DCEA yamdaka nesi msaidizi akiwa na kilo 174.77 za heroine juu ya kitanda Tabata Relini

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA),Gerald Musabila Kusaya amesema, mamlaka hiyo imemkamata nesi msaidizi, Bw.Salum Shabani Mpangula mkazi wa Tabata Relini katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam akiwa na kilo 174.77 za Dawa za Kulevya aina ya Heroine.
Ameyasema hayo leo Juni 3,2022 wakati akitoa taarifa kuhusu mambo mbalimbali yaliyofanywa na mamlaka hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Mei, 2022.

Amesema kuwa, mtuhumiwa alikamatiwa nyumbani kwake eneo la Tabata Relini lililopo Halamshauri ya Wilaya ya Ilala jiini Dar es Salaam.

"Mei 12, 2022 katika eneo la Tabata Relini Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilikamata kilogramu 174.77 za dawa za kulevya aina ya heroine.

"Katika tukio hilo Salum Shabani Mpangula mwenye umri wa miaka 54,mkazi wa Relini Tabata ambaye ni nesi msaidizi Kariakoo Dispensary amekamatwa kwa kusafirisha dawa hizo,"amesema Kamishna Jenerali Kusaya.

Amefafana kuwa,mtuhumiwa alikamatwa kufuatia upekuzi uliofanywa nyumbani kwake. "Pakiti 162 zenye unga uliodhaniwa kuwa dawa za kulevya zilikutwa ndani ya viroba sita vilivyokuwa vimehifadhiwa chumbani kwa mtuhumiwa, na pakiti moja ya unga huo ilikuwa imewekwa kwenye mfuko mweusi wa nailoni na kufichwa chini ya kitanda,"amesema.

Kamishna Jenerali Kusaya amesema kuwa, taarifa za uchunguzi wa kitaalam kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali zimethibitisha kuwa pakiti zote 163 zilikuwa na dawa za kulevya aina ya heroine ambazo jumla yake ni kilogramu 174.77 na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu za kisheria kukamilika,"amesema.

Post a Comment

0 Comments