Soko la bima Tanzania lazidi kustawi kwa kasi, TIRA yatoa leseni tatu kidijitali

NA DIRAMAKINI

SOKO la bima nchini Tanzania limeendelea kustawi kwa kasi kutokana na wadau wengi kuvutiwa kuwekeza ili kuwafikishia wananchi huduma kwa njia mbalimbali mijini na vijijini ikiwemo kupitia mfumo wa kidijitali.
Hayo yamethibitika leo Julai 9, 2022 baada ya Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Tanzania (TIRA), Dkt.Baghayo Saqware kukabidhi leseni kwa kampuni tatu ambazo zimekidhi vigezo vya kutoa huduma za bima kidijitali nchini.
Dkt.Saqware akizungumza katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam amesema, kampuni zilizokabidhiwa leseni leo ni Voda Bima, Imatic Tehnologies na Axieva Bima.

Amesema, makampuni hayo yamekabidhiwa leseni hizo kufuatia kusajiliwa na mamlaka na kukidhi vigezo vinavyotakiwa katika utoaji wa huduma hizo. 
"Kampuni hizo zimesajiliwa na mamlaka wamekuja hapa Sabasaba wamejaza fomu zetu na tumefanya assessment ndani ya siku saba, tumejiridhisha na tunawapa leseni. Kampuni hizo ni Axieva Bima, ambayo itapewa leseni ya kusambaza bima kupitia mitandao Digital Platforms,"amesema Saqware.

"Kampuni ya pili ni Imatic Tehnologies ambayo pia imepewa leseni ya kusambaza bima kupitia mtandao na kampuni ya tatu ni Voda bima ya VodaCom Tanzania nao wamepewa leseni ya kusambaza bima kupitia mtandao,"amesema Dkt.Saqware na kuongeza kuwa,
"Tunawahimiza Watanzania na makampuni ya bima watumie kampuni hizi ambazo zimepata leseni na kampuni zingine ambazo wanazitumia katika kusambaza bima zao, tunawashauri kwa mujibu wa mwongozo wetu ambao tumeutoa mwezi wa tano mwaka huu wa 2022. Wanatakiwa waje wasajili kampuni hizo, taasisi hizo, ambazo zinatoa huduma za kidigital kwenye taasisi zote za bima ambazo zimesajiliwa Tanzania," amesema Kamishna Dkt.Saqware.

Post a Comment

0 Comments