Rais Dkt.Mwinyi ateta na taasisi ya Kimataifa ya kidemokrasia

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amekutana na Uongozi wa Taasisi ya Kidemokrasia inayoshughulikia masuala ya Kimataifa (NDI), ukiongozwa na Mkurugenzi wa taasisi hiyo nchini, Sandy Quimbaya, ambapo ulifika Ikulu kujitambulisha na kuelezea shughuli inazofanya.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Kidemokrasia Inayoshughulikia Masuala ya Kimataifa (NDI), Bi. Sandy Quimbaya, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo. (Picha na Ikulu).

Akizungumza na ujumbe huo pamoja na mambo mengine, Dkt. Mwinyi aliipongeza taasisi hiyo kwa kazi nzuri inayofanya kwa kushirikiana na asasi za kiraia hapa nchini.

Akigusia dhana ya NDI juu ya uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU), Dkt. Mwinyi alisema ni eneo muhimu kwa msingi kuwa Serikali hiyo unaimarisha umoja wa Taifa na wananchi wake, pamoja na kudumisha amani, ikiwa ni hatua muhimu kufikia maendeleo ya kiuchumi.

Alisema kupitia Asasi za Kiraia NDI imefanya kazi nzuri ya kuwafikia wananchi na hatimaye kupendekeza nini kifanyike ili kuwa na Serikali yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa iliyo imara zaidi.

Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suliuhu Hassan kwa kuanzisha Kikosi Kazi, huku akibinisha umuhimu wa kuwa na kikosi kazi kidogo kitakachokuwa maalum kwa ajili ya kushughulikia changamoto zinazoikabili Zanzibar pekee.

Aidha, Dkt. Mwinyi aliunga mkono hatua ya NDI inayolenga kusaidia kuwainua kiuchumi wananchi, ikiwemo wakulima wa zao la mwani.

Naye Mtafiti kutoka Asasi za Kiraia ya JUWAUZA, Rashid Azizi, akichambua dhana ya Mradi wa Serikali ya umoja wa Kitaifa (GNU) na changamoto zilizopo, alisema utafiti umebainisha wananchi walio wengi nchini wanaunga mkono uwepo wa GNU.

Alisema, kwa mujibu w aamelezo ya wananchi uwepo wake umesaidia sana kuimarisha hali ya amani na umoja mongoni mwa Wazanzibari, huku wakipongeza hatua ya Rais Dk. Mwinyi ya kuweka utaratibu wa kutembelea nyumba za Ibada (misikiti) na kuhubiri umoja.

Azizi alibainisha baadhi ya mambo ambayo wananchi wanahisi kuwa ni changamoto katika GNU, ikiwemo upatikanaji wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, kwa kigezo kuwa wanachelewa kuvipata pamoja na kutolewa kwa misingi ya itikadi za kisiasa.

Alisema mchakato wa uchaguzi ni eneo jengine ambalo wn anachi wanaelezea kuwa lina changamoto na kubainisha umuhimu wa kuwepo uwazi tangu hatua za awali za uandikishaji.

Aidha, alisema wananchi walio wengi hususan wale walioko vijijini wamaelezea umuhimu wa kupatiwa huduma mbalimbali muhimu za kijamii.

Alisema upatikanaji wa ajira ni eneo ambalo wananchi wanalalamikia na kuishauri Serikali haja ya kuwepo mfumo unaozingatia weledi huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza nguvu katika usimamizi, kupitia mfumo wa Mtandao wa ZAN Ajira.

Kuhusiana na Uchumi wa Buluu, Mchambuzi huyo alisema wananachi wamependekeza kuongezewa thamani zao la Mwani kwani bei inayolipwa hivi sasa na Kampuni zinayojishughulisha na ununuzi wa zao hilo ni ndogo mno, huku wakilalamika kuwa baadhi ya wanunuzi hao kuwa hawaaminiki.

Post a Comment

0 Comments