Mkataba wa Simba, M Bet watajwa kuvunja rekodi, Mo Dewji apongezwa kupaisha chapa

NA DIRAMAKINI

KWA mara ya kwanza, Klabu ya Simba yenye maskani yake Msimbazi jijini Dar es Salaam imeingia mkataba wa udhamini wa shilingi Bilioni 26.1 ambao unatajwa kuvunja rekodi ndani na nje ya Tanzania.
Udhamini mpya wa Simba kupitia M Bet unatajwa kuwa moja wapo ya hamasa na kichocheo cha kukuwa kwa soka la Tanzania, huku pongezi nyingi zikipelekwa kwa mwekezaji Mo Dewji ambaye kwa kiwango kikubwa amefanikiwa kupaisha chapa ya Simba na kuwa na mvuto zaidi.

Akizungumza leo Agosti 1, 2022 wakati wa hafla ya kuutambulisha rasmi udhamini huo, Mkurugenzi wa Masoko wa M-Bet, Allen Mushi amesema, wana imani kubwa kuhusu ushirikiano huo.

"Tunaamini kama M-Bet tukishirikiana na Simba tutajitangaza ndani na nje ya Tanzania,"amesema Bw.Mushi wakati akizungumzia kuhusu hatua hiyo leo jijini Dar es Salaam.

Akitoa mchanganuo wa udhamini huo, Mushi amesema kwamba mwaka wa kwanza Simba watapata shilingi Bilioni 4.670, mwaka wa pili shilingi Bilioni 4.925, mwaka wa tatu shilingi Bilioni 5.205, mwaka wa nne shilingi Bilioni 5.514 na mwaka wa tano shilingi Bilioni 5.853.

"M-Bet ni kampuni namba moja ya michezo ya kubashiriki sasa tunashirikiana na klabu namba moja Tanzania,” amesema Mushi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salum Abdallah Muhene (Try Again) amesema, wanathamini na kuheshimu sana juhudi za wadhamini wote, kwani dhamira yao ni moja ya kuhakikisha wanalifanya soka la Tanzania kusonga mbele.

“Sisi Simba ni waungwana, tunawashukuru wadhamini waliopita, sasa tuko na mdhamini mpya na tunaamini tutafanya kazi kwa karibu.Tunakaribisha makampuni mengine kufanya nayo kazi sababu hii ni klabu ya watu, wasiogope tuko tayari kufanya nao kazi.

"M-Bet mlichotaka mtakipata. Pesa ni nyingi hizi, tumieni hii nafasi kutanua biashara yenu kupitia mashabiki wetu.Mimi sijawahi kuona Simba Day kama hii, imeandaliwa ikaandalika, naona kama siku haifiki. Tuje kwa wingi siku hiyo,"amesema Muhene.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba,Barbara Gonzale amesema kuwa leo ni siku kubwa kwa Simba na kampuni ya kubashiri ya M-Bet ambao ni wadhamini wao wakuu walioweka mezani fedha nyingi kwa muda wa miaka mitano.

”Leo ni siku kubwa kwa Simba na M-Bet. Swali kubwa ni kwanini M-Bet. Sababu kubwa ni wameweza kukidhi mahitaji yetu. Kwa ukubwa wa Simba ni lazima kujihusisha na kampuni ambayo inaongoza kwenye biashara ambayo wanafanya. Mkiangalia takwimu M-Bet wanaongoza kwa ukubwa Tanzania.

“Washirika wote wa Simba kwa sasa wamejitoa kwa Simba tu.Hii ni mara ya kwanza mdhamini mkubwa anakuwa na senior team pekee, huko nyuma mdhamini mkuu alikuwa kwa timu zote lakini sasa timu zingine tunaweza kuzitafutia mdhamini wake,"amesema Gonzale.

Kwa nyakati tofauti,baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo wameeleza kuwa, mafanikio yote yanatokana na uwekezaji wa Mo Dewji ambaye licha ya changamoto mbalimbali anazokumbana nazo ameendelea kuwa mvumilivu na kuijenga klabu hiyo kitaaluma zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news