Serikali yawataka wananchi kutumia fursa Mkalama

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa Kata za Iguguno, Ntonda, Kiyangire na Wilaya ya Mkalama kutumia fursa ya daraja la Msingi lililopo Lukomo na barabara zilizojengwa na TARURA kusafirisha mazao na biashara zao ili kuendelea kujikwamua kiuchumi.
Kauli hiyo ameitoa wilayani Mkalama wakati akikagua ujenzi wa daraja la Lukomo barabara ya Iguguno-Kikhonda-Kinampanda lenye urefu wa mita 30 ambalo limekamilika kwa asilimia 100 mapema ambapo amewataka wananchi kulitumia kama fursa ya kiuchumi kwani linaunganisha Kata za Wilaya hiyo na mkoa wa Simiyu.

“Andaeni biashara zenu, tumieni fursa ya daraja na barabara zilizojengwa kupitisha biashara zenu, ubora wa daraja hili ni ubora wa kudumu, niwapongeze sana Wahandisi wa TARURA mkoa wa Singida, huu ni ubunifu wa kujenga daraja kwa shilingi milioni 550 badala ya shilingi Bilioni moja iliyotakiwa itumike,”alisema Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali itafanya kazi usiku na mchana kuwatumikia wananchi ili kuhakikisha inafikia malengo.

Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa daraja hilo Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Tembo David amesema daraja hilo limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 550 na litakuwa na uwezo wa kupitisha magari ya mizigo yaliyobeba mpaka tani elfu 40 na litasaidia kuokoa maisha ya watu yaliyokuwa yakipotea karibu kila mwaka kwa takribani miaka 40.

“Daraja hili limejengwa kwa kutumia mawe na nondo na limetumia muda mfupi kukamilika, kutoa ajirra kwa maeneo huisika, kukamilika kwa ujenzi huu wa daraja kutaondoa changamoto ya mawasiliano iliyokuwepo hasa kipindi cha masika, aidha kutaimarisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Kata za Iguguno, Kikhonda na Kiyangire,”alisema.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (AFYA) Mhe. Dkt. Festo Dugange amesema kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI imekubaliana na Mameneja wa TARURA kuwa wabunifu na kuhakikisha barabara wanazosimamia zinapitika kwa kipindi cha mwaka mzima. Ameishukuru Serikali kuongeza bajeti ya barabara kupitia Wakala wa Barabara TARURA kutoka shilingi Bilioni sita hadi shilingi Bilioni 23.4 kwa mwaka mkoani Singida sawa na ongezeko la asilimia 389 na shilingi milioni 600 hadi shilingi Bilioni 2.2 kwa Halmashauri ya Mkalama.

Kwa upande wake Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Isack Mtinga amesema Serikali imefanya jambo kubwa kujenga daraja la Lukomo na lakini ameiomba Serikali kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Lukomo ili ianze kutoa huduma.

Naye Mzee Omari Ngaa mwenyeji wa eneo la Lukomo - Iguguno amesema tangu akiwa kijana mdogo eneo hilo huwa mto mkubwa kipindi cha masika na kipindi cha kiangazi haukauki na kabla ya daraja halijajengwa watu zaidi ya 15 walipoteza maisha. “daraja hili ni zuri sana, ninaishukuru sana Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan mimi toka nikiwa mdogo nimeshuhudia watu zaidi ya 15 wakichukuliwa na maji na kufa, daraja hili litatusaidia usafiri kwani mwanzo usafiri ulikuwa wa tabu sana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news