Prof.Muhongo afikisha elimu ya Sensa kila kitongoji huku akifanya tathmini ya miradi ya maendeleo Musoma Vijijini

NA FRESHA KINASA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Prof.Sospeter Muhongo ameendelea na Kampeni ya Sensa ya Watu na Makazi jimboni humo sambamba na kufanya tathmini ya maendeleo yaliyopatikana ndani ya miaka kumi 10 yaani 2012-2022.
Huku akisisitiza kwamba wananchi watambue umuhimu wa Sensa, kwani takwimu za watu na makazi kwenye kata, vijiji na vitongoji husika zina manufaa makubwa katika kuiwezesha Serikali kuwaletea maendeleo, hivyo ushiriki wao katika Sensa ya Watu na makazi Agosti 23, 2022 ni nyenzo muhimu sana ya maendeleo yao thabiti.

Aidha, Prof.Muhongo mbali na kutumia kampeni ya hamasa na utoaji wa elimu kwa wananchi washiriki kuhesabiwa, pia amekuwa mstari wa mbele katika kufanya tathmini ya maendeleo ndani ya jimbo hilo katika kuhakikisha miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali inazidi kuimarika kwa manufaa ya wananchi jimboni humo.

Kufuatia juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini kuwezesha maendeleo ya wananchi. Kata pekee ya Ifulifu iliyokuwa haina sekondari imeweza kupata sekondari. Ambapo wananchi wa kata hiyo wametoa shukrani zao za dhati kwa Rais Samia na Mheshimiwa Muhongo kufanikisha Sekondari katika kata hiyo.

"Kata ya Ifulifu ilikuwa Kata pekee ndani ya Jimbo letu isiyokuwa na Sekondari yake. Kwa sasa Kata hiyo inazo mbili zitakazofunguliwa Januari 2023.Ifulifu Sekondari, imejengwa Kijijini Kabegi kwa mchango mkubwa wa Serikali yetu iliyochangia Milioni 470 na bado itaendelea kuchangia. Shukrani nyingi sana kwa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan,"imeeleza sehemu ya taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini kama ilivyoonwa na DIRAMAKINI.

Wanavijiji na viongozi wao, akiwemo Mbunge wa Jimbo, nao wamechangia ujenzi wa Sekondari hiyo ya kisasa na yenye maabara 4 physikia, chemia, biologia na jographia.
Pia, Nyasaungu Sekondari, hii inajengwa Kijijini Nyasaungu kwa nguvu kazi na michango ya fedha taslimu za Wanakijiji wa Nyasaungu, Viongozi wao akiwemo Mbunge wa Jimbo Mheshimiwa Prof. Muhongo, Mfuko wa Jimbo nao unachangia ujenzi huo ambayo pia itafunguliwa Januari 2023.

Aidha, taarifa hiyo pia imeeleza kuwa, "Wakati tunamalizia kiu ya kuwepo kwa Sekondari 1 hadi 2 kwa kila Kata, tunazo Kata 21 kifuatacho ni ujenzi wa 'High Schools' za masomo ya Sayansi Jimboni mwetu kazi hii imeanza."

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo amesema Shule hiyo ya Sekondari Ifulifu iliyojengwa Kijiji cha Kabegi ni nzuri sana, na pia akawahimiza Wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa ajili ya maendeleo.

Charles Chota ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kabegi ambapo ameishukuru Serikali na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini kwa kufanikisha ujenzi wa Shule hiyo na kwamba itawasaidia wanafunzi kusoma karibu na kuondokana na Changamoto ya kutembelea umbali mrefu kwenda Nyakatende kusoma.
"Watoto wangu walikuwa wanatembea kutoka Nyasurura mpaka Nyakatende walikuwa wakiondoka saa 12:00 asubuhi na kurudi jioni wakiwa njaa na wamechoka. Kwa Sasa wataondokana na changamoto hii na hivyo watasoma kwa ufanisi na pia kuondokana na mimba na vishawishi vingi walivyokuwa wakivipata shukrani kwa Rais Samia na Mbunge kutujengea Sekondari hii,"amesema mmoja wa wananchi katika mazungumzo na DIRAMAKINI.

"Tunamshukuru sana Mheshimiwa Muhongo Mbunge wetu, amekuwa pamoja nasi wakati wote, linapokuja Jambo linalohusu maendeleo yuko mstari wa kwanza kuchangia na kutoa hamasa kwa Wananchi ili kushiriki kwa ufanisi. Tumeona kwenye Sensa alivyohamasisha kijiji kwa Kijiji na katika mambo mengine ya Maendeleo amekuwa akifanya kwa moyo wa dhati kabisa iwe ujenzi wa Shule, Zahanati, Vituo vya afya na mambo ya Kijamii tuko naye wakati wote, pia Pongezi kwa Rais Samia Hassan kuzidi kutoa fedha nyingi ambazo zinatekeleza miradi ya maendeleo jimboni mwetu Mungu azidi kumpa afya njema,"amesema Aneth Peter.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news