SUBIRI MHESABIWE:Mipango ipangiliwe Na bajeti mpatiwe, Mwishowe tufanikiwe

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

"Niwaase Watanzania wote, tushiriki kwa ufanisi,Sensa ya mwaka huu itakuwa ya sita kufanyika baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana. 
 
"Hakuna sababu ya mtu kuzuia watu wasihesabiwe, bali tuhimize watu wahesabiwe. Sensa hata nyumba za ibada zinafanyika, mfano wachungaji wanahesabu idadi ya mahudhurio ya washirika, vivyo hivyo kila mzazi anafahamu idadi ya familia na mali zake ili aweze kutoa huduma bora na kwa ufanisi, zoezi hili lifanyike vizuri sana bila kukwamishwa.

"Sensa ina faida kubwa sana kwa nchi, Serikali itatambua hali za maendeleo ya wananchi, hali ya ajira, hali ya utoaji wa huduma za jamii, kupata takwimu sahihi na mambo mengine mengi ya muhimu kila kitu cha thamani kinahesabiwa na ndio maana fedha zinahesabiwa sembuse na binadamu ambaye thamani yake ni kubwa kuliko chochote.
"Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.

"Hivyo Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012. 
 
Huo ni mwongozo wa mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande (KiMPAB) wakati akikupa nafasi ya kuandaa mahali pa kuketi ili aweze kukushirikisha yaliyo mema kutokana na zoezi muhimu la sensa ambalo linafanyika baada ya siku mbili zijazo nchini kote, karibu;

1. Subiri mhesabiwe,
Idadi tuielewe,
Mipango ipangiliwe,
Na bajeti mpatiwe,
Wala msipungukiwe,
Kasma mbaguliwe,
Na miradi ichelewe,
Agosti shina tatu.

2. Ya Rais yasikiwe,
Vizuri yaangaliwe,
Tena atekelezewe,
Na sisi tuhesabiwe,
Takwimu zichukuliwe,
Hizo kazi zifanyiwe,
Na sote tufanikiwe,
Agosti shina tatu.

3. Ratiba ziandaliwe,
Tarehe ziheshimiwe,
Sensa muda ipangiwe,
Na nafasi itengewe.
Ya kwetu tusizidiwe,
Na wala tusipitiwe,
Sote na tuhesabiwe,
Agosti shina tatu.

4. Kazi zetu zifanyiwe,
Na karani tufikiwe,
Sote na tuhesabiwe,
Mtu sisahauliwe,
Wa nyumbani waambiwe,
Umuhimu waujuwe,
Na huo ufagiliwe,
Agosti shina tatu.

5. Wagonjwa wahesabiwe,
Na wazima wapitiwe,
Mtu asibaguliwe,
Alivyo ahesabiwe,
Idadi tuielewe,
Kwa mipango itumiwe,
Na nchi ifanikiwe,
Agosti shina tatu.

6. Kampeni na zisikiwe,
Kutaka tuhesabiwe,
Wasojua waambiwe,
Na wao waandaliwe,
Na sote tuhesabiwe,
Majanga tuepushiwe,
Kwa afya tubarikiwe,
Agosti shina tatu.

7. Mume mke aambiwe,
Muhimu ahesabiwe,
Tarehe asichelewe,
Maswali ayaelewe,
Na vizuri yajibiwe,
Ukweli tuuelewe,
Mwishowe tufanikiwe,
Agosti shina tatu.

8. Idadi tutambuliwe,
Takwimu zichambuliwe,
Vizuri tuhudumiwe,
Mipango ipangiliwe,
Tuendako tuelewe,
Mtu asisingiziwe,
Uchumi tuinuliwe,
Agosti shina tatu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news