KIKAO CHA KWANZA CHA MAHAKAMA TATU ZA AFRIKA KUFANYIKA ZANZIBAR TAREHE 27-29 JUNI 2022

NA DIRAMAKINI

KIKAO cha kwanza kinachojumuisha mahakama tatu za Afrika, ambazo ni Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ) Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Magharibi (ECOWAS CCJ) kitafanyika Zanzibar, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzia tarehe 27 hadi 29 Juni 2022. 

Mazungumzo hayo ya siku tatu yatajadili, miongoni mwa mengine, mbinu bora za kuimarisha ushirikiano wa kimahakama na utetezi wa haki za binadamu ndani ya bara la Afrika, na utaratibu bora wa utekelezaji wa maamuzi ya mahakama hizo.

Mazungumzo hayo yatakayojumuisha Majaji wapatao 30 na mawakili zaidi ya 50 kutoka mahakama hizo tatu za bara na kikanda, yatafunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye atahutubia kikao hicho.
‘’Mazungumzo haya yatatoa fursa za kubadilishana maarifa na namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazofanana,’’ amesema Rais wa Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu, Mhe. Jaji Imani Daud Aboud.

Naye Rais wa EACJ Mhe Jaji Nestor Kayobera amesema kuwa, “Mazungumzo hayo yatatoa jukwaa la kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama hizo tatu na wadau wengine muhimu, kupitia kubadilishana mawazo juu ya mambo mbalimbali ya msingi yenye maslahi ya pamoja, ikiwa ni pamoja na kanuni bora na taratibu za kukabiliana na masuala yanayojitokeza wakati mahakama hizo zinatekeleza majukumu yao.” 

Rais wa ECOWAS CCJ, Jaji Edward Amoako Asante alikaribisha mazungumzo kama “fursa ya kihistoria ya kujenga msingi wa ushirikiano wa kudumu kati ya mahakama hizo na wadau katika kuimarisha ufanisi zaidi wa mahakama hizo katika kutekeleza majukumu yao, hasa katika kuzifanya nchi za Afria kuwajibika katika kutekeleza maamuzi ya mahakama hizo.” 

Kikao hiki kinafanyika kwa masaada wa Taasisi ya Haki za Binadamu ya Raoul Wallenberg kupitia msaada wa Shirika la Maendeleo la Sweeden, na kwa ushirikiano wa Konrad Stiftung, GIZ na Ofisi ya Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu.

Post a Comment

0 Comments