DC Mkasaba awapongeza washiriki michezo mbalimbali Tamasha la Kizimkazi mwaka huu

NA DIRAMAKINI

WASHINDI wa michezo mbalimbali ya Tamasha la Kizimkazi wamepongezwa kwa ushiriki wao, hatua ambayo imeonesha jinsi wanavyoendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mwasisi na mlezi wa tamasha hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Mheshimiwa Rajab Yussuf Mkasaba ameyasema hayo mara baada ya kukabidhi zawadi kwa washindi mbalimbali wa michezo iliyofanyika katika Tamasha la Kizimkazi hivi karibuni, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Sheha wa Shehia ya Kizimkazi Dimbani.

Katika maelezo yake, Mkuu huyo wa wilaya aliwapongeza wanamichezo hao kwa ushiriki wao huo na kuwasisitiza kuendelea kushiriki katika michezo hiyo hapo mwakani kwa azma ya kuendelea kumuunga mkono muasisi na mlezi wa tamasdha hilo, Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa, kuwepo kwa michezo hiyo kumeongeza ladha ya tamasha hilo, kwani wana michezo na wananchi wa wilaya hiyo wameweza kushiriki vyema pamoja na kuendelea kujenga umoja, mshikamano na udugu walio nao kupitia mashindano hayo.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya alieleza umuhimu wa michezo huku akiwataka washindi kuendelea kushika nafasi zao na wale walioshindwa kujitahidi hapo mwakani ili na wao wawe washindi na hatimaye wapate zawadi nono.

Pamoja na hayo, Mheshimiwa Mkasaba alitumia fursa hiyo kuwapongeza wanamichezo wote walioshiriki katika michezo ya tamasha hilo ambapo kilele chake kilifanyika Septemba 3, mwaka huu huko Kizimkazi Dimbani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan alikuwa ndiye mgeni rasmi.

Mkasaba pia alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulilea tamasha hilo pamoja na kuungana na wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwazindulia miradi yao sita ya maendeleo kwa siku moja siku ya Septemba 2, 2022 ikiwa ni siku moja kabla ya kilele cha tamasha hilo.

Pia, alitumia fursa hiyo kuipongeza Benki ya CRDB kwa kudhamini mashindano hayo pamoja na kuipongeza Kamati ya Tamasha la Kizimkazi kwa kuratibu vyema shughuli hizo huku akiwapongeza viongozi na wananchi waliohudhuria katika tamasha hilo linalofanyika kila mwaka katika wilaya hiyo.

Miongoni mwa michezo iliyoshindaniwa katika tamasha hilo la Kizimkazi ni mpira wa miguu, mpira wa pete, nage, ngalawa, kuvuta kamba, baskeli, bao la kete, karata, chanis, karata wahedi wa60, drafti, kufua na kukuna nazi, kusokota kamba pamoja na mashindano ya michezo mitano kwa wanafunzi wa skuli za maandalizi.
Sambamba na hayo pia, Mkuu wa wilaya hiyo alitoa zawadi kwa washindi wa mashindano ya “General knowledge kidato cha Pili” ambayo yaliwashirikisha wanafunzi kutoka skuli ya Sekondari Hasnu Makame, Skuli ya Sekondari Kizimkazi Dimbani na Skuli ya Sekondari Kizimkazi Mkunguni. Pia alitoa zawadi kwa washindi wa mashindano ya kuhifadhi Quran.

Mashindano yote hayo yaliwashirikisha wanaume na wanawake ambapo zawadi za fedha taslimu zilitolewa kwa washindi pamoja na washiriki wote ambapo kiasi cha shilingi milioni 26,780,000 zilitolewa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news