaha ya kujaza fomu za OPRAS ili apimwe utendaji kazi wake hivyo ujio wa mfumo mpya utaondoa mapungufu yaliyojitokeza na utajenga imani na furaha ya watumishi kupimwa utendaji kazi wao,” Bw. Gapchojiga amefafanua.

Sanjari na hilo, Bw. Gapchojiga amesema kuwa kupitia timu hiyo iliyoundwa, watumishi ambao ndio wadau wakuu wanaolengwa na Mfumo wa Kupima Utendaji kazi utakaopendekezwa watapata fursa ya kutoa maoni yatakayoiwezesha Serikali kupata mfumo mzuri na imara wa kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma.

Naye, Afisa Sheria Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bi. Savela Kalinda amepongeza uamuzi wa Mhe. Jenista Mhagama kuunda timu ya kuupitia mfumo wa OPRAS uliopo akiamini kuwa, ni muda sahihi na muafaka kuupitia mfumo huo kwasababu umekuwa si rafiki kwa Watumishi wa Umma kutokana na mapungufu yaliyojitokeza kwenye mfumo huo.

Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma (OPRAS) ulianza kutumika rasmi na Serikali kwa ajili ya kupima utendaji kazi wa Mtumishi wa Umma mmoja mmoja mwaka 2004.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news